Jumatano, 5 Oktoba 2022

MAHAKAMA SPORTS NETIBOLI USIPIME

 ·Yamchanachana mtu mbele ya Waziri Mhagama

Na Faustine Kapama-Mahakama, Tanga

Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Netiboli leo tarehe 5 Octoba, 2022 imeichanachana Timu ya Kilimo na baadaye kuishindilia vikapu 28:26 katika ufunguzi rasmi wa mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayofanyika jijini hapa.

Mchezo huo ambao umechezwa katika Viwanja vya Bandari baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama kufungua mashindano hayo ulianza majira ya mchana kwa kasi huku timu zote zikishambuliana kwa zamu.

Timu ya Kilimo ilikuwa ya kwanza kubahatisha kutupia vikapu kwenye lango la Mahakama. Muda mchache baadaye, Mahakama Sports walijibu mapigo na kuanza kulishambulia lango la wapinzani wao kama nyuki na kuwafanya wapoteane, hivyo kufanikiwa kutupia vikapu kadhaa.

Mchezo huo ambao ulichezwa kwa dakika 40 ulivutia mashabiki wengi katika mashindano hayo ambapo baadhi ya timu pinzani ambazo tayari zimeshagalagazwa na Mahakama Sports kwenye michezo mbalimbali zilijitahidi kuishangilia timu ya Kilimo ili kuweza kuipa nguvu.

Hata hivyo, pamoja na janja janja hizo, wachezaji wa Mahakama Sports waliunyamazisha umati wa washangiliaji wa timu pinzani baada ya kuendeleza kichapo cha hapa na pale na kufanikiwa kujizolea kapu la magori katika mpambano huo.

Wachezaji wa Mahakama Sports wanaoshiriki kwenye mashindano ya SHIMIWI katika michezo mingine walitunishiana misuri na mashabiki wa timu pinzani katika kushangilia timu zao na kufanikiwa kuwanyamazisha licha ya uchache wao, hasa baada ya Mahakama kucheza kwa kujiamini na kwa ubora wa hali ya juu.

Hadi timu zinaenda mapumziko, Kilimo walikuwa wanaoongoza kwa idadi ndogo ya vikapu. Kipindi cha pili kilipoanza, Mahakama Sports ikazidisha mashambulizi na kulisakama lango la wapinzani wao mara kwa mara huku wakitupia tupia vikapu kadri wanapofika kwenye eneo la timu hiyo.

Juhudi za wachezaji wa Mahakama za kuongeza mashambulizi na umakini katika mchezo zililipa na hadi mechi hiyo inamalizika ikafanikiwa kuondoka na ushindi wa vikapu hivyo 28 kwa 26 walizoambulia Kilimo, ambao hawakuamini kabisa kile kilichotokea, licha ya kupata kuungwa mkono na taasisi zingine marafiki kwenye ushangiliaji.

Akizungumza baada ya mechi hiyo, Mwalimu wa Timu Mtumwa Sululu amewapongeza wachezaji wa timu yake kwa kuendeleza vichapo kwenye mashindano hayo na ameahidi timu itakayokumbana nayo huko mbele ya safari itakumbana na kichapo kikali zaidi.

"Nawapongeza sana vijana wangu kwa ushindi huu, kwa kweli wamecheza vizuri ingawa mechi ilikuwa ngumu kiasi chake maana inaonekana wapinzani wetu walikuwa wametukamia sana. Lakini wachezaji wangu wamesimama imara kabisa katika kuitetea timu yao na hatimaye wameibuka na ushindi," alisema.

Kabla ya kuanza kwa mchezo huo, Waziri Mhakama alizikagua timu zilioshiriki kwenye ufunguzi huo na kuzitakia heri katika mashindano hayo.

Wachezaji wanaoiwakilisha Mahakama Sports kwenye mchezo huo wa Netiboli ni Filomena Haule, Upendo Mapunda, Nyangi Saimora, Veronica Kajobi, Dianes Akanganyila, Shani Ally, Tarita Kayuni, Marikia Nondo, Margaret Kanyaga, Agnes Kilian, Jackline Paul, Adeudata Mkonkosha, Sharifa Selemani, Sophia Songoro, Taus Mwambujale, Agness Mwanyika na Kuruthum Mkundawatu.

Viongozi ambao wameambatana na Timu ni Mwenyekiti Wilson Dede, Makamu Mwenyekiti Fidelis Choka, Katibu Mkuu Robert Tende, Katibu Mkuu Msaidizi Theodosia Mwangoka, Mweka Hazina Rajab Ally, Timu Meneja Antony Mfaume, Afisa Michezo Nkrumah Katagile na Mjumbe Mwakilishi wa SHIMIWI Taifa Shaibu Kanyochole.

Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Netiboli wakimsubiri Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama kwa ajili ya utambulisho kabla ya kumenyana na Timu ya Kilimo.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama akifanya ukaguzi wa Timu ya Mahakama Sports Netiboli kabla ya kumenyana na Timu ya Kilimo. Katika picha, Katibu Mkuu Msaidizi wa Mahakama Sports Theodosia Mwangoka akimtambulisha Nahodha wa Timu hiyo, Nyangi Saimora.

Nahodha wa Timu ya Mahakama Sports Netiboli Nyangi Saimora akimtambulisha Mjumbe Mwakilishi wa SHIMIWI Taifa Shaibu Kanyochole kwa Waziri Mhagama.
Makamu Mwenyekiti wa Mahakama Sports Fidelis Choka akisalimiana na Waziri Mhagama wakati wa ukaguzi huo.
Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede akiteta jambo na Waziri Mhagama.
 Nahodha wa Timu ya Mahakama Sports Netiboli Nyangi Saimora akimtambulisha kwa Waziri Mhagama Meneja Vifaa  Teresia Mogani.

Nahodha wa Timu ya Mahakama Sports Netiboli Nyangi Saimora akiendelea na utambulisho (picha ya juu na mbili chini).


Mchezaji  wa Mahakama Sports Netiboli Shani Ally akimnong'oneza kitu Waziri Mhagama.
Nahodha wa Timu ya Mahakama Sports Netiboli Nyangi Saimora (juu na chini) akiendelea na utambulisho.



Timu ya Mahakama Sports ikiwa katika picha ya pamoja baada ya ufunguzi wa mashindano ya SHIMIWI.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni