Ijumaa, 22 Machi 2024

JAJI NDUNGURU AWASISITIZA MAHAKIMU KUTUMIA MIFUMO YA KIELEKTRONIK

Na Mwinga Mpoli- Mahakama, Mbeya

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, Mhe. Dunstan Ndunguru amewasisitiza Mahakimu kuzingatia matumizi ya mfumo wa Kielektronik wa Usimamnizi wa Mashauri (e-CMS) katika majukumu yao ya kila siku na kuwataka kutambua kwamba, zoezi la matumizi ya mifumo hiyo ya Mahakama halitarudi nyuma hivyo kila mmoja anatakiwa kuendelea kutumia mifumo hiyo huku changamoto zingine zikiendelea kufanyiwa kazi.

Ameyasema hayo hivi karibuni katika kikao kazi kilichofanyika Mahakama Kuu Mbeya, na kuwataka Mahakimu wafawidhi kufuatilia matumizi ya mifumo hiyo katika vituo vyao kwa karibu. Kikao hicho kiliwajumuisha Majaji, Manaibu Wasajili, na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wote wa Kanda ya Mbeya.

 “Ni wajibu wa kila Hakimu Mfawidhi kuhakikisha anasimamia na kufuatilia vyema matumizi ya mfumo huu wa e-CMS katika kituo chake” alisema Mhe. Ndunguru

Aidha, Mhe. Ndunguru alisisitiza juu ya suala la kumaliza mashauri ya muda mrefu, hasa yale ya utekelezaji wa hukumu za Mahakama yaliyokaa muda mrefu Mahakamani pamoja na ukaguzi wa kina katika Mahakama zao.

“Ni vyema kukawa na mikakati thabiti ya namna ya kumaliza mashauri ya muda mrefu lakini pia kila mmoja wetu achukue nafasi yake na tuelezane ukweli pale penye changamoto. Zaidi tuhakikishe tunafanya ukaguzi wa kina katika Mahakama zetu na tukague pia vyumba vya vielelezo na tuhakikishe kila kielelezo kipo katika utaratibu unaotakiwa” alisisitiza Jaji Ndunguru

Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Victoria Nongwa katika kikao hicho aliwapitisha Mahakimu Wafawidhi kwenye takwimu za mashauri kwa mwaka 2023 kama ilivyokuwa imetolewa na kurugenzi ya mashauri katika kikao cha Majaji Wafawidhi Arusha na kisha kujadiliana kwa pamoja na kufanya tathmini ya utoaji haki kwa mwaka 2023 na kujiwekea mikakati ya kumaliza mashauri yote ya mrundikano ifikapo June, 2024 lakini pia kuzuia kabisa mlundikano wa mashauri kwa mwaka 2024.

Naye, Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Temu alisisitiza juu ya kushiriki kikamilifu katika uandaaji wa taarifa mbalimbali na zaidi wazikague taarifa hizo kabla ya kuzituma na wajenge utamaduni wa kupitia barua pepe mara kwa mara kwani zinatumika kutoa maelekezo mbalimbali ya viongozi.

Kikao kazi hicho kilitoka na maadhimio kadhaa ikiwemo suala la umalizaji wa mashauri ya mlundikano, matumizi ya mifumo ya uendeshaji wa mashauri na kubadirishana uzoefu katika masuala ya utekelezaji wa hukumu za Mahakama.

Sehemu Majaji walioshiriki kikao kazi hicho, katikati ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya Mhe. Dunstan Ndunguru, (kulia) ni Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya Mhe. Victoria Nongwa na (kushoto) ni Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya Mhe. Emmanuel Kawishe. 

Jaji wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Mbeya Mhe. Victoria Nongwa akiwapitisha washiriki wa kikao kazi katika takwimu za mashauri mwaka 2023.


Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Aziza Temu akieleza jambo wakati wa kikao kazi hicho.

Sehemu ya Mahakimu Wakazi Wafawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya walioshiriki kikao hicho. 






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni