Na Stanslaus Makendi- Mahakama, Dodoma
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, ambaye ni Mlezi wa Chama cha
Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) Tawi la Dodoma, Mhe. Gerson Mdemu amehimiza
umoja, ushirikiano na uwajibikaji katika chama hicho ili kuongeza tija wanapotekeleza majukumu yao.
Mhe. Mdemu alitoa rai hiyo hivi karibuni katika mkutano wa
JMAT Tawi la Dodoma uliofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha. Akiongea
katika mkutano huo, Jaji Mfawidhi huyo aliwahimiza wajumbe wa chama hicho ambao
walikuwa katika hifadhi hiyo kwa ajili ya kufanya utalii wa ndani kuwa na utaratibu wa kutembeleana na
kubadilishana uzoefu ndani ya Mkoa, nje
na ndani ya Kanda hiyo
ili kuboresha mahusiano miongoni mwao.
Kadhalika,
Jaji Mfawidhi huyo aliwahimiza Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama
za Wilaya ndani ya Mkoa wa Dodoma kuhamasisha na kuhakikisha uhai wa chama
unaendelea kuwepo na kuendelea kuimarika
chama hicho katika
maeneo yao kwani wao ndio walezi katika ngazi hizo, huku akisisitiza zaidi wanachama hao kutoa
michango yao ya kila mwezi.
Akihitimisha
kikao hicho, Mhe. Mdemu aliwasisitiza wajumbe wa
JMAT Tawi la Dodoma kukumbuka na kuwajibika kujaza fomu za maadili, zoezi
ambalo ni endelevu kwa mujibu wa Sheria na linapaswa kutekelezwa kabla ya
tarehe 31 Disemba kila Mwaka. Aliwaomba Majaji na Mahakimu kujenga desturi ya
kutembelea Magereza na kushiriki kutatua
changamoto zinazobainika ili kuondokana na kero na malalamiko yanayoelekezwa mahakamani.
Majaji na
Mahakimu waliotembelea hifadhi
hiyo walipata fursa ya kujionea vivutio
mbalimbali vya utalii na kupata mafunzo yanayohusu uhifadhi, historia ya
Hifadhi ya Ruaha, namna inavyoendeshwa, changamoto zinazoikabili na mipango ya
kuiboresha zaidi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni