Jumanne, 4 Oktoba 2022

MAHAKAMA SPORTS MPIRA WA MIGUU, NETIBOLI ZATAKATA SHIMIWI

 Na Faustine Kapama-Mahakama, Tanga

Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Mpira wa Miguu Wanaume na Netiboli leo tarehe 4 Octoba, 2022 zimetakata katika mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayofanyika jijini hapa baada ya kufanya vizuri kwenye michezo waliyocheza.

Timu ya Mpira wa Miguu iliwapapasa Timu ya Ukaguzi kwa bao moja kwa nunge, huku Netiboli ikiwatoa jasho Timu ya Ujenzi baada ya kutoshana nguvu kwa kila timu kutupia vikapu 20.

Ilikuwa mechi ya Netiboli iliyoanza kuchezwa majira ya saa tisa alasiri katika Viwanja vya Polisi Chumbageni ambapo kila timu ilionyesha kumkamia mwenzake. Ujenzi walianza mchezo kwa kasi na  kutupia tupia kwenye lango la Mahakama.

Hata hivyo, Mahakama ikaja juu baada ya dakika chache na kuanza kulisakama lango la wapinzani wao huku wakijaza kapu la magori kila baada ya dakika. Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Ujenzi walikuwa wameitangulia Mahakama kwa kikapu kimoja tu.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo Mahakama ilifungulia msululu wa vikapu na kuweza kuwafunika wapinzani wao, ambao nao walikuwa wakijibu kila kichapo walichokuwa wanakipokea. Hadi mchezo unamalizika, kila timu ilikuwa imeshatupia vikapu 20:20.

Akizungumza baada ya mechi hiyo, Mwalimu wa Timu Mtumwa Sululu aliwapongeza vijana wake kwa kupambana na kujituma muda wote kama alivyowaelekeza, hivyo kupata matokeo mazuri katika mchezo huo.

“Hawa wenzetu walidhani Mahakama ni mdebwedo, tumewaonyesha kazi na wanabahati sana. Walikuwa wanapumulia mashine hawa, niliwaona viongozi wao muda wote walikuwa wanaomba mechi iishe, tulishawakamata kisawasawa. Mchezo huu umeisha, tunajipanga kwa mechi nyingine,” alisema.

 

Baada ya mechi hiyo kumalizika, mzuka ukahamia kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari ya Galanosi ambapo Mahakama Sports Mpira wa Miguu Wanaume ilikuwa ikipepetana na Ukaguzi.

Mchezo huo ulianza majira ya saa kumi jioni kwa kasi, huku Mahakama ikilishambulia lango la wapinzani wao kama nyuki. Juhudi hizo zilizaa matunda katika dakika ya kumi tu ya mchezo ambapo kiungo mkabaji Selemani Magawa alikukwamisha mpira wavuni na kuuandikia timu yake bao la kuongoza.

Baada ya kupachikwa bao hilo, timu zote zilishambuliana kwa zamu na kulikuwepo na kosa kosa za magori za hapa na pale. Hadi timu zinaenda mapumziko, ubao wa matangazo ulikuwa unasoma mabao 1:0 kwa Mahakama na Ukaguzi, mtawaliwa.

Timu zote mbili zilifanya mabadiliko ya wachezaji kadhaa katika kipindi cha pili huku zikiwa zinashambuliana kwa zamu. Gori hilo la Mahakama lilidumu hadi mwisho wa mchezo na kuiwezesha timu hiyo kujizolea pointi zote tatu muhimu katika mashindano hayo.

Akiongea baada ya mchezo huo, Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede amesema Mahakama Sports haitapoa hata siku moja mpaka ushindi upatikane. “Tumesema tangu mwanzo kuwa tutakuwa tunatoa dozi ya kutwa mara tatu. Nadhani umesikia kilichotokea leo asubuhi pale viwanja vya Usagala, mchana Polisi Chumbageni tumewatoa kamasi watu, hapa napo tumewafumua kwa bao moja, hiyo siyo dozi! Hizi ni mvua za rasharasha tu, masika yanakuna,” alisema.

Mwalimu wa Timu Spear Mbwembwe amewapongeza vijana wake kwa ushindi huo na kwa kazi nzuri waliyoifanya. Amewataka wachezaji wake kujipanga vilivyo kwenye mechi inayofuata. “Jamani, bado hatujamaliza. Najua tunakamiwa sana, lakini sisi mwendo wetu ni ule ule wa kutoa dozi takatifu kama hizi tulizotoa leo. Tutaendelea na dozi hizi mpaka mwisho wa mashindano,” alisema.

Wachezaji walioiwakilisha Mahakama katika mchezo wa Netiboli walikuwa Filomena Haule, Upendo Matunda, Nyange Simola, Veronica Kajobi, Diane's Akanganyila, Shani Ally, Tarita Kayuni. Wachezaji wa akiba walikuwa Marikia Nondo, Margaret Kanyaga, Agnes Kilian,Jackline Paul, Adeudata Mkonkosha.

Kwa upande wa Mpira wa Miguu, wachezaji wa Mahakama walikuwa Fahamu Kibona; Iman Patson; Gisbert Chentro; Akida Mzee; Emmanuel Mwamole; Selemani Magawa; Frank Obadia; Gabriel Tabana; Martin Mpanduzi; Mwinjuma Bwanga, Shamte Seif, Hassan Aufi; Nassoro Mwampamba; Kelvin Rutalemwa; Shabiru Hood na Beatus Simwanza.

Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uiso, ambaye pia ndiye mlezi wa Mahakama Sports leo amekutana na wanamichezo wote wa Mahakama wanaoshiriki katika mashindano ya SHIMIWI na kuwapongeza kwa kazi nzuri wanayofanya, hususani ushindi wanaoupata kwenye michezo mbalimbali.

“Taarifa zenu ninazo, Mwenyekiti wenu amenipa taarifa ya kile kinachoendekea, niwapongeze sana kwa kazi nzuri mnayofanya na mimi nawatakia kila heri ili mpate ushindi kwenye michezo yote,” alisema.

Viongozi ambao wameambatana na Timu ni Mwenyekiti Wilson Dede, Makamu Mwenyekiti Fidelis Choka, Katibu Mkuu Robert Tende, Katibu Mkuu Msaidizi Theodosia Mwangoka, Mweka Hazina Rajab Ally, Timu Meneja Antony Mfaume, Afisa Michezo Nkrumah Katagile na Mjumbe Mwakilishi wa SHIMIWI Taifa Shaibu Kanyochole.

Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Netiboli kabla ya mchezo.
Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Mpira wa Miguu Wanaume kabla ya mchezo.
Mchezaji wa Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Netiboli akitumbukiza kikapu kwenye gori la Timu ya Ujenzi.
Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) ikishangilia baada ya mechi ya Netiboli kumalizika.
Gorikipa wa Timu ya Ukaguzi akilamba nyasi baada ya kutobolewa gori moja na Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Mpira wa Miguu Wanaume.
Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) ikishangilia baada ya mchezo wa mpira wa miguu wanaume kumalizika.
Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uiso (aliyevaa kofia) akizungumza na wanamichezo wa Mahakama.
Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uiso (aliyevaa kofia) akiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa Timu ya Netiboli.
Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uiso (aliyevaa kofia) akiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa Timu ya Mpira wa Miguu Wanaume.
Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uiso (aliyevaa kofia) akiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa Timu ya Kamba Wanawake.

Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Erasmus Uiso (aliyevaa kofia) akiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa Timu ya Kamba Wanaume.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni