·Wasalimu amri Mahakama Kamba Wanaume, Wanawake wakielekea robo fainali
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Tanga
Timu ya Mahakama ya
Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanaume na Wanawake imetinga katika hatua ya
robo fainali baada ya kutembeza kichapo kikali kwa wapinzani wao, TARURA na RAS Simiyu katika mashindano ya Shirikisho la Michezo
ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayofanyika jijini hapa.
Ulikuwa mchezo wa Kamba
Wanawake ulioanza kuchezwa majira ya saa nne asubuhi katika Viwanja vya Shule
ya Sekondari Usagala ambapo vijana wa Mahakama hawakutaka kuleta utani na mtu
na kuwakamata kisawasawa wapinzani wao ambao hawakupata nafasi yoyote ya
kupumua.
RAS Simiyu walijaribu
kujitutumua kwa sekunde kadhaa lakini wakaamua kukiri makosa mahakamani na kujikuta
maji waliyokuwa wanataka kuyaoga yameshafika shingoni na kukubali yaishe kwenye
mzunguko wa kwanza.
Kipindi cha pili hakikuwa
na ugumu wowote kwa Mahakama kwa jinsi walivyokuwa wamejipanga kuumaliza mchezo
huo bila kupoteza muda. Hadi mchezo unamalizika RAS Simiyu wakaondoka uwanjani
wakiwa vichwa chini, huku wakiiacha Mahakama Sports ikisherekea ushindi walioupata.
Baada ya mechi hiyo,
Kamba Wanaume ilifuata ambapo Mahakama Sports waliparurana na TARURA ambao
hawakutoa upinzani wowote kwa wababe wa mchezo huo. Wapinzani hao wa Mahakama
walijuta kujitokeza katika mchezo huo baada ya kupoteana katika mzunguko wa
kwanza.
Kama ilivyokuwa kwa dada zao,
Mahakama Sports Kamba wanaume walitembeza kichapo kitakatifu katika mzunguko wa
pili baada ya wapinzani wao nao kukiri makosa ya kushindana na Mahakama, hivyo
kuahidi Mungu akipenda watajaribu tena baadaye.
Kufuatia matokeo hayo,
Mahakama Sports Kamba Wanaume itakutana na Uchukuzi kwenye robo fainali.
Uchukuzi waliwango’oa kwenye mashidano hayo timu ya Maji huku Mahakama Sports
Wanawake ikikabiliana vilivyo na RAS Iringa ambao waliwatoa upepo Haki.
Akizungumza baada ya
mechi hizo, Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede amewapongeza vijana wake
kwa kutoa salamu kwa wapinzani kuwa hawana utani na mtu. Amesema mapambano bado
yanaendelea na watapambana mpaka mwisho kwani kilichowaleta Tanga kinajulikana.
"Sisi hatuna papara
na mtu kama walivyo wengine ambao wanakuja uwanjani na mikwara ya hapa na pale,
sijui wanamtisha nani. Ninawashangaa sana, unakuta mtu anapita na mikwara kututisha,
hivi wanaijua Mahakama hawa, nawaonea hurumia sana hawa," alisema.
Kabla ya kuingia kwenye
16 bora, Mahakama Sports ilikutana na timu zingine nne katika hatua ya makundi.
Kwa upande wa Wanaume, mechi ya kwanza Mahakama ilikutana na Haki ambayo
ilikamuliwa kisawaswa katika hatua zote. Mechi ya pili Mahakama iliwabana mbavu
Ikulu na baadaye wakaikaribisha RAS Singida ambao nao wakakumbana na kichapo
kikali kabla ya kuwanyonyoa RAS Dodoma.
Mahakama Sports Kamba
Wanawake ilimaliza mechi zake za makundi kwa kushinda zote na kufanya iongoze
kwenye kundi hilo. Ilicheza mechi yake ya kwanza ya makundi na RAS Singida
ambapo ilitoa kichapo kikali.
Mechi yake ya pili
ilikutana na Maji ambayo yalikamuliwa kisawasawa kwa mizunguko yote miwili na
katika mechi ya tatu ilipangiwa na RAS Manyara ambao waliingia mitini baada ya
kuogopa kupokea dozi iliyokuwa imeandaliwa kwa ajili yao. Mahakama Sports
ilikutana na Viwanda na kuisambaratisha vikali katika mechi yake ya nne.
Wachezaji wa Kamba
Wanawake ni Zahara Abdallah, Beatrice Dibogo, Judith Mwakyalagwe, Melina
Mwinuka, Dotto Mlandula, Rebecca Mwakabuba, Salma Mwamende, Sarafina Mkumbo,
Mariam Mayala, Zawadi Amir, Namweta Mcharo, Valeria Ntyangili, Anna Hebron,
Lucy Mbwaga, Rose Mwalongo na Tumaini Kizito.
Katika mchezo wa Kamba
Wanaume, Mahakama Sports inawakilishwa na Leonard Kazimzuri, Yuda Mgalla,
Patrick Mundwe, Denis Kipeta, Joseph Chokela, Mjuni Denis, Komba Mussa, Mochiwa
Marko, Abdul Mumini, Mushi Martin, Magesa Phabian, Emmanuel Datsan, Robert
Oguda, Rajab Mwaliko, Fidelis Choka na Exavery Kasembe.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni