Ijumaa, 7 Oktoba 2022

MAHAKAMA SPORTS YANYONGA MTU TANGA

·Baada ya kuwashindilia Maendeleo ya Jamii magori sita

Na Faustine Kapama-Mahakama, Tanga

Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Mpira wa Miguu Wanaume leo tarehe 7 Octoba, 2022 imetinga kibabe katika hatua ya 16 bora kwenye mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayofanyika jijini hapa baada ya kuwashindilia Maendeleo ya Jamii kwa magori 6:1.

Mchezo huo uliochezwa katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Galanosi majira ya saa tano asubuhi ulianza kwa kasi huku Mahakama Sports ikilisakama goli la wapinzani wao na kufanikiwa kupachika bao katika dakika ya kwanza ya mchezo huo kupitia kwa mshambuliaji wake hatari Martin Mapinduzi.

Mapinduzi alipokea pasi mpenyezo kutoka kwa mshambuliaji na Nahodha wa timu hiyo, Selemani Magawa kabla ya kufunga bao hilo. Dakika ya tatu baadaye katika kipindi hicho cha kwanza, mshambuliaji huyo huyo aliwainua mashabiki wa Mahakama Sports kwenye viti vyao baada ya kuiandikia timu yake bao la pili baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa winga wa kulia, Frank Odadia.

Baada ya kupachikwa kwa magori hayo, timu zote zilianza kushambuliana kwa zamu na katika dakika ya 15 Maendeleao ya Jamii wakafanikiwa kupata bao la kufutia machozi. Timu hiyo ililazimika kufanya mabadiliko ya haraka haraka katika dakika ya 20 baada ya kuzidiwa kimchezo na kufanikiwa kuwazuia Mahakama Sports kuendelea kulishambulia lango lao.

Hadi timu zote mbili zinaenda mapunziko, matokeo yalikuwa 2:1 kwa Mahakama na Maendeleo ya Jamii, mtawaliwa. Katika kipindi cha pili, Mahakama Sports ilifanya mabadiliko kadhaa ya wachezaji kwa kumtoa mfungaji wa mabao yote mawili ya mwanzo, Martin Mpanduzi na kumwingiza Timoth Mwakisambwe.

Mwalimu wa Timu hiyo Spear Mbwembwe pia alimbadilisha Shamte Seif na kumwingiza Beatus Simwanza na baadaye akamwingiza David Mnubi badala ya Gabriel Tabana. Mabadiliko hayo yalileta uhai kwenye timu ya Mahakama Sports ambao walikuwa wanalishambulia lango la wapinzani wao kama nyuki.

Katika dakika ya 50 ya mchezo, winga hatari Frank Obadia akafanikiwa kuweka mpira kwenye kamba kwa kichwa baada ya mlinda mlango wa timu ya Maendeleo ya Jamii kuutema mpira kufuatia shuti kali liliomshimnda ambalo lilichezwa na mshambuliaji, Beatus Simwanza. Bao hilo liliiwezesha Mahakama Sports kuongoza kwa mabao 3:1.

Kana kwamba haitoshi, Mahakama Sports ilizidisha mashambulizi ambapo mshambuliaji hatari, nahodha wa timu na mchezaji nyota wa mchezo huo, Selemani Magawa akafanikiwa kupachika bao safi kwa kichwa katika dakika ya 60, hivyo kuiandikia timu yake bao la nne.

Kufungwa kwa bao hilo kuliamsha ari ya wachezaji wa Mahakama Sports na kulisakama lango la timu pinzani mara kwa mara. Wachezaji wa Mahakama Sports walikosa magori mengi ya wazi kwa kushindwa kuwa watulivu, hasa wanapoingia kwenye miguu 18 karibu na lango la wapinzani wao.

Ilibidi mwalimu wao awatulize na kuanza kucheza pasi fupifupi, mbinu ambayo ikafanikisha Mahakama Sports kuingia tena kwenye kamba katika dakika ya 65 ya mchezo baada ya mchezaji wake Timoth Mwakisambwe anayechezea winga ya kushoto kuupachika mpira kwenye wavu na kuiandikia timu yake bao la tano baada ya kupokea pasi maridadi kutoka kwa Selemani Magawa.

Katika dakika za lala salama, mshambuliaji Beatus Simwanza aliunganisha pasi safi kutoka kwa Timoth Mwakisambwe na kuukwamisha mpira katika nyavu na kuiandikia timu yake bao la sita. Hadi mpira unamalizika, Mahakama Sports ilikuwa imevuna mabao sita, huku Maendeleo ya Jamii ikiambulia bao moja la kufutia machozi.

Akiongea baada ya mchezo huo, Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede aliwapongeza vijana wake kwa kupigana kufa na kupona na baadaye kupata ushindi mnono wa kalamu ya magori, ambayo hata wapinzani wao hawakutegemea kupata kipigo kikali kama hicho.

“Nimefurahishwa sana, na nadhani kila mmoja wetu amefurahishwa na matokeo haya. Ninawapongeza sana wachezaji wetu kwa kujituma na kucheza kitimu. Matokeo haya yanatuweka katika nafasi nzuri ya kuendelea kwenye hatua inayofuata, hongereni sana,” alisema.

Mwalimu Mbwembwe amewapongeza vijana wake kwa ushindi huo na kwa kazi nzuri waliyoifanya. “Nimefurahi, nimefurahi sana. Vijana wangu wamefanyia kazi yale niliyowaelekeza. Hawa jamaa (Maendeleo ya Jamii) wanabahati sana. Tulikuwa tunawapiga zaidi ya bao 10 hawa. Lakini tumshukuru Mungu hata kwa hiki tulichokipata, nawapa salamu wale watakaokumbana na sisi, wataumia,” alisema.

Wachezaji wa Mpira wa Miguu walioiwakilisha Mahakama katika mchezo huo walikuwa Fahamu Kibona; Iman Patson; Gisbert Chentro; Akida Mzee; Emmanuel Mwamole; Selemani Magawa; Frank Obadia; Gabriel Tabana; Martin Mpanduzi; Mwinjuma Bwanga, Shamte Seif, Hassan Aufi; Nassoro Mwampamba; Kelvin Rutalemwa; Shabiru Hood; David Mnubi; Beatus Simwanza na Timoth Mwakisambwe.

Viongozi ambao wameambatana na Timu ni Mwenyekiti Wilson Dede, Makamu Mwenyekiti Fidelis Choka, Katibu Mkuu Robert Tende, Katibu Mkuu Msaidizi Theodosia Mwangoka, Mweka Hazina Rajab Ally, Timu Meneja Antony Mfaume, Afisa Michezo Nkrumah Katagile na Mjumbe Mwakilishi wa SHIMIWI Taifa Shaibu Kanyochole.

Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Mpira wa Miguu Wanaume (juu) ikiwa katika picha ya pamoja kabla ya kumenyana na Maendeleo ya Jamii (chini).

Timu zote mbili zikipata maelekezo kutoka kwa viongozi kabla ya mpambano.
Mlinda mlango wa Timu ya Maendeleo ya Jamii aliwalaumu wachezaji wenzake baada ya kupachikwa bao kwenye lango lake, huku wachezaji wa Mahakama Sports na Maendeleo ya Jamii wakiusindikiza mpira ukiingia kwenye nyavu.
Mchezaji wa Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) akimlamba chenga mchezaji kutoka Timu ya Maendeleo ya Jamii.
Nahodha wa Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Selemani Magawa akiukwamisha mpira kwenye nyavu kwa kichwa kwenye lango la Timu ya Maendeleo ya Jamii, huku Mlinda Mlango wa timu hiyo akibaki ameduwaa.
Mashabiki wa Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) wakishangilia bao hilo.
Wachezaji wa Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) wakishangilia aina ya ushangiliaji wa Beki Kisiki wa Timu ya Simba, Henock Inonga.
Mchezaji wa Mahakama Sports akiokota mpira kwenye kamba baada ya timu yake kufunga bao la sita huku Mlinda mlango wa Timu ya Maendeleo ya Jamii akilalama akiwa chini.
Mashabiki wa Mahakama Sports wakiliamsha nje ya uwanja baada ya ushindi.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga, Mhe. Beda Nyaki (juu) akizungumza na wanamichezo wa Mahakama baada ya kumalizika kwa mchezo kati ya Mahakama Sports na Maendeleo ya Jamii. Chini ni sehemu ya wanamichezo hao.

Sehemu ya Watumishi wa Mahakama kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania, Tanga wakiongozwa na Naibu Msajili Beda Nyaki (wa pili kushoto waliosimama nyuma) wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kuitembelea kambi ya wanamichezo wa Mahakama wanaoshiriki katika mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni