Na Faustine Kapama-Mahakama, Tanga
Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanaume leo tarehe 6 Octoba,2022 imekamilisha
mechi za makundi katika mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara
za Serikali (SHIMIWI) yanayofanyika jijini hapa baada ya kuinyonyoa Timu ya RAS
Dodoma kwa mivuto yote miwili.
Mchezo huo uliochezwa majira ya saa moja asubuhi
katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagala haukuwa na ugumu wowote kwa vile
wapinzani hao wa Mahakama walikuwa si lolote wala chochote. Walikuwa RAS Dodoma
waliokuwa wa kwanza kuingia uwanjani huku wakitamba kuwamaliza Mahakama.
Katika mzunguko wa kwanza, Mahakama hawakuwa na papara
ya mchezo ambapo RAS Dodoma walijaribu kujitutumua huku mashabiki wao
wakiwashangilia kwa nguvu na kuwapa motisha ili washinde mchezo huo, lakini
wakajikuta hawasogei hata nusu hatua.
Mahakamani iliwagandisha wapinzani wao kwa sekunde
kadhaa kabla ya kuwasasabua kwa mvuto mmoja pekee na kuwatoa katika mchezo, hivyo
kujizolea pointi zote katika mzunguko huo. Hatua hiyo ilipelekea mashabiki wa
RAS Dodoma kushona midomo yao na kubaki kimya muda wote.
Katika mzunguko wa pili,Timu ya Mahakama iliendelea na
mfumo huo huo wa uchezaji wa kutuliza kamba mkononi huku wakiwaachia wapinzani
wao kujitutumua na kujipa matumaini. Kama ilivyokuwa katika mzunguko wa kwanza,
Mahakama Sports iliumaliza mchezo huo kwa mvuto mmoja na kuiacha Timu ya RAS
Dodoma isiwe na cha kufanya.
Mahakama Sports Kamba Wanaume imemaliza mechi za kwenye makundi bila kupoteza mchezo wowote. Katika mechi ya kwanza, Mahakama ilikutana na Haki ambayo ilikamuliwa kisawaswa katika hatua zote. Mechi ya pili waliikaribisha RAS Singida ambao nao wakakumbana na kichapo kikali kabla ya kuwabana mbavu Ikulu kwenye mizunguko yote miwili.
Katika mchezo wa Kamba wanaume, Mahakama Sports inawakilishwa
na Leonard Kazimzuri, Yuda Mgalla, Patrick Mundwe, Denis Kipeta, Joseph
Chokela, Mjuni Denis, Komba Mussa, Mochiwa Marko, Abdul Mumini, Mushi Martin,
Magesa Phabian, Emmanuel Datsan, Robert Oguda, Rajab Mwaliko, Fidelis Choka na
Exavery Kasembe.
Viongozi ambao wameambatana na Timu ni Mwenyekiti
Wilson Dede, Makamu Mwenyekiti Fidelis Choka, Katibu Mkuu Robert Tende, Katibu
Mkuu Msaidizi Theodosia Mwangoka, Mweka Hazina Rajab Ally, Timu Meneja Antony
Mfaume, Afisa Michezo Nkrumah Katagile na Mjumbe Mwakilishi wa SHIMIWI Taifa
Shaibu Kanyochole.
Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanaume kabla ya mechi.
Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanaume (juu) pamoja na Timu ya RAS Dodoma zikijiweka sawa kabla ya mechi kuanza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni