Na Faustine Kapama-Mahakama, Tanga
Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) imefanikiwa
kuingiza timu nne kwenye 16 bora baada ya kufanya vizuri kwenye hatua ya makundi
katika mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali
(SHIMIWI) yanayofanyika jijini hapa.
Timu hizo ni Kamba Wanaume, Kamba Wanawake, Netiboli
na Mpira wa Miguu Wanaume. Mahakama Sports Kamba Wanaume ilimaliza mechi za
kwenye makundi bila kupoteza mchezo wowote.
Katika mechi ya kwanza, Mahakama ilikutana na Haki
ambayo ilikamuliwa kisawaswa katika hatua zote. Mechi ya pili Mahakama
iliwabana mbavu Ikulu na baadaye wakaikaribisha RAS Singida ambao nao
wakakumbana na kichapo kikali kabla ya kuwanyonyoa RAS Dodoma.
Katika mchezo wa Kamba Wanaume, Mahakama Sports
inawakilishwa na Leonard Kazimzuri, Yuda Mgalla, Patrick Mundwe, Denis Kipeta,
Joseph Chokela, Mjuni Denis, Komba Mussa, Mochiwa Marko, Abdul Mumini, Mushi
Martin, Magesa Phabian, Emmanuel Datsan, Robert Oguda, Rajab Mwaliko, Fidelis
Choka na Exavery Kasembe.
Mahakama Sports Kamba Wanawake ilimaliza mechi zake za
makundi kwa kushinda zote na kufanya iongoze kwenye kundi hilo. Ilicheza mechi
yake ya kwanza ya makundi na RAS Singida ambapo ilitoa kichapo kikali.
Mechi yake ya pili ilikutana na Maji ambayo
yalikamuliwa kisawasawa kwa mizunguko yote miwili na katika mechi ya tatu
ilipangiwa na RAS Manyara ambao waliingia mitini baada ya kuogopa kupokea dozi
iliyokuwa imeandaliwa kwa ajili yao. Mahakama Sports ilikutana na Viwanda na
kuisambaratisha vikali katika mechi yake ya nne.
Wachezaji wa Kamba Wanawake ni Zahara Abdallah, Beatrice
Dibogo, Judith Mwakyalagwe, Melina Mwinuka, Dotto Mlandula, Rebecca Mwakabuba,
Salma Mwamende, Sarafina Mkumbo, Mariam Mayala, Zawadi Amir, Namweta Mcharo,
Valeria Ntyangili, Anna Hebron, Lucy Mbwaga, Rose Mwalongo na Tumaini Kizito.
Katika mechi za makundi, Mahakama Sports Netiboli ilianza
kwa kuiadhibu RAS Mtwara kwa vikapu 40:4 na baadaye kutoana jasho na Ujenzi kwa
kila timu kutupia vikapu 20. Baada ya hapo, Mahakama Sports ilikuta na Kilimo
na kuichanachana kwa vikapu 28:26 kabla ya kuwatoa kamasi Waziri Mkuu Kazi
baada ya kuwaadhibu kwa vikapu 25:23.
Wachezaji wanaoiwakilisha Mahakama Sports kwenye
mchezo huo wa Netiboli ni Filomena Haule, Upendo Mapunda, Nyangi Saimora,
Veronica Kajobi, Dianes Akanganyila, Shani Ally, Tarita Kayuni, Marikia Nondo,
Margaret Kanyaga, Agnes Kilian, Jackline Paul, Adeudata Mkonkosha, Sharifa
Selemani, Sophia Songoro, Taus Mwambujale, Agness Mwanyika na Kuruthum
Mkundawatu.
Kwa upande wa Mahakama Sports Mpira wa Miguu, timu
hiyo ilianza kwenye mechi za makundi kwa kukutana na Timu ya Utumishi na kuisanua
mabao mawili kwa nunge na baadaye ikakutana na Hazina katika mechi ya pili na
kupoteza kwa taaaabu kwa mabao mawili kwa moja. Katika mechi yake ya tatu, Mahakama
ilimenyana na Ukaguzi na kuwafumua kwa bao moja kwa yai na baadaye ilifanya mauaji
kwa kuishindilia timu ya Maendeleo ya Jamii kwa mabao sita kwa moja.
Wachezaji wa Mpira wa Miguu walioiwakilisha Mahakama
katika michezo hiyo walikuwa Fahamu Kibona; Iman Patson; Gisbert Chentro; Akida
Mzee; Emmanuel Mwamole; Selemani Magawa; Frank Obadia; Gabriel Tabana; Martin
Mpanduzi; Mwinjuma Bwanga, Shamte Seif, Hassan Aufi; Nassoro Mwampamba; Kelvin
Rutalemwa; Shabiru Hood; David Mnubi; Beatus Simwanza na Timoth Mwakisambwe.
Viongozi ambao wameambatana na Timu ni Mwenyekiti
Wilson Dede, Makamu Mwenyekiti Fidelis Choka, Katibu Mkuu Robert Tende, Katibu
Mkuu Msaidizi Theodosia Mwangoka, Mweka Hazina Rajab Ally, Timu Meneja Antony
Mfaume, Afisa Michezo Nkrumah Katagile na Mjumbe Mwakilishi wa SHIMIWI Taifa
Shaibu Kanyochole.
Mashindano ya SHIMIWI ambayo yalianza tarehe 1 Octoba,
2022 na kufunguliwa rasmi tarehe 5 Octoba, 2022 yanafanyika katika viwanja
tofauti tofauti ikiwemo Viwanja vya Mkwakwani, Shule ya Sekondari Popatlal,
Galanos Sekondari, Bandari, Shule ya Tanga, Polisi Chumbageni na Viwanja vya
Gymkhana kwa kuhusisha michezo kadhaa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni