Alhamisi, 6 Oktoba 2022

TIMU YA WAZIRI MKUU KAZI ULIMI NJE

·Baada ya kubanwa mbavu na Mahakama Sports Netiboli

Na Faustine Kapama-Mahakama, Tanga

Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Netiboli leo tarehe 6 Octoba, 2022 imeibamiza Timu ya Waziri Mkuu Kazi kwa vikapu 25:23 katika mechi ya mwisho ya makundi katika mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayofanyika jijini hapa.

Mchezo huo ambao umechezwa majira ya saa tano asubuhi katika Viwanja vya Polisi Chumbageni ulitawaliwa na kosa kosa za kutupia vikapu vya hapa na pale huku timu zote mbili zikishambuliana kwa zamu.

Ilikuwa Timu ya Mahakama Sports iliyofungua msululu wa kutupia vikapu ambapo wachezaji wake walilisakama lango la wapinzani wao kila mara. Hata hivyo, Timu ya Waziri Mkuu Kazi ilijitahidi kusawazisha mambo baada ya kupata vikapu kadhaa kwa kutumia makosa yaliyofanywa na Mahakama Sports.

Hadi timu zinaenda kwenye mapumziko, Mahakama Sports ilikuwa inaongoza kwa vikapu kadhaa. Kipindi cha pili kilipoanza, Timu ya Waziri Mkuu ililisakama lango la Mahakama Sports, hasa katika dakika za mwazo na kufanikiwa kutupia vikapu kadhaa, hatua iliyowafanya kuongoza kwenye mchezo huo.

Baada ya hapo, Mahakama Sports ilichachamaa na kuanza kumkimbiza mwizi kimya kimya na kufanikiwa kusawazisha vikapu ambavyo timu pinzani ilikuwa imetangulia kutupia na baadaye kupindua meza kwa kuwajaza wapinzani hao vikapu vya haraka haraka.

Kitendo hicho kiliwanyamazisha mashabiki wa Timu ya Waziri Mkuu Kazi waliokuwa wanashangilia kwa nguvu kila timu yao inapotupia kikapu.

Shangwe hizo zilihamia upande wa pili wa shilingi, yaani Mahakama Sports baada ya wachezaji wake kukonga nyoyo zao, hasa baada ya kutulia na kurudi kwenye mchezo na kulishambulia lango la Waziri Mkuu Kazi kama nyuki.

Hadi mechi inamalizika, ubao wa matokeo ulikuwa unasoma vikapu 25 kwa Mahakama Sports huku Timu ya Waziri Mkuu Kazi ikiambulia vikapu 23 ilivyovitupia kufuatia makosa ya wachezaji wa Mahakama Sports.

Akizungumza baada ya mechi hiyo, Mwalimu wa Timu Mtumwa Sululu aliwasifia wachezaji wa timu yake kwa kusahihisha makosa katika kipindi cha pili, kitendo kilichoichanganya timu pinzani na kuifanya ipoteane.

"Tunashukuru tumepata matokeo mazuri na kumaliza mechi zetu za makundi tukiwa katika nafasi nzuri. Kati ya mechi nne tumeshinda tatu na kutoka sululu mechi moja. Nawapongeza sana vijana wangu kwa kufanya vizuri,” alisema.

Katika mechi za makundi, Mahakama Sports ilianza kwa kuiadhibu RAS Mtwara kwa vikapu 40:4 na baadaye kutoana jasho na Ujenzi kwa kila timu kutupia vikapu 20. Baada ya hapo, Mahakama Sports ilikuta na Kilimo na kuichanachana kwa vikapu 28:26.

Wachezaji wanaoiwakilisha Mahakama Sports kwenye mchezo huo wa Netiboli ni Filomena Haule, Upendo Mapunda, Nyangi Saimora, Veronica Kajobi, Dianes Akanganyila, Shani Ally, Tarita Kayuni, Marikia Nondo, Margaret Kanyaga, Agnes Kilian, Jackline Paul, Adeudata Mkonkosha, Sharifa Selemani, Sophia Songoro, Taus Mwambujale, Agness Mwanyika na Kuruthum Mkundawatu.

Viongozi ambao wameambatana na Timu ni Mwenyekiti Wilson Dede, Makamu Mwenyekiti Fidelis Choka, Katibu Mkuu Robert Tende, Katibu Mkuu Msaidizi Theodosia Mwangoka, Mweka Hazina Rajab Ally, Timu Meneja Antony Mfaume, Afisa Michezo Nkrumah Katagile na Mjumbe Mwakilishi wa SHIMIWI Taifa Shaibu Kanyochole.

Mchezaji wa Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Netiboli akitupia mpira kwenye kikapu cha Timu wa Waziri Mkuu Kazi katika mechi iliyofanyika leo tarehe 6 Octoba, 2022 katika Viwanja vya Polisi Chumbageni jijini Tanga.

Mpira uliorushwa na mchezaji wa Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Netiboli ukitumbukia kwenye kikapu.

Mashabiki wa Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Netiboli wakishangilia kwa furaha baada ya kumalizika kwa mchezo huo na timu yao kuibuka kidedea.
Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Netiboli (juu na picha mbili chini) ikionyesha mchezo safi.



Wachezaji wa Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Netiboli (juu na chini) wakipashapasha kabla ya mchezo kuanza.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni