Ijumaa, 22 Machi 2024

MAHAKAMA YA WILAYA MOROGORO YAFANYA KIKAO CHA KITAALUMA

Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro

 

Mahakama ya Wilaya ya Morogoro jana tarehe 21 Machi, 2024 ilifanya kikao cha kitaaluma ili kujadili namna bora ya kuwa na uelewa wa pamoja katika uboreshaji wa utoaji haki.

 

Kikao hicho kilichofanyikia katika Ukumbi wa Mkutano ulioko ndani ya Jengo la Kituo Jumuishi kilichopo Kanda ya Morogoro kilifunguliwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya, Mhe. Mary Kallomo.

 

Kufanyika kwa Kikao hicho ni sehemu ya maelekezo ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Mhe. Latifa Mansoor ya kuitaka kila Mahakama ya Wilaya ndani ya Kanda hiyo kufanya kikao kama hicho.

 

Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho, Mhe. Kallomo alieleza matumaini yake kuona kila mshiriki anaenda kufanya kazi kwa uadilifu, weledi na uwajibikaji kama ilivyo salamu ya Mahakama na kuhakikisha Mahakama ya Tanzania inatangazwa vyema.

 

Katika Kikao hicho, masuala mbalimbali yalijadiliwa ikiwemo mawasilisho kadhaa ya makosa yanayojirudia katika usikilizaji wa mashauri, kuainisha maeneo ya kisheria yanayohitaji mjadala wa pamoja, kuainisha maeneo yanayohitaji mafunzo ya ziada, kuhimiza kuhuisha mashauri kwa wakati na namna bora ya kujaza taarifa za kimashauri.

 

Sanjari na hayo, kikao kiliwashirikisha wajumbe mbalimbali kama Mahakimu, Afisa Utumishi wa Wilaya, Ofisi ya Waendesha Mashtaka na baadhi ya watumishi wa Mahakama katika kada zingine.

 

Miongoni mwa maazimio yaliyowekwa ilikuwa ni kuhakikisha mwananchi anapata haki yake kwa wakati bila kukwamishwa na kuhuisha mashauri kwa wakati.


Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Morogoro, Mhe. Mary Kallomo akizungumza wakati wa kufungua kikao cha kitaaluma katika Mahakama hiyo.


Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Wilaya Morogoro, Mhe. Robert Kasele akitoa mada ya namna bora ya kuandika hukumu kwa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo.


Mwezeshaji toka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Morogoro Shabani Kabelwa akitoa mada wakati wa kikao hicho.


Sekretarieti ikiendelea na majukumu wakati wa kikao hicho.


Meza Kuu waliokaa mbele ikiongozwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya, Mhe. Mary Kallomo, wa pili toka kulia, wa kwaza kulia ni Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Wilaya, Mhe. Robert Kasele na wa tatu toka kulia ni Afisa utumishi wa Mahakama hiyo, Bi. Dativa Michael, wakiwa katika picha ya pamoja na wawasilisha mada.



Meza Kuu waliokaa mbele ikiongozwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya, Mhe. Mary Kallomo, wa pili toka kulia, wa kwanza kulia ni Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Wilaya, Mhe. Robert Kasele na wa tatu toka kulia ni Afisa Utumishi wa Mahakama hiyo, Bi. Dativa Michael, wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa kikao hicho.

Sehemu ya washiriki wa kikao.

 

 (Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 

 


 


 

 


 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni