· Maji yashindwa kuupanda na kutiririshwa nje mashindano SHIMIWI
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Tanga
Wimbo usemao Mungu
akipenda tutaonana tena baadaye leo tarehe 9 Octoba, 2022 ulitawala katika
Viwanja vya Shule ya Sekondari Galanos mara baada ya Timu ya Mahakama Sports
Mpira wa Miguu Wanaume kuyakausha Maji kwenye mashindano ya Shirikisho la
Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayofanyika jijini hapa.
Mahakama Sports iliichapa
Timu ya Maji mabao 5:3 kwa mikwaju ya matuta baada ya timu zote mbili kushindwa
kufungana katika muda wa kawaida. Hatua hiyo imeiwezesha Mahakama Sports
kutinga katika hatua ya robo fainali.
Mchezo huo ambao
umechezwa majira ya saa nane mchana ulianza kwa kasi huku timu zote mbili
zikishambuliana kwa zamu. Maji ndiyo waliokuwa wa kwanza kulisakama lango la
Mahakama, lakini beki yao ilikuwa makini na kuzuia hatari zote zilizokuwa
zinaelekezwa upande wao.
Baada ya dakika chache,
wachezaji wa Mahakama walitulia na kuanza kucheza pasi fupi fupi na kufanikiwa
kumiriki mpira muda wote. Hatua hiyo iliamsha shangwe za mashabiki wa Mahakama
Sports ambao waliishangilia timu yao muda wote wa mchezo huo.
Mahakama ilitengeneza
nafasi nyingi za kuweza kujipatia mabao, lakini wachezaji walishindwa kutumia
nafasi hizo katika vipindi vyote viwili. Kulikuwepo na zomea zomea na kejeli za
kimichezo za hapa na pale kutoka pande zote mbili, lakini
kandanda safi lililoonyeshwa na Mahakama Sports liliwanyamazisha mashabiki wa
timu pinzani.
Hadi mwamuzi anapuliza
kipenga kuashiria kumalizika kwa mpambamo huo timu zote zilikuwa zimetoshana
nguvu sawa. Baada ya mikwaju ya matuta kuamriwa kupigwa, Mahakama Sports ndiyo
iliyooanza kuukwamisha mpira kambani.
Katika upigaji huo,
Mahakama Sports ilipata mikwaju yote mitano na Maji wakaambulia mitatu baada ya Mdaka Mabomu wa Mahakama, Hassan Aufi kupangua mkwaju mmoja na kuwafanya timu
hiyo pinzani kuondoshwa kwenye mashindano hayo.
Mwalimu wa Timu hiyo
Spear Mbwembwe alishindwa kuzungumza chochote baada ya kumalizika kwa mchezo
huo kutokana na furaha kubwa aliyokuwa nayo. Katibu Mkuu wa Mahakama Sports
Robert Tende alisema vijana wake wameau Jitu jingine kwenye mashindano hayo.
"Timu ya Maji ndiyo
iliyokuwa inaogopwa kwenye mchezo huu. Tumewahukumu kifungo cha mwaka mmoja
kutokushiriki kwenye mashindano haya. Jalada la kesi hii limefungwa, tuonane
mwakani," Katibu huyo alitamba.
Kabla ya kufikia hatua
hiyo, Mahakama Sports Mpira wa Miguu ilishiriki kwenye mechi za makundi na
ilianza kwa kukutana na Timu ya Utumishi na kuisanua mabao mawili kwa nunge na
baadaye ikakutana na Hazina katika mechi ya pili na kupoteza kwa taaaabu kwa
mabao mawili kwa moja.
Katika mechi yake ya
tatu, Mahakama ilimenyana na Ukaguzi na kuwafumua kwa bao moja kwa yai na
baadaye ilifanya mauaji kwa kuishindilia timu ya Maendeleo ya Jamii kwa mabao
sita kwa moja.
Wachezaji wa Mpira wa
Miguu walioiwakilisha Mahakama katika michezo hiyo walikuwa Fahamu Kibona; Iman
Patson; Gisbert Chentro; Akida Mzee; Emmanuel Mwamole; Selemani Magawa; Frank
Obadia; Gabriel Tabana; Martin Mpanduzi; Mwinjuma Bwanga, Shamte Seif, Hassan
Aufi; Nassoro Mwampamba; Kelvin Rutalemwa; Shabiru Hood; David Mnubi; Beatus
Simwanza na Timoth Mwakisambwe.
Viongozi ambao
wameambatana na Timu ni Mwenyekiti Wilson Dede, Makamu Mwenyekiti Fidelis
Choka, Katibu Mkuu Robert Tende, Katibu Mkuu Msaidizi Theodosia Mwangoka, Mweka
Hazina Rajab Ally, Timu Meneja Antony Mfaume, Afisa Michezo Nkrumah Katagile na
Mjumbe Mwakilishi wa SHIMIWI Taifa Shaibu Kanyochole.
Mashindano ya SHIMIWI
ambayo yalianza tarehe 1 Octoba, 2022 na kufunguliwa rasmi tarehe 5 Octoba,
2022 yanafanyika katika viwanja tofauti tofauti ikiwemo Viwanja vya Mkwakwani,
Shule ya Sekondari Popatlal, Galanos Sekondari, Bandari, Shule ya Tanga, Polisi
Chumbageni na Viwanja vya Gymkhana kwa kuhusisha michezo kadhaa.
Sehemu nyingine ya mashabiki wa Timu ya Mahakama Sports (juu na chini) wakishangilia ushindi baada ya kuibandua Timu ya Maji kwenye mashindano.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni