Jumamosi, 8 Oktoba 2022

MAHAKAMA SPORTS YAANZA KUNYANYUA MAKWAPA SHIMIWI

Na Faustine Kapama-Mahakama, Tanga

Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) imeanza kukusanya makombe katika mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayofanyika jijini hapa baada ya mkimbiza upepo wake hatari, Atugonza Justa kufanya vizuri kwenye mchezo wa riadha mita 3,000 na kuwatimulia vumbi wapinzani wake.

Mwanariadha huyo wa Mahakama alishika nafasi ya kwanza kwenye mchezo huo uliofanyika majira ya asubuhi leo tarehe 8 Octoba, 2022 katika Viwanja vya Shule ya Ufundi Tanga na kuwaacha kwa mbali wapinzani wake kutoka katika taasisi mbalimbali zinazoshiriki katika mashindano hayo.

Kufuatia hatua hiyo, Mchezaji huyo wa Mahakama Sports anakuwa mshindi katika riadha mita 3,000 na kumfanya asubiri kukabidhiwa medali ya dhahabu na kikombe cha mshindi wa kwanza kwenye mchezo huo kwenye kilele cha mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika tarehe 15 Octoba, 2022.

Mbali na mchezo huo, Mahakama Sports pia ilishiriki katika mbio za mita 400 kwa Wanawake ambapo mchezaji wake Upendo Mapunda alifanikiwa kushikia nafasi ya tatu kwenye mechi ya makundi, hivyo kutinga katika hatua ya fainali.

Kadhalika, wafukuza upepo wa Mahakama, Atugonza Justa, Upendo Mapunda, Zamoyoni Komba na Filomena Haule walishiriki kwenye mchezo wa kupokezana vijiti na kushika nafasi ya tatu kwenye hatua ya makundi, hatua iliyowawezesha kufika fainali katika mchezo huo.

Kadhalika, wanamichezo wa Mahakama Sports, Gisbert Chentro, Frank Obadia, Martin Mpanduzi na John Masunga nao walishiriki katika mchezo huo wa kupokezana vijiti na kufanikiwa kukamata nafasi ya pili, hivyo kutinga katika fainali. Fainali zote hizo zinategemewa kufanyika leo tarehe 9 Octoba, 2022.

Mahakama Sports ambayo imeambatana na viongozi mbalimbali ipo jijini Tanga kushiriki katika mashindano ya SHIMIWI yaliyoanza tarehe 1 Octoba, 2022 na kufunguliwa rasmi tarehe 5 Octoba, 2022 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama.

Viongozi ambao wameambatana na Timu ni Mwenyekiti Wilson Dede, Makamu Mwenyekiti Fidelis Choka, Katibu Mkuu Robert Tende, Katibu Mkuu Msaidizi Theodosia Mwangoka, Mweka Hazina Rajab Ally, Timu Meneja Antony Mfaume, Afisa Michezo Nkrumah Katagile na Mjumbe Mwakilishi wa SHIMIWI Taifa Shaibu Kanyochole.

Mwamba Atugonza Justa, mshindi wa riadha mita 3,000.

Mwana Mahakama Sports Atugonza Justa akichanja mbuga kwenye mchezo wa riadha mita 3,000, huku akiwaacha washindani wake kwa mbali ajabu.


Mwana Mahakama Sports Atugonza Justa akikamilisha mbio za mita 3,000.
Mwana Mahakama Sports Atugonza Justa akiongozwa na Mwenyekiti wake Wilson Dede na Daktari wa Timu Jamari Mkumba kwenda kujiandikisha baada ya kuibuka mshindi wa kwanza kwenye mbio hizo.
Waamuzi wakichukua kumbukumbu kutoka kwa Mwamba Atugonza Justa.
Mwana Mahakama Sports Frank Obadia akijiandaa kuchomoka alipokuwa anashiriki katika mchezo wa kupokezana vijiti. Mahakama Sports ikishika nafasi ya pili na kutinga fainali. 
Mwana Mahakama Sports Gisbert Chentro akiwatimulia vumbi wapinzani wake alipokuwa anashiriki katika mchezo wa kupokezana vijiti. 
Mwana Mahakama Sports Gisbert Chentro akishangilia ushindi. Picha chini akipongezwa na wanamichezo wenzake.

Mwana Mahakama Sports Upendo Mapunda akijiandaa kuchomoka alipokuwa anashiriki mbio za mita 400. Upendo aliibuka mshindi wa tatu kwenye mechi za makundi na kutinga fainali.

Mwana Mahakama Sports Upendo Mapunda akikamilisha mbio za mita 400.
Mwamba Atugonza Justa akijiandikisha baada ya kushiriki kwenye mbio za kupokezana vijiti pamoja na wenzake na kufanikiwa kushika nafasi ya tatu kwenye makundi, hivyo kutinga fainali. Kulia kwake ni Katibu Mkuu wa Mahakama Sports Robert Tende na kulia kwake ni Upendo Mapunda.

Miamba ya mbio ndefu ikiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Mahakama Sports, Katibu Mkuu Msaidizi Theodosia Mwangoka (kulia) na Makamu Mwenyekiti Fidelis Choka (wa tatu kulia mstari wa nyuma). Kutoka kushoto ni John Masunga, Zamoyoni Komba, Atugonza Justa, Upendo Mapunda na Filomena Haule.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni