Jumapili, 2 Oktoba 2022

MAHAKAMA SPORTS NETIBOLI YATOA ONYO KALI SHIMIWI

Na Faustine Kapama-Mahakama, Tanga

Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Netiboli leo tarehe 2 Octoba, 2022 imeyaanza mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) kwa kutoa onyo kali kwa timu pinzani baada ya kuwabamiza timu ya RAS Mtwara kwa vikapu 40:4.

Mchezo huo ambao umechezwa katika Viwanja vya Polisi Chumbageni kuanzia majira ya saa 11 jioni ulianza kwa kasi huku Timu ya Mahakama ikilisakama goli la wapinzani wao na haikuchukua muda ikaanza kutupia vikapu.

Mchezo huo ambao ulichezwa kwa dakika 40 mara zote uliegemea upande mmoja kufuatia umahiri wa wachezaji wa Mahakama ambao walikuwa imara na walicheza kwa umahiri mkubwa.

Wachezaji wote walicheza kwa ushirikiano wa hali ya juu na kulishambulia lango la wapinzani wao kwa mwendo wa karne ya 21, hivyo kutupia tupia vikapu mara kwa mara.

Mwiba na nyota wa mchezo huyo walikuwa wachezaji wa Mahakama Sports Filomena Haule na Upendo Matunda ambao kila dakika walikuwa wanatupia vikapu, kiasi cha mashabiki wao kuwabatiza kwa jina la Mayele.

Mashabiki wa Timu ya RAS Mtwara waliojitutumua mwanzo kuwatia moyo wachezaji wao walitokomea kusikojulikana baada ya Timu yao kugeuzwa mdebwedo na Timu ya Mahakama ya Tanzania.

Hadi mwisho wa mchezo, Mahakama Sports ilishatupia vikapu 40 huku RAS Mtwara wakiambulia vikapu vinne (4) tu na kwenda kujiburudisha na korosho walizokuja nazo.

Akizungumza baada ya mechi hiyo, Mwalimu wa Timu Mtumwa Sululu amesema siri ya ushindi huo ni vijana wake kucheza kitimu, kuwa na nidhamu na kuzingatia programu aliyokuwa ameiweka.

"Nawapongeza sana vijana wangu kwa ushindi huu mnono. Tunajipanga kwa mechi inayokuja na niwahakikishie vipigo kama hivi vitaendelea," alisema. 

Wachezaji walioiwakilisha Mahakama ni Filomena Haule, Upendo Matunda, Nyange Simola, Veronica Kajobi, Diane's Akanganyila, Shani Ally, Tarita Kayuni. Wachezaji wa akiba walikuwa Marikia Nondo, Margaret Kanyaga, Agnes Kilian,Jackline Paul, Adeudata Mkonkosha.

Viongozi wa Mahakama Sports ambao wamerongozana na timu mbalimbali ni Mwenyekiti Wilson Dede, Makamu Mwenyekiti Fidelis Choka, Katibu Mkuu Robert Tende, Katibu Mkuu Msaidizi Theodosia Mwangoka, Mweka Hazina Rajab Ally, Timu Meneja Antony Mfaume, Afisa Michezo Nkrumah Katagile.

Mashindano ya SHIMIWI ambayo yalianza jana tarehe 1 Octoba, 2022 yanatarajiwa kufunguliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassimu Majaliwa tarehe 5 Octoba, 2022. Kauli mbiu ya mashindano ya SHIMIWI 2022 ni “Michezo hupunguza magonjwa yasiyo ambukiza na kuongeza tija mahala pa kazi.”

Mashindano hayo ambayo yanashirikisha michezo mbalimbali yatafanyika katika viwanja tofauti tofauti nane ambavyo ni Viwanja vya Mkwakwani, Shule ya Sekondari Popatlal, Galanos Sekondari, Bandari, Shule ya Tanga, Polisi Chumbageni na Viwanja vya Gymkhana.

Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Netiboli kabla ya mchezo.
Mchezaji wa Timu ya Mahakama Sports Netiboli akitupia kikapu kwenye gori la RAS Mtwara.

Wachezaji wa Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Netiboli (juu na chini) wakijiandaa kutupia vikapu kwenye gori la RAS Mtwara.


Sehemu ya viongozi na benchi la ufundi la Timu ya Mahakama Sports Netiboli likifuatilia mechi hiyo.
Mwalimu wa Timu Mtumwa Sululu akizungumza na wachezaji wake wakati wa mapumziko.
Mchezaji wa Mahakama Sports akimdhibiti vilivyo mshambuliaji wa Timu ya RAS Mtwara.
Sehemu ya mashabiki wa Mahakama Sports (juu na chini) wakishangilia timu yao.
Mashabiki wa Mahakama Sports wakijimwaga uwanjani kushangilia ushindi baada ya mechi kuisha.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni