Na Faustine Kapama-Mahakama, Tanga
Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Mpira
wa Miguu Wanaume leo tarehe 2 Octoba, 2022 imeipeperusha vyema bendera ya
Mahakama baada ya kuwachapa mabao 2-0 Timu ya Tume ya Utumishi katika mchezo wa
kwanza hatua ya makundi kwenye mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na
Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayofanyika jijini hapa.
Mechi hiyo iliyochezeshwa kuanzia majira ya saa mbili
asubuhi katika Viwanja vya Shule ya Sekondari ya Galanosi ilianza kwa timu zote
mbili kusomana na kuusoma mchezo wote kwa ujumla, huku kukiwepo na mashambulizi
ya hapa na pale.
Kulikuwepo na kosa kosa kadhaa katika kipindi cha kwanza
ambapo Timu ya Mahakama ilikuwa ikilishambulia lango la wapinzani wao kama
nyuki. Nayo Timu ya Tume ilipata mipira iliyokufa mara kadhaa kutokana na
madhambi yaliyokuwa yanafanywa na wachezaji wa Mahakama.
Hata hivyo, timu hiyo ilishindwa kutumia nafasi hizo
na kushindwa kupata mabao kutokana na umahiri wa walinzi na mdaka mishale wa
Mahakama Sports. Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika timu zote zilienda kwenye
mapumziko zikiwa nguvu sawa.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi kwa timu ya
Mahakama kulisakama lango la wapinzani wao. Mashambulizi hayo yalilipa ambapo katika
dakika ya 43 ya mchezo Winga wa Kulia hatari Frank Obadia, “Aziz Ki” alifanikiwa
kuukwamisha mpira wavuni na kuiandikia timu yake bao la kwanza na la kuongoza baada
ya kuwachambua kama karanga mabeki wa timu pinzani.
Kupachikwa kwa bao hilo kuliwafanya Timu ya Tume
kupoteana, hivyo kuchochea mashambulizi na hamasa kubwa kwa wachezaji kutoka
Timu ya Mahakama ambao walikuwa wanafika katika lango la wapinzani wao mara kwa
mara na kosa kosa za hapa na pale kutokana na kukosekana kwa utulivu.
Hata hivyo, ilipofika katika dakika ya 56, mwamba yule
yule (Frank Obadia) aliwanyanyua mashabiki wa Mahakama Sports baada ya kufunga
bao la pili kutokana na pasi mpenyezo iliyotoka kwa mshambuliaji hatari wa kati
Beatus Semwanza na kuifanya timu yake kuongoza kwa mabao mawili.
Bao hilo lilifuatiwa na mashambulizi kadhaa kutoka timu
zote mbili na ilibakia kidogo tu katika dakika za lala salama kwa Mchezaji namba
10 wa Mahakama Sports Martin Mpanduzi kuipatia timu yake bao la tatu baada ya
kushindwa kuukwamisha mpira nyavuni akiwa yeye na kipa wa Timu ya Tume. Hadi mchezo
una malizika, Mahakama Sports 2 na Timu ya Tume ya Utumishi 0.
Akizungumza baada ya mechi hiyo ya kusisimua, Mwalimu
wa Mahakama Sports Spear Mbwembwe amewapongeza vijana wake kwa kujituma na
kufanikiwa kupata ushindi huo. Amesema wataendelea kutoa dozi takatifu hata kwa
timu zingine kwa vile wamedhamiria kuchukua kombe katika mashindano hayo.
“Nawapongeza sana vijana wangu, wamefanya vizuri. Ila
bado sijaridhika na ushindi huu. Pamoja na kupata ushindi, sisi tunataka magori
zaidi. Kwa vile leo ndiyo tumeanza nategemea mabao mengi zaidi kwenye mechi
zijazo. Vijana wangu wote wapo vizuri sana, ila kwa leo nadhani walikuwa na
hofu ya mchezo ndiyo maana hawa jamaa (Timu ya Utumishi) wamesalimika,”
alisema.
Naye Mwenyekiti wa Mahakama Sports Wilson Dede amesema
mapambano bado yanaendelea. “Hatujamaliza kaka, ndiyo kwaaanza tunaanza.
Wapinzani wetu wasifikiri hii ni nguvu ya soda. Tutawashangaza wengi mwaka huu.
Tumekuja kuzoa kila kitu kwenye mashindano haya,” alisema.
Katika mchezo wa leo, Mahakama Sports iliwakilishwa na
Fahamu Kibona; Iman Patson; Gisbert Chentro; Akida Mzee; Emmanuel Mwamole; Selemani
Magawa; Frank Obadia; Gabriel Tabana; Martin Mpanduzi; Mwinjuma Bwanga na Shamte
Seif. Wachezaji wa akiba walikuwa Hassan Aufi; Nassoro Mwampamba; Kelvin
Rutalemwa; Shabiru Hood na Beatus Simwanza.
Mbali na Mwenyekiti, viongozi wengine ambao wameambatana
na Timu ni Makamu Mwenyekiti Fidelis Choka, Katibu Mkuu Robert Tende, Katibu
Mkuu Msaidizi Theodosia Mwangoka, Mweka Hazina Rajab Ally, Timu Meneja Antony
Mfaume, Afisa Michezo Nkrumah Katagile.
Mashindano ya SHIMIWI ambayo yalianza jana tarehe 1
Octoba, 2022 yanatarajiwa kufunguliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassimu Majaliwa tarehe 5 Octoba, 2022. Kauli mbiu
ya mashindano ya SHIMIWI 2022 ni “Michezo hupunguza magonjwa yasiyo ambukiza na
kuongeza tija mahala pa kazi.”
Mashindano hayo ambayo yanashirikisha michezo
mbalimbali yatafanyika katika viwanja tofauti tofauti nane ambavyo ni Viwanja
vya Mkwakwani, Shule ya Sekondari Popatlal, Galanos Sekondari, Bandari, Shule
ya Tanga, Polisi Chumbageni na Viwanja vya Gymkhana.
Mwalimu wa Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Mpira wa Miguu Wanaume Spear Mbwembe akizungumza na wachezaji wake wakati wa mapumziko.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni