Na Faustine Kapama-Mahakama, Tanga
Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Kamba
Wanawake leo tarehe 7 Octoba, 2022 imekamilisha mechi yake ya mwisho ya makundi
katika mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali
(SHIMIWI) yanayofanyika jijini hapa baada ya kuisambaratisha Timu ya Viwanda.
Mchezo huo uliochezwa majira ya saa moja asubuhi
katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagala ulianza kwa kasi ambapo Viwanda
walionekana kukamia, lakini wachezaji wa Mahakama walibaki kuwa watulivu muda
wote, huku wakiwasoma wapinzani wao.
Mchezo ulipoanza katika mzunguko wa kwanza, Mahakama
Sports hawakuwa na jambo jingine zaidi ya kutembeza kichapo kikali kwa mvuto
moja na kuwaacha wapinzani wao wakipoteana huku wakiugulia maumivu waliyoyapata.
Nusura timu ya Viwanda igomee kurudi uwanjani katika
mzunguko wa pili kufuatia kugalagazwa vibaya na mabingwa hao wa mchezo wa Kamba
Wanawake katika mashindano hayo ya SHIMIWI.
Kama ilivyodhaniwa hapo awali, mzunguko wa pili
ulipoanza timu ya Mahakama Sports haikuwa na huruma na mtu baada ya
kuwasambaratisha wapinzani wao kwa mara nyingine kwa mvuto mmoja pekee, hivyo
kujizolea pointi zote muhimu.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Mwenyekiti wa
Mahakama Sports Wilson Dede amewapongeza vijana wake kwa kuonyesha mchezo mzuri
na wa kiungwana baada ya kuwavuta wapinzani wao kistaarabu.
"Nimeuangalia mchezo huo vizuri. Ni huruma tu
ambayo imetumika kumaliza mchezo huu. Nina wasiwasi kwenye mechi zijazo
atavunjwa mbavu mtu hapa. Mahakama Sports Kamba Wanawake siyo timu ya kuchezea,
kaa nayo mbali, vinginevyo utaumia," alisema.
Mahakama Sports Kamba Wanawake imemaliza mechi zake za
makundi kwa kushinda zote na kufanya iongoze kwenye kundi hilo. Ilicheza mechi
yake ya kwanza ya makundi na RAS Singida ambapo ilitoa kichapo kikali.
Mechi yake ya pili ilikutana na Maji ambayo
yalikamuliwa kisawasawa kwa mizungo miwili na katika mechi ya tatu ilipangiwa
RAS Manyara ambao waliingia mitini baada ya kuogopa kupokea dozi iliyokuwa imeandaliwa
kwa ajili yao.
Wachezaji wa Kamba Wanawake ni Zahara Abdallah, Beatrice
Dibogo, Judith Mwakyalagwe, Melina Mwinuka, Dotto Mlandula, Rebecca Mwakabuba,
Salma Mwamende, Sarafina Mkumbo, Mariam Mayala, Zawadi Amir, Namweta Mcharo,
Valeria Ntyangili, Anna Hebron, Lucy Mbwaga, Rose Mwalongo na Tumaini Kizito.
Viongozi ambao wameambatana na Timu ni Mwenyekiti
Wilson Dede, Makamu Mwenyekiti Fidelis Choka, Katibu Mkuu Robert Tende, Katibu
Mkuu Msaidizi Theodosia Mwangoka, Mweka Hazina Rajab Ally, Timu Meneja Antony
Mfaume, Afisa Michezo Nkrumah Katagile na Mjumbe Mwakilishi wa SHIMIWI Taifa
Shaibu Kanyochole.
Mashindano ya SHIMIWI ambayo yalianza tarehe 1 Octoba, 2022 na kufunguliwa rasmi tarehe 5 Octoba, 2022 yanafanyika katika viwanja tofauti tofauti ikiwemo Viwanja vya Mkwakwani, Shule ya Sekondari Popatlal, Galanos Sekondari, Bandari, Shule ya Tanga, Polisi Chumbageni na Viwanja vya Gymkhana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni