Jumapili, 17 Machi 2024

KAMATI YA BUNGE UTAWALA, KATIBA NA SHERIA YAUFURAHIA MFUMO WA TTS

Yaipongeza Mahakama, Serikali kwa maboresho makubwa

Yaishauri Bunge kutumia Mfumo huo pia

Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeonesha kufurahishwa na ufanyaji kazi wa Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri (TTS) wa Mahakama ya Tanzania mara baada ya kuukagua Mfumo huo leo tarehe 17 Machi, 2024.

Akizungumza kwa niaba ya Kamati hiyo katika ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma mara baada ya kufanyiwa ‘demonstration’ ya jinsi Mfumo huo unavyofanya kazi, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Joseph Muhagama amesema uwepo wa Mfumo huo ni mapinduzi makubwa katika tasnia ya Haki nchini.

“Siku ya leo tunahitimisha safari ya kama miaka mitatu ya kutafuta na kujenga Mfumo huu ambayo leo tumeshuhudia ukifanya kazi kwa vitendo na si nadharia, tunayo furaha na hivyo kama Kamati tunaipongeza Mahakama na Serikali kwakuwa tumepiga hatua kubwa sana kama Nchi,” amesema Mhe. Dkt. Muhagama.

Mhe. Dkt. Muhagama ameishauri Mahakama ya Tanzania kupanua huduma kwa kusimika Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri (TTS) katika ngazi zote za Mhimili huo ili kuongeza ufanisi katika utoaji haki kwa wananchi.

Kadhalika, Mwenyekiti huyo amesema, kupitia Mfumo huo ameona fursa ambapo amelishauri Bunge la Tanzania kuangalia namna ya kufanya ili nao waweze kuutumia Mfumo huo hususani katika uandishi wa kumbukumbu rasmi za Bunge ‘Hansard’.

“Tunatumia muda mwingi kunukuu mazungumzo ya vikao vya Bunge, ni mchakato mrefu na ni gharama, hata hivyo nashauri Bunge kuangalia uwezekano wa kutumia Mfumo kama huu ili kurahisisha uandishi wa ‘hansard’,” ameeleza Mwenyekiti huyo.

Kadhalika ameishauri Serikali kuutangaza Mfumo huo katika nchi Jirani zinazotumia lugha ya Kiswahili ili kuweza kupata mapato kwa Taifa.

Akitoa salaam za shukrani, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Pindi Chana ameishukuru Kamati hiyo kwa ushirikiano na kuahidi kuwa, Wizara pamoja na Mahakama watashirikiana kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Kamati hiyo.

“Napenda kutoa shukrani za dhati kwa Kamati, tunaamini yote mliyoyaona na changamoto zilizopo, mtatusaidia kuzingatia, hata katika bajeti yetu ya mwaka ujao wa fedha,” amesema Mhe. Dkt. Chana.

Ameongeza kuwa, Wizara iko milango wazi ili kuhakikisha kwamba inatoa ushirikiano katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata haki kwa wakati.

Mwenyekiti huyo ambaye aliambatana na Wajumbe wa Kamati hiyo, walipata fursa ya kuangalia na kuelezwa jinsi Mfumo wa TTS unavyofanya kazi pamoja na kufanya igizo la kuendesha kikao cha Bunge kwa kutumia Mfumo huo.

Mara baada ya igizo walilofanya kukamilika, Wabunge hao walionyeshwa kupitia ‘screen’ jinsi ambavyo Mfumo ulivyonukuu mwenendo mzima wa kikao hicho kilichoendeshwa katika Lugha ya Kiswahili kuanzia mwanzo hadi mwisho na baadae kutoa tafsiri ya mwenendo wa kikao hicho kwa Lugha ya Kiingereza.

Kwa kipindi kirefu kumekuwa na malalamiko ya kuchelewa kupatikana kwa mienendo ya mashauri na kuwepo kwa mapungufu katika mienendo ya mashauri hayo. Ili kuondokana na kadhia hiyo, Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Kampuni ya ALMAWAVE ya Italia imejenga Mfumo unaotumia akili mnemba (Artificial Intelligence) kufundisha lugha ya Kiswahili na Kiingereza cha Kisheria.

Miongoni mwa faida za Mfumo wa TTS ni pamoja na kuwapunguzia kazi kubwa waliyokuwa wanaifanya Majaji na Mahakimu ya kuandika kwa mkono mienendo ya mashauri na hivyo kuwawezesha wananchi kupata haki kwa wakati.

Mpaka sasa Mfumo huo tayari umefungwa katika Mahakama 11 na mpango uliopo ni kufunga katika Mahakama zote nchini.

Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akiwa ameambatana na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Joseph Muhagama (kulia) pamoja na wajumbe wa Kamati hiyo walipowasili Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma leo tarehe 17 Machi, 2024 kwa ajili ya kukagua Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri (TTS) wa Mahakama ya Tanzania.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Joseph Muhagama akizungumza jambo baada ya zoezi la ukaguzi wa Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri (TTS) wa Mahakama ya Tanzania leo tarehe 17 Machi, 2024. 


Mkurugenzi Msaidizi Usimamizi wa Mashauri, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Hawa Mnguruta akitoa ufafanuzi kuhusu Mfumo wa TTS kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria (hawapo katika) leo wakati waliofika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma kukagua Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria na Washiriki wengine wakimsikiliza Mkurugenzi Msaidizi Kurugenzi ya Usimamizi wa Mashauri, Mhe. Hawa Mnguruta (hayupo katika picha) alipokuwa akiwaelezea jinsi Mfumo wa TTS unavyofanya kazi.

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Pindi Chana akizungumza jambo wakati wa kikao kati ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria pamoja na Mahakama ya Tanzania wakati wa ukaguzi wa Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri (TTS).

Mtendaji Mkuu, Mahakama ya Tanzania akizungumza jambo wakati Wajumbe Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria walipotembelea IJC Dodoma kwa ajili ya kukagua Mfumo wa Unukuzi na Tafsiri wa Mahakama ya Tanzania leo tarehe 17 Machi, 2024.

(Picha na Jeremia Lubango, Mahakama-Dodoma)


 





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni