Jumatano, 5 Oktoba 2022

WAZIRI MHAGAMA APALILIA NYONGEZA YA MUDA MASHINDANO YA SHIMIWI

Na Faustine Kapama-Mahakama, Tanga

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama leo tarehe 5 Octoba, 2022 amefugua rasmi mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayofanyika jijini hapa na kutoa wito kwa uongozi wa shirikisho hilo kukutana na Serikali ili kujadili njia bora, ikiwemo ongezeko la muda wa ushiriki katika mashindano.

Akizungumza katika Uwanja wa Mkwakwani baada ya kupokea maandamano ya wanamichezo kutoka taasisi mbalimbali wanaoshiriki katika michezo hiyo, Waziri Mhagama alisema kuwa watumishi wa umma wakipata muda mrefu wa kucheza wataweza kuonyesha umahiri na vipaji walivyonavyo, hivyo kuchangia upatikanaji wa wachezaji wazuri katika ngazi ya vilabu na taifa kwa ujumla.

“Naomba kutoa wito kwa SHIMIWI, washiriki wa michezo wanaongezeka, timu zinaongezeka, hebu tukae na Serikali tujadili, naona huko mbele inatupasa kuongeza muda wa uwepo wa michezo hii, kwani muda uliopo hautoshi. Tungependa kuona watumishi wa umma wanapata nafasi ya kucheza, lakini siyo kucheza tu, wanaonyesha umahiri na vipaji vyao ili mwisho wa siku tuache kuagiza (wachezaji nje), tunataka wawe watumishi wa umma hapa nchini,” alisema.

Waziri Mhagama alisema kuwa uwepo wa muda wa kutosha katika kushiriki kwenye mashindano hayo kutayafanya yawe na tija na kusaidia nchi kuwa na timu bora ambazo zinaweza kushindana kwenye medani za kitaifa kutoka katika wafanyakazi au watumishi wa umma nchini.

“Napenda kuishukuru Wizara ya Utamaduni na Michezo kwa kusimamia utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kuhakikisha michezo inadumishwa nchini na wananchi wote Tanzania, wakiwemo watumishi wote wa umma, wanapata fursa ya kushiriki, hivyo kujikinga na maradhi yasiyoambukiza kupitia michezo,” alisema.

Waziri huyo akatoa wito kwa SHIMIWI kuandaa programu maalumu ya mashindano itakayoshirikisha Wizara mbalimbali kushindana kila mwezi jijini Dodoma ili kuendeleza michezo, hatua itakayosaidia kuinua ari ya watumishi wa umma kufanya mazoezi kila siku na kujiandaa na ratiba ya michezo ya kila mwezi.

Kadhalika, Waziri Mhagama aliishauri SHIMIWI kuwa karibu na vyama vya michezo ambavyo vinautalaamu wa kutosha ili kusaidia kupata ubobezi katika medani za michezo ya namna mbalimbali ambayo wamekuwa wakishiriki.

Alitumia nafasi hiyo kuwaagiza waajiri wote kutoa ruhusa kwa watumishi kwa ajili ya kujiandaa na mashindano hayo kwani kuja kwenye mashindano ni jambo moja na maandalizi ni jambo jingine na wala haipendezi kwa mwanamichezo kuja kwenye mashindano bila kujiandaa.

Aidha, aliwakumbusha watumishi hao kuongozwa na maadaili ya utumishi wa umma kwani suala hilo siyo la mjadala wala hiari. Akawataka kufuata taratibu za utumishi wa umma na kuhakikisha kila mmoja wao anazingatia sheria na taratibu zilizowekwa na shirikisho.

Waziri huyo aliwapongeza wakuu wa taasisi za umma na wakala wa serikali kwa kuwaruhusu wachezaji kufanya maandalizi na kuja kushiriki kwenye michezo hiyo kwani ameshuhudia watumishi wakiwa wamewezeshwa kusafiri, kupata stahili na stahiki za kujikimu kwa kipindi chote watakapokuwa Tanga.

“Tumeshuhudia taasisi zilizoweza kuwawezesha wanamichezo kupata mavazi nadhifu ya michezo na leo uwanja umependeza sana. Nitoe wito kwa taasisi ambazo hazijajiandaa vizuri mwakani zijitahidi kufanya hivyo,” alisema.

Awali, akizungumza katika halfa hiyo, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Pauline Gekul aliwapongeza wanamichezo wote kwa kuonyesha utayari wa kushiriki kwenye michezo hiyo. Alitoa rai michezo hiyo kuendeshwa kwa weledi na nidhamu ya hali ya juu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

“Michezo ni undugu, michezo ni afya na michezo ni ajira. Ninaamini kwamba tutakapoondoka hapa Tanga tutakuwa tumeboresha haya yote na ni azma ya Rais ambaye ameridhia tuendelee na michezo hii,” alisema.

Aliwakumbusha wanamichezo kuwa michezo ni taaluma ambayo inahitaji nidhamu na weledi kama zilivyo taaluma zingine, hivyo ni imani yake michezo hiyo itakuwa chachu ya upendo, mshikamano, amani na umoja kwa watumishi wote na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa SHIMIWI Daniel Mwalusamba alimwambia Waziri Mhagama kuwa michezo ya mwaka huu (2022) imekuwa na mwitikio mkubwa ukilinganisha na mwaka jana (2021). Alisema kuwa mwaka jana timu 47 zilishiriki kwenye michezo hiyo iliyofanyika mkoani Morogoro.

“Lakini mwaka huu timu zinazoshiriki ni 63, mwaka jana ni mikoa 11 ilishiriki kwenye mashindano haya pale Morogoro, mwaka huu ni mikoa 18 inashiriki kwenye mashindano haya. Tunawashukuru viongozi wa mikoa kwa kuwa na mwitikio na kuongeza ushiriki wa watumishi kutoka kwenye mikoa yao,” alisema.

Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) inashiriki katika mashindano ya SHIMIWI kwenye michezo nane ambayo ni Kamba Wanaume na Wanawake, Mpira wa Miguu Wanaume, Netiboli, Bao, Karata, Tufe, Riadha Wanaume na Wanawake pamoja na Baiskeli na tayari imeshaanza kutembeza vipigo kwenye baadhi ya michezo hiyo kwenye hatua ya makundi.

Viongozi ambao wameambatana na Timu ni Mwenyekiti Wilson Dede, Makamu Mwenyekiti Fidelis Choka, Katibu Mkuu Robert Tende, Katibu Mkuu Msaidizi Theodosia Mwangoka, Mweka Hazina Rajab Ally, Timu Meneja Antony Mfaume, Afisa Michezo Nkrumah Katagile na Mjumbe Mwakilishi wa SHIMIWI Taifa Shaibu Kanyochole.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayofanyika jijini Tanga.
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Pauline Gekul akitoa salamu katika ufunguzi wa mashindano hayo.
Mwenyekiti wa SHIMIWI Daniel Mwalusamba akisisitiza jambo wakati wa ufunguzi huo.
Sehemu ya wanamichezo wa Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports)wanaoshiriki katika mashindano ya SHIMIWI (juu na chini) ikipita mbele ya Waziri Mhagama ndani ya uwanja wa Mkwakwani Tanga.

Sehemu nyingine ya wanamichezo wa Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports)wanaoshiriki katika mashindano ya SHIMIWI (juu na chini) ikipita mbele ya Waziri Mhagama ndani ya uwanja wa Mkwakwani Tanga.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama (katikati) akiwapungia mikono wanamichezo wa Mahakama Sports (picha juu na Tume ya Utumishi ya Mahakama (chini).
Sehemu ya watumishi wa Tume ya Utumishi ya Mahakama ya Tanzania ikiingia ndani ya Uwanja wa Mkwakwani Tanga.

Sehemu ya wanamichezo wa Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports)wanaoshiriki katika mashindano ya SHIMIWI (picha mbili juu na moja chini) ikielekea katika Uwanja wa Mkwakwani Tanga kushiriki katika ufunguzi wa Mashindani ya SHIMIWI.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni