Na Festo Sanga, Mahakama-Kigoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha amewapongeza wadau wa vikao vya Kamati za kusukuma mashauri ya Jinai na Madai ngazi ya Wilaya, Mkoa na Kanda ya Kigoma kwa kuiwezesha Mahakama Kigoma kupiga hatua kubwa katika utoaji wa haki kwa wakati na kuongeza kiwango cha kutumainiwa na wananchi.
Jaji Mlacha alitoa pongezi hivi karibuni wakati akifungua Mafunzo ya siku mbili kwa wajumbe wa Kamati yaliyohusisha wadau wa vikao vya Haki Jinai (Case flow management) na Madai (Bench- Bar Committee) kutoka Wilaya zote katika Kanda ya Kigoma.
“Kutokana na ushirikiano wa wadau hawa, mashauri ya mlundikano yamepungua kutoka mashauri 64 mwezi Machi 2022 hadi kufikia mashauri 10 kwa Kanda nzima ambayo nayo yako katika hatua mbalimbali za usikilizwaji,” alisema Mhe. Mlacha.
Amesema kuwa, Kanda imeweza kusajili mashauri yote kwa njia ya mtandao na kasi ya usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao imeongezeka kutoka mashauri 37 kwa mwaka 2020 ulipoaanza hadi mashauri 1,003 kwa mwaka 2022 (Januari 2022 hadi Septemba 2022).
Aidha; Jaji Mfawidhi huyo ameongeza kuwa, tathmini iliyofanyika kupitia mfumo wa kuratibu mashauri (JSDS 2) kwa muda wa kumaliza shauri mahakamani kuanzia Januari hadi Septemba 2022 ni siku 153 Kwa Mahakama Kuu, Siku 179 Mahakama ya Hakimu Mkazi na wastani wa siku 154 katika Mahakama za Wilaya. Alisema kuwa kutokana na kumalizika kwa mashauri ya mlundikano ambayo yalifanya muda wa kumalizika kwa shauri kuongezeka, kwa sasa Kanda ya Kigoma inakwenda kuwa na muda mfupi wa shauri kukaa mahakamani kama nchi ya Singapore.
“Kanda imeweza kupunguza muda wa shauri kukaa mahakamani hadi kukaribia kufikia wastani wa miezi Mitano (5) ikiikaribia Singapore ambayo kwa mwaka 2015 ilikuwa na wastani wa siku 150” alisema Jaji Mlacha.
Aliwaasa washiriki wa Mafunzo kuendana na kasi ya mageuzi ya TEHAMA na kuwaelimisha wananchi na wale wanaowaongoza ili kuenda sambamba na kasi ya Mahakama katika matumizi ya TEHAMA ambayo kwa sasa yameshika kasi na kusisitiza kuwa kasi hiyo siyo ya zima moto.
Naye mshiriki wa mafunzo ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili Mkoa wa Kigoma, Bw. Daniel Rumenyela alipongeza uboreshaji wa huduma za Mahakama hususani eneo la TEHAMA kwa kuwa imesaidia katika kuharakisha usikilizwaji wa Mashauri na kupunguza gharama za uendeshaji wa Mashauri.
Bw. Rumenyela alikiri kunufaika na mageuzi hayo kwa kudhihirisha namna anavyofaidika na mifumo ya Usajili na usikiizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao, upatikanaji wa nakala za hukumu kwenye mfumo wa tanzLII na upatikanaji wa ratiba ya mashauri (causelist) kwenye mfumo wa (JSDS 2)
Washiriki wa mafunzo walijifunza na kujadili kuhusu miongozo ya uanzishwaji, muundo na majukumu ya Kamati za kusukuma mashauri ya jinai na Madai katika kuhakikisha kuwa, haki inapatikana kwa wote na kwa wakati. Aidha walikumbushana wajibu wa wadau mbalimbali katika usimamizi wa mashauri na kubwa zaidi ilikuwa ni nafasi ya matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma za haki na kupunguza au kuondoa kabisa mlundikano wa Mashauri Mahakamani.
Mafunzo hayo yaliandaliwa ili kuwaongezea wajumbe wa kamati hizo uelewa wa pamoja wa hatua za maboresho ya Mahakama na umuhimu wa wadau hao kuwekeza katika TEHAMA ili kongeza ufanisi na tija katika kazi ya utoaji haki na chini ya kaulimbiu ya Kanda ya kumaliza mwaka 2022 bila ya mashauri mlundikano wala mashauri yaliyosajiliwa mwaka 2022.
Wakati huohuo, Kamati za kusukuma mashauri ya Jinai na Madai Kanda ya Kigoma kwa kuwashirikisha wajumbe wa Kamati hizo ngazi ya Wilaya zote na Mkoa, zilifanya vikao vyake kwa robo mwaka ya Julai hadi Septemba ambapo tathmini iliyotolewa ilionesha Kanda nzima kuwa na mashauri 4 tu ya mlundikano ambayo yaliwekewa mkakati wa kumalizika kabla ya kuisha mwaka 2022.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe Lameck Mlacha akifungua Mafunzo kwa washiriki wa Mafunzo (hawapo pichani). Mafuhnzo hayo yamefanyika hivi karibuni katika Ukumbi wa 'Lake Tanganyika' mkoani Kigoma.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Kigoma, Bw. Moses Mashaka akitambulisha Washiriki wa Mafunzo pamoja kueleza lengo la Mafunzo hayo yaliyofanyika hivi karibuni.
Mwezeshaji wa Mafunzo
ambaye ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe Gadiel Mariki
akiwasilisha mada katika mafunzo hayo yaliyofanyika hivi karibuni.
Mshiriki wa Mafunzo kutoka ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw. Boniface Kamwesige akifafanua jambo kwa washiriki wakati wa mafunzo yaliyofanyika hivi karibuni.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Kigoma, Mhe Jaji Lameck Mlacha (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya Washiriki wa Mafunzo. Aliyeketi kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe Fredrick Manyanda na kushoto ni Bw. Peter Muryuki kutoka Ofisi ya Shirika la Wakimbizi 'UNHCR' Kigoma. waliosimama nyuma ni wajumbe wa kikao cha kusukuma mashauri ya madai na Jinai ngazi ya Mkoa na Kanda.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania- Kanda ya Kigoma, Mhe. Lameck Mlacha (katikati) akiwa katika picha ya Wajumbe pamoja na wajumbe wa kikao cha kusukuma mashauri ya Jinai ngazi za Wilaya za Mkoa wa Kigoma. Kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Fredrick Manyanda na kushoto ni Bw. Peter Muryuki kutoka ofisi ya UNHCR Kigoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni