Jumatatu, 18 Machi 2024

ZINGATIENI HAKI ZA MTOTO KULINGANA NA MIKATABA NA SHERIA ZILIZOPO; JAJI RWIZILE

Na Aidan Robert, Mahakama Kigoma

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile amewataka wadau na wasimamizi wa mashauri ya watoto kuzingatia haki za mtoto kulingana na Sheria na Mikataba ya Kimataifa inayolinda haki za Watoto ambayo Serikali ya Tanzania imeridhia.

 Mhe. Rwizile aliyasema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati akifunga mafunzo ya siku tano (5) yaliyotolewa kwa jumla ya watumishi na wadau wa Mahakama 64 walio mstari wa mbele katika kushughulikia mashauri ya Watoto mahakamani.

“Kimsingi mmepata weledi na ufahamu mkubwa juu ya hizo sheria na mikataba  kupitia mafunzo hayo ili kuhakikisha Sheria hizi zinafanya kazi katika kulinda haki ya mtoto afikishwapo katika vyombo vyetu vya kutoa haki,” alisema Jaji Mfawidhi.

Jaji Rwizile alisema kuwa, kupitia mafunzo hayo ana imani kwamba wamefahamu uendeshaji wa mashauri ya mtoto kuwa kuna utofauti mkubwa kulinganisha na mashauri mengine na hivyo kuwataka wadau kushirikiana kwa pamoja kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika kusimamia mashauri hayo hasa kwa watoto wanaokinzana na Sheria.

“Tunapofunga mafunzo haya isiwe mwisho wa kufunga vitabu maana elimu ni endelevu kwa sababu tulichofanya hapa tumeongeza ujuzi zaidi ili twende kumuhudumia huyo mtoto kwa namna bora zaidi,” alisisitiza Mhe. Rwizile.

Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Pamela Mazengo, aliwashukuru Waratibu wa mafunzo hayo ambao ni Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF).

Mafunzo hayo yalihusisha Mahakimu wa Mahakama za Wilaya, Waendesha Mashitaka, Maafisa Ustawi wa Jamii wa halmashauri, Watoa Msaada wa Sheria kutoka Taasisi mbalimbali na Wasaidizi wa Kumbukumbu na Nyaraka wa Mahakama.

Kwa upande wake Mratibu wa Masuala ya Haki ya Mtoto, toka Chuo cha uongozi wa Mahakama (IJA), Bi. Helena Gabriel, kwa niaba ya Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) alisema mafunzo hayo tangu yafunguliwe hadi kufika hitimisho washiriki na wawezeshaji wameonyesha uwezo, weledi na ufahamu mkubwa juu ya Sheria na Miongozo mbalimbali inayolinda haki ya mtoto anapokinzana na sheria katika jamii.

Kadhalika aliwapongeza wakufunzi mbalimbali walioendesha mafunzo hayo wakiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile kwa weledi na umahiri wao walipokuwa wakiwasilisha mada wakati wa mafunzo hayo.

Akitoa shukrani kwa niaba ya washiriki wote, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Uvinza, Mhe. Misana Majula walikishukuru Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa ufadhili pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF) kwa kutoa mafunzo hayo.

“Tulikuwa na uelewa mdogo juu ya uendeshaji wa kesi za watoto na haki zao, kwa sasa tumeiva vizuri kwa ajili ya kumhudumia mtoto wa kigoma na Tanzania kwa ujumla wake,” alisema Mhe. Majula.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile akitoa hotuba yake ya kufunga  mafunzo ya jinsi ya kuendesha Mashauri ya Mtoto tarehe 15, Machi 2024 yaliyotolewa kwa watumishi wa Mahakama na Wadau wake katika ukumbi wa The Warreth mkoani Kigoma.

Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Pamela Mazengo akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wakufunzi wa mafunzo ya J
insi ya Kuendesha Mashauri ya Mtoto. Wakufunzi hao walioongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile. 
Mratibu wa Masuala ya Haki ya Mtoto kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Bi. Helena Gabriel, akitoa neno la shukrani kwa niaba ya  Mkuu wa Chuo hicho.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (kulia katikati) akitoa vyeti kwa washiriki wa mafunzo ya Jinsi ya Kuendesha Mashauri ya Mtoto. Anayepokea cheti ni  Hakimu Mkazi Mahakama ya Wilaya Kigoma, Mhe. Eva Mushi.

Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, 
Mhe. Aziza Mbadjo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mratibu wa Masuala ya Haki ya Mtoto kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA), Bi. Helena Gabriel (kulia) na kushoto Msaidizi wa Kumbukumbu Mwandamizi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha-Pwani, Bi. Eunice Lugiana pamoja na Wasaidizi wa Kumbukumbu kutoka Kanda ya Kigoma.

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni