Na Faustine Kapama-Mahakama, Tanga
Timu ya Mahakama ya Tanzania (Mahakama Sports) Kamba
Wanaume na Wanawake leo tarehe 2 Octoba, 2022 imeanza vizuri kwenye mashindano ya Shirikisho
la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayofanyika jijini hapa baada
ya kuwaadhibu vikali wapinzani wao, Timu za Haki na RAS Singida.
Ilikuwa Kamba Wanaume katika mchezo wa makundi ulioanza
ambapo Timu ya Haki iliingia hofu na kusita kwa dakika kadhaa kuingia uwanjani
mara baada ya kuwaona wababe hao wa Mahakama pamoja na kuitwa na wasimamizi wa
mchezo huo mara kwa mara.
Haikumchukuwa Njiwa kumeza punje ya mtama pale mchezo
ulipoanza ambapo Mahakama walitumia dakika sifuri kuwagaragaza Haki. Kadhalika,
kazi ilikuwa nyepesi katika kipindi cha pili baada ya Timu ya Haki kuchekechwa
vilivyo, hivyo kushindwa kabisa kufurukuta na kupoteza pointi zote tatu kwenye
mchazo huo.
Baada ya mchezo huo wa upande wa wanaume kumalizika, mchezo
wa Kamba Wanawake wa makundi ulianza kwa Mahakama Sports kukabiliana na RAS Singida.
Katika hatua ya mwanzo, RAS Singida walinyofolewa kirahisi licha ya kuingia
kwenye uwanjani huku wakihamasishana.
Mahakama Sports ilikuwa haijamaliza kwani katika hatua
ya pili wapinzani hao wa watoa haki walijikuta wakilamba nyasi za uwanja baada
ya kupokea ‘kamba mchomoko’ na hivyo kuachia pointi zote tatu katika mchezo huo
wa awali wa makundi.
Akiongea baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Katibu
Mkuu wa Mahakama Sports Robert Tende amesema ushindi ambao Timu yake imeupata
ni salamu tosha kwa wapinzani wao kwa vile wamejipanga kutoa haki sawa ambayo inaambatana na dozi takatifu kwa
kila timu watakayokumbana nayo.
“Hapa bado hatujamaliza, ndiyo tunaanza. Nawaomba
wenzetu wawe wavumilivu, wameamua kuingia kwenye mashindano haya wao wenyewe na
hawajalazimishwa na mtu. Hivyo, watulie ili sindano iingie vizuri na wapate
dozi kamili. Tulishasema tunatoa dozi ya kutwa mara tatu, wajifunze kilichotokea
leo kama walikuwa hawajaelewa tulichokuwa tunamaanisha,” alisema.
Katika mchezo wa leo, Kamba wanaume iliwakilishwa na Leonard
Kazimzuri, Yuda Mgalla, Patrick Mundwe, Denis Kipeta, Joseph Chokela, Mjuni
Denis, Komba Mussa, Mochiwa Marko, Abdul Mumini na Mushi Martin. Wachezaji wa
akiba walikuwa Magesa Phabian, Emmanuel Datsan, Robert Uguda, Rajab Mwaliko na
Exavery Kasembe.
Kwa upande wa Kamba Wanawake wachezaji walikuwa Beatrice
Dibogo, Judith Mwakyalagwe, Merino Mwinuka, Dotto Mlandula, Rebecca Mwakabuba,
Salma Mwamende, Safina Mkumbo, Maria Mayala, Zawadi Amir, Namweta Mcharo. Wachezaji
wa akiba walikuwa Valeria Ntyangili, Anne Hebron, Lucy Mbwaga na Rose Mwalongo.
Matokeo ya michezo mingine iliyochezwa kwenye kundi A kwenye
Kamba wanaume ilikuwa RAS Dodoma ambayo haikufua dafu kwa Timu ya Ikulu, huku
Kamba Wanawake ikishirikisha Timu ya Maji ambayo ilipata pointi moja dhidi ya
Viwanda baada ya kutoshana nguvu kwenye hatua ya kwanza.
Viongozi ambao wameambatana na Timu ni Mwenyekiti
Wilson Dede, Makamu Mwenyekiti Fidelis Choka, Katibu Mkuu Robert Tende, Katibu
Mkuu Msaidizi Theodosia Mwangoka, Mweka Hazina Rajab Ally, Timu Meneja Antony
Mfaume, Afisa Michezo Nkrumah Katagile.
Mashindano ya SHIMIWI ambayo yalianza jana tarehe 1
Octoba, 2022 yanatarajiwa kufunguliwa rasmi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassimu Majaliwa tarehe 5 Octoba, 2022. Kauli
mbiu ya mashindano ya SHIMIWI 2022 ni “Michezo hupunguza magonjwa yasiyo
ambukiza na kuongeza tija mahala pa kazi.”
Mashindano hayo ambayo yanashirikisha michezo
mbalimbali yatafanyika katika viwanja tofauti tofauti nane ambavyo ni Viwanja
vya Mkwakwani, Shule ya Sekondari Popatlal, Galanos Sekondari, Bandari, Shule
ya Tanga, Polisi Chumbageni na Viwanja vya Gymkhana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni