Na Tiganya Vincent-Mahakama ya Tanzania
Mahakama
ya Tanzania imeanzisha namba maalum kwa ajili ya upokeaji wa taarifa na utoaji
wa elimu sahihi kwa wananchi ili kupunguza na kuondoa migogoro inayotokana na
masuala ya mirathi.
Akizungumza
leo tarehe 04 Oktoba, 2022 ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amesema Mahakama imeamua
kuongeza mifumo ya utoaji wa taarifa na elimu kwa wananchi katika eneo la
mirathi baada ya kuona watu wengi wanakosa haki zao kwa sababu ya kutokuwa na
elimu na taarifa sahihi.
Amesema
taarifa na elimu hiyo inatolewa saa 24 mwaka mzima kupitia namba maalum ya 0739 502 401 na barua pepe ambayo ni ccamirathi@judiciary.go.tz ambapo wananchi
wapata fursa ya kuuliza maswali na kufuatilia masuala ya mirathi.
Prof.
Ole Gabriel ameongeza kuwa, huduma hiyo imeanzishwa kupitia Kituo cha Mrejesho
wa Taarifa (Call Center) cha Mahakama ili kuwawezesha wananchi kupata taarifa
kwa haraka na uongozi wa Mahakama kupata mrejesho wa jinsi wateja
wanavyohudumiwa katika eneo la mirathi.
“Masuala
ya mirathi yanawasumbua wananchi wengi wakiwemo wanawake wanapata shida sana na
ndio maana kupitia Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Juma tumeamua kuja
na mfumo utakaosaidia kutoa taarifa na elimu sahihi ya jinsi ya kushughulikia
masuala ya mirathi. Mfumo huu utasaidia kuondoa vishoka na baadhi ya watu wachache
ambao sio waaminifu wanaodhulumu haki za wananchi kwa sababu ya kutokuwa na
elimu sahihi,” amesisitiza.
Aliongeza
wananchi wanayo fursa pia ya kupata elimu kuhusu masuala ya mirathi kupitia
barua pepe na namba hiyo wakati wowote.
“Tunawaomba
wananchi waweze kuitumia namba hiyo na barua pepe hiyo kutoa taarifa sahihi ili
tuweze kuwahuduma kwa wakati na wawe na muda wa kutosha katika kutekeleza
shughuli nyingine za maendeleo,” amesema.
Prof.
Ole Gabriel ameongeza kuwa, uanzishwaji wa huduma hii ni mwendelezo wa Mahakama
katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa uboreshaji wa huduma za Mahakama
ikiwemo utawala bora, uwazi na tija katika mnyororo wa utoaji haki kwa
wananchi.
Amesema,
huduma hii ina lengo la kuondoa vishoka na watu wengine ambao sio waaminifu
ambayo wamekuwa wakiwaumiza wananchi wanaofuatilia masuala ya mirathi ambao
hawana taarifa na elimu sahihi kuhusu jinsi ya kufuatilia masuala ya mirathi.
Huu
ni mfumo wa pili kuwa ndani ya Kituo cha Huduma kwa Mteja (Call Center) cha
Mahakama ya Tanzania ikitanguliwa na ule wa kutoa maoni na malalamiko kupitia
namba 0752 500 400.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel
akizungumza na Waandishi wa Habari leo tarehe 04 Oktoba, 2022 ofisini kwake jijini Dar es Salaam, kuhusu uanzishwaji wa namba maalum ya utoaji wa huduma
elimu na taarifa za ufuatiliaji wa masuala ya mirathi ya 0739 502 401.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akizungumza leo tarehe 4 Oktoba , 2022 na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam ,kuhusu uanzishwaji wa namba maalum ya utoaji wa huduma elimu na taarifa za ufuatiliaji wa masuala ya mirathi ya 0739 502 401.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni