Jumanne, 4 Oktoba 2022

JITU LIMEKUFA SHIMIWI TANGA

·Baada ya Mahakama kuwabamiza Ikulu

·Kamba Wanawake yatisha, RAS Manyara wakimbia

Na Faustine Kapama-Mahakama, Tanga

Usemi usemao usicheze na Mahakama utaumia umejidhihirisha leo tarehe 4 Octoba, 2022 katika mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayofanyika jijini hapa baada ya Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanaume kuwabamiza bila huruma Ikulu.

Mchezo huo uliovutia washiriki wa mashindano hayo karibia wote kutoka taasisi mbalimbali za Serikali ulichezwa majira ya saa moja asubuhi katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagala, huku zomea zomea kutoka kwa mashabiki wa pande zote mbili ikichagiza mchezo huo.

Ikulu waliingia uwanjani kwa kujiamini na kuikejeli Mahakama kuwa safari hii haichomoi, huku wakihamasishana kwa kuimba "Ilete Mahakama, ilete Mahakama,” ili kuumaliza mchezo huo dakika za awali. Kitendo hicho kiliibua shangilia shangilia za hapa na pale uwanjani hapo.

Hata hivyo, wachezaji wa Mahakama walibaki kimya na watulivu huku wakiwasoma wapinzani wao jinsi watakavyoanza mpambano huo. Mchezo ulipooanza Ikulu wakadaka kamba kwa kasi na kuwatikisa Mahakama kwa sekunde kadhaa. Lakini walijikuta wakigonga mwamba baada ya Mahakama kuwaonyesha 'mtu kazi' na kuwagalagaza vibaya.

Tukio hilo lilisababisha kibao kugeuka na uwanja mzima ukalipuka kwa furaha baada ya kukamilika kwa hatua ya kwanza ambapo Ikulu walionekana kuchanganyikiwa na wakaanza kulaumiana kwa kushindwa kutimiza ndoto yao ya mchana waliyoota.

Baadaye ikaanza minong'ono ya hapa na pale kutoka kwa mashabiki huku wakiisifia Mahakama. "Hawa jamaa wameshindikana, lakini ngoja tusubiri hatua ya pili tuone itakuwaje," alisikika shabiki mmoja akisema.

Hatua hiyo ya pili ilianza kwa kupokelewa na wimbo kutoka kwa wanamichezo mbalimbali waliokuwa wakiimba, " walete Ikulu, walete ikulu, walete Ikulu" na Mahakama haikuwa na cha kufanya zaidi ya kutembeza kuchapo cha mbwa koko na kuwakamua kisawasawa Ikulu ambao walijikuta wakilamba nyasi bila wao kutegemea.

Ikulu waliondoka katika Viwanja hivyo wakiwa vichwa chini, huku wakisindikizwa kwa wimbo maarufu kutoka kwa mashabiki wa Mahakama, "hawaamini macho yao, hawaamini macho yao, hawaamini macho yao." Alisikika shabiki mmoja akiuliza, "Mlisema leo Mahakama haichomoi, kwani ilikuwa imechomeka wapi?"

Baada ya mchezo wa Kamba Wanaume kumalizika, Kamba Wanawake ilifuata ambapo Mahakama ilipangwa kumenyana na RAS Manyara. Ilipofika wakati wa mchezo huo Mahakama Sports walitinga katika uwanja kibabe.

Hatua hiyo iliyowatisha wapinzani wao na kuondoka mmoja mmoja na kutokomea kabisa kusikojulikana, hivyo Mahakama Sports ikajizolea pointi zote tatu za mchezo huo baada ya RAS Manyara kuitwa mara tatu na waammuzi na kushindwa kutokea uwanjani.

Akiongea baada ya mchezo huo, Katibu Mkuu wa Mahakama Sports Robert Tende alisema hajafurahishwa na tabia ya wapinzani wao katika mashindano hayo ya kuwakimbia kwani walishaahidi kutoa dozi kwa kila mmoja anayostahili.

"Kama ulivyoona mjomba, Ikulu wamepata dozi yao saaafi kabisa na haki waliyokuwa wanaitaka wameipata na imetendeka, kila mtu ameona. Tunataka na wengine waje tuwape haki yao. Hii ndiyo kazi ya Mahakama, hatujazoea kufanya mambo mengine sisi," alisema.

Katika mchezo wa leo, Kamba wanaume iliwakilishwa na Leonard Kazimzuri, Yuda Mgalla, Patrick Mundwe, Denis Kipeta, Joseph Chokela, Mjuni Denis, Mussa Komba, Mochiwa Marko, Abdul Mumini na Mushi Martin, Magesa Phabian, Emmanuel Datsan, Robert Oguda, Rajab Mwaliko, Fidelis Choka na Exavery Kasembe.

Kwa upande wa Kamba Wanawake wachezaji walikuwa Beatrice Dibogo, Judith Mwakyalagwe, Merino Mwinuka, Dotto Mlandula, Rebecca Mwakabuba, Salma Mwamende, Safina Mkumbo, Maria Mayala, Zawadi Amir, Namweta Mcharo, Valeria Ntyangili, Anne Hebron, Lucy Mbwaga na Rose Mwalongo.

Viongozi ambao wameambatana na Timu ni Mwenyekiti Wilson Dede, Makamu Mwenyekiti Fidelis Choka, Katibu Mkuu Robert Tende, Katibu Mkuu Msaidizi Theodosia Mwangoka, Mweka Hazina Rajab Ally, Timu Meneja Antony Mfaume, Afisa Michezo Nkrumah Katagile.

Mashindano ya SHIMIWI ambayo yalianza jana tarehe 1 Octoba, 2022 yanatarajiwa kufunguliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassimu Majaliwa kesho tarehe 5 Octoba, 2022. Kauli mbiu ya mashindano ya SHIMIWI 2022 ni “Michezo hupunguza magonjwa yasiyo ambukiza na kuongeza tija mahala pa kazi.”

Mashindano hayo ambayo yanashirikisha michezo mbalimbali yatafanyika katika viwanja tofauti tofauti nane ambavyo ni Viwanja vya Mkwakwani, Shule ya Sekondari Popatlal, Galanos Sekondari, Bandari, Shule ya Tanga, Polisi Chumbageni na Viwanja vya Gymkhana.

Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanaume na Wanawake ikiwa katika picha ya pamoja kabla ya mchezo.
Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanaume ikiwa katika hali ya utulivu huku ikiwasoma wapinzani wao kabla ya mchezo kuanza.
Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanaume (juu) ikikamuana vilivyo na Timu ya Ikulu (chini).

Timu ya Ikulu Kamba Wanaume wakilaumiana baada ya kupoteza mchezo katika hatua ya kwanza.
Timu ya Ikulu Kamba Wanaume wakiwa hawaamini macho yao baada ya kulambishwa nyasi na Timu ya Mahakama Sports Kamba Wanaume.
Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanaume wakipongezwa na kushangiliwa na mashabiki (juu na chini) baada ya kuwagalagaza Ikulu.

Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanawake wakiwa uwanjani kuwakabiri RAS Manyara.
Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanawake ikijitayarisha kumaliza mchezo baada ya RAS Manyara kutokomea kusikojulikana.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni