Jumatatu, 3 Oktoba 2022

OMBA MUNGU USIKUTANE NA MAHAKAMA SPORTS

·Kamba Wanaume yawakalisha RAS Singida

·Wanawake wanyunyiza, wakamua Maji

Na Faustine Kapama-Mahakama, Tanga

Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanaume na Wanawake leo tarehe 3 Octoba, 2022 imeendeleza wimbi la ushindi kwenye mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayofanyika jijini hapa baada ya kuwachakaza vibaya wapinzani wao, Timu za RAS Singida Wanaume na Maji Wanawake.

RAS Singida wamepata kile walichokuwa wanakitaka baada ya kukumbana na kibano kikali kutoka kwa magwiji hao wa mchezo wa kamba nchini na kuwafanya waondoke kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Usagala wakiwa vichwa chini. Kipigo kama hicho kiliwakuta Maji baada ya kunyunyizwa na baadaye kukamuliwa na Mahakama kwenye viwanja hivyo.

Mchezo huo ambao ulifanyika majira ya saa moja asubuhi ulianza kwa kuwakutanisha Kamba Wanaume katika kundi A na iliwachukua muda mchache kwa Mahakama Sports kuwapumlia wapinzani wao pumzi ya moto na kuwafanya wasiamini kilichokuwa kinaendelea.

Alisikia mchezaji mmoja kutoka timu pinzani akihoji, “Hivi nyinyi mnakula nini?” Kichapo cha mbwa mwizi kiliendelea katika hatua ya pili ambapo RAS Singida walionekana kuchanganyikiwa baada ya kuvutwa mara moja na kukubali yaishe, hivyo kuachia pointi zote tatu zikienda kwa mabingwa hao watetezi wa mchezo huo.

Baada ya mchezo huo wa upande wa wanaume kumalizika,Kamba Wanawake ulifuata kwa Mahakama Sports kuwakamua Maji ambao walionekana si lolote si chochote baada ya kupokea kipigo kikali na kukubali kutiririsha maji kwenye viwanja hivyo katika awamu zote mbili za mchezo.

Katika kipindi cha pili, Maji walijaribu kuwatunishia misuri Mabingwa hao watetezi katika mchezo huo. Hata hivyo, haikuchukua hata nusu sekunde wakanyosha mikono na kuamua kuachia pointi zote tatu kwende kwa Mahakama Sports. “Acha washinde bwana, sisi hatuwawezi,” alisikika mchezaji mmoja kutoka timu pinzani akisema.

Akizungumza katika viwanja hivyo baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Katibu Mkuu wa Mahakama Sports Robert Tende amesema kazi inaendelea na bado mapambano yanaendelea. “Nikwambie kitu kaka, safari hii hatuna utani na mtu. Wembe ni ule ule, ni ushindi mbele kwa mbele, hakuna kurudi nyuma,” alisema.

Katika mchezo wa leo, Kamba wanaume iliwakilishwa na Leonard Kazimzuri, Yuda Mgalla, Patrick Mundwe, Denis Kipeta, Joseph Chokela, Mjuni Denis, Komba Mussa, Mochiwa Marko, Abdul Mumini na Mushi Martin, Magesa Phabian, Emmanuel Datsan, Robert Oguda, Rajab Mwaliko, Fidelis Choka na Exavery Kasembe.

Kwa upande wa Kamba Wanawake wachezaji walikuwa Beatrice Dibogo, Judith Mwakyalagwe, Merino Mwinuka, Dotto Mlandula, Rebecca Mwakabuba, Salma Mwamende, Safina Mkumbo, Maria Mayala, Zawadi Amir, Namweta Mcharo, Valeria Ntyangili, Anne Hebron, Lucy Mbwaga na Rose Mwalongo.

Viongozi ambao wameambatana na Timu ni Mwenyekiti Wilson Dede, Makamu Mwenyekiti Fidelis Choka, Katibu Mkuu Robert Tende, Katibu Mkuu Msaidizi Theodosia Mwangoka, Mweka Hazina Rajab Ally, Timu Meneja Antony Mfaume, Afisa Michezo Nkrumah Katagile.

Mashindano ya SHIMIWI ambayo yalianza jana tarehe 1 Octoba, 2022 yanatarajiwa kufunguliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassimu Majaliwa tarehe 5 Octoba, 2022. Kauli mbiu ya mashindano ya SHIMIWI 2022 ni “Michezo hupunguza magonjwa yasiyo ambukiza na kuongeza tija mahala pa kazi.”

Mashindano hayo ambayo yanashirikisha michezo mbalimbali yatafanyika katika viwanja tofauti tofauti nane ambavyo ni Viwanja vya Mkwakwani, Shule ya Sekondari Popatlal, Galanos Sekondari, Bandari, Shule ya Tanga, Polisi Chumbageni na Viwanja vya Gymkhana.

Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanawake leo tarehe 3 Octoba, 2022 kabla ya mchezo.
Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanaume leo tarehe 3 Octoba, 2022 kabla ya mchezo.

Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanaume (juu) ikiwakalisha RAS Singida (chini).




Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanaume ikishangilia kwa furaha pamoja na mashabiki wao baada ya kumaliza kazi iliyowaleta SHIMIWI Tanga.

Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanawake ikijiandaa kunyunyiza.
Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanawake (juu) ikiwakamua Maji (chini).

Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Kamba Wanawake (juu na chini) wakiwa na mashabiki wao wakishamngilia ushindi.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni