Jumatatu, 3 Oktoba 2022

WANA-JMAT MBEYA WAKUMBUSHWA KUZINGATIA MAADILI YA KAZI

Na Mohamed Kimungu, Mahakama-Mbeya

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. Rose Ebrahim amewaasa Mahakimu wa Mkoa huo kuzingatia mambo manne katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kufanya kazi kwa pamoja (team work), bidii katika utendaji kazi, nidhamu, weledi na kuwataka kulinda na kudumisha uhuru wa Mahakama.

Akizungumza hivi karibuni wakati akifungua Kongamano la Chama cha Majaji na Mahakimu (JMAT) tawi la Mbeya, Mhe. Rose aliwataka pia Maafisa hao wa Mahakama kuzingatia kanuni za maadili kwa maafisa wa Mahakama “Code of Conduct for Judicial Officers of Tanzania’ ili wasiende kinyume na miongozo ya utendaji kazi ya Mhimili huo.

“Ni vyema pia muendelee kujielimisha kwa kusoma mabadiliko ya Sheria mbalimbali pamoja na kusoma uamuzi wa Mahakama za juu, (Courts of records)” alisema Mhe. Rose.

Katika Kongamano hilo, lililobeba maudhui ya ‘timu moja, Lengo moja- pamoja kufikia mafanikio’ Mada mbalimbali zilitolewa kwa Wanachama lengo likiwa kuwajengea uwezo na kukumbashana masuala mbalimbali yanayolenga kuimarisha jukumu la utoaji haki.

Aidha; katika kongamano hilo lilihitimishwa kwa Chama hicho kufanya uchaguzi Mkuu na wajumbe mbali mbali waliteuliwa ambapo Mhe.  Andrew Scout aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa JMAT Mbeya, Mhe Ayubu Shellimo aliteuliwa kuwa Katibu, Mhe Angela Byera aliteuliwa kuwa Muweka Hazina na  Mhe Tedy Mlimba kuwa Mwakilishi wa JMAT Taifa.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe. Rose Ebrahim  akifungua Kongamano la Chama cha Majaji na Mahakimu tawi Mbeya. Kongamano hilo lilifanyika katika katika ukumbi wa 'Matema beach' jijini Mbeya.

Washiriki wa Kongamano wakimsikiliza Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe. Rose Ebrahim  alipokuwa akifungua kongamano lililofanyika hivi karibuni.
Washiriki wakiwa katika Kongamano hilo.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya, Mhe. David Ngunyale akitoa neno katika Kongamano hilo.
Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe Aziza Temu  akiwasilisha Mada kwa Washiriki wa Kongamano.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni