- Ahimiza maadili, upendo kazini
- Asema suluhu ni bora, haiachi jeraha
Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina amewahimiza Wawakilishi Binafsi kufanya kazi kwa upendo, weledi, maadili na kwa kuzingatia taratibu wanapotekeleza majukumu yao waliyokasimiwa na sheria.
Mhe. Mlyambina alitoa wito huo hivi karibuni alipokuwa anafungua Kikao cha Wawakilishi Binafsi kilichofanyika kwenye ukumbi wa wazi katika Divisheni hiyo jijini Dar es Salaam.
“Kwa kufanya hivyo, mtaweza kuitekeleza kazi hiyo kwa ufasaha kwakuwa mteja anapokuchagua, sheria inakuhitaji kuitekeleza.Ni wajibu wako kuwa mwadilifu ili kuhakikisha mteja anapata kile anachokistahili,” alisema.
Jaji Mfawidhi aliwaeleza Wawakilishi Binafsi hao kuwa ni vyema wakajitathmini kama utendaji wao unakidhi lengo la kukuza uchumi wa wananchi na kuwavutia wawekezaji na kwa kufanya hivyo watakuwa wametekeleza wajibu wao.
“Hata siku yako ya kustaafu ikifika, tutasema sasa pumzika kwa amani,” Mhe. Dkt. Mlyambina alisema huku akimnukuu Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Hayati Nelson Mandela.
Katika moja ya nukuu zake, Hayati Mandela aliwahi kusema: “Mtu anapofanya kile anachokiona kuwa wajibu wake kwa watu wake na Nchi yake, mtu huyo anaweza kupumzika kwa amani.”
Jaji Mfawidhi aliwaeleza Wawakilishi hao kuwa katika kipindi chote cha ufanyaji kazi pamoja nao amebaini baadhi yao wanafanya kazi nzuri na kila siku huwaombea waendelee kuitetea haki kazi kwa uadilifu na weledi zaidi.
Hata hivyo, Mhe. Dkt. Mlyambia alibainisha mambo kadha ambayo kiuhalisia yanahitaji kufanyiwa maboresho au marekebisho kwa kuwa Wawakilishi hao wamekuwa wakifanya kazi bila ya kuwa na kanuni ya kuwaongoza.
“Hali hii imepelekea kutokea kwa changamoto mbalimbali. Mfano wa changamoto hizo ni pamoja na kutokuwa na anuani za ofisi zinazofikika, hivyo kuleta usumbufu kwa wengi wa wateja ambao wanawachagua kuwawakilisha ambao hufika ofisini kwangu kutaka msaada,” alisema.
Alitaja changamoto nyingine ni baadhi ya Mawakili ambao hawajahuisha leseni zao za Uwakili kufika mahakamani na kujitambulisha kama Wawakilishi Binafsi na baadhi yao kutokujua sheria na kanuni mbalimbali za kazi.
Changamoto nyingine ni Wawakilishi Binafsi kuandaa nyaraka za Mahakama zenye makosa yasiyoweza tibika, baadhi yao kuwa mabingwa wa kutaka kushinda kesi kwa njia za kiufundi na kutokujua wajibu wao wa msingi.
Katika kutatua changamoto hizo, Mhe. Dkt. Mlyambina aliwaeleza Wawakilishi hao kuwa kumekuwa na mijadala mbalimbali iliyowajumuisha Wadau wote wa kazi kuhusiana na weledi pamoja na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu wanayopatiwa na wateja.
Alibainisha kuwa baada ya majadiliano mbalimbali, kamati ikapitisha kuwa lipelekwe ombi kwa Jaji Mkuu wa Tanzania ili waweze kurasimishwa kwa kutungiwa kanuni za kuwaongoza.
“Napenda kuchukua fursa hii kuwafahamisha kuwa ombi hilo tumelifikisha na Jaji Mkuu ameridhia. Tayari nimeunda kamati ya ndani ambayo inaandaa rasimu hiyo ya kanuni ili tuiwasilishe kwa kamati ya wadau wa kazi ili kuipitia na kufanyiwa marekebisho kama yapo na kisha kuiwasilisha kwa Jaji Mkuu,” alisema.
Jaji Mfawidhi alibainisha kuwa wao kama wawakilishi wa wateja wawapo mahakamani na mbele ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi husaidia haki kupatikana na hasa haki kwa njia ya usuluhishi. Alisema kuwa haki inayopatikana kwa suluhu ni bora zaidi kwani haiachi majeraha ya uhasama na uadui.
Alifafanua kuwa kitendo cha kutengeneza mahusiano mazuri baina ya mwajiri na mwajiriwa kutafanya migogoro inayoibuka baina yao kuisha kwa haraka na kuacha mahusiano mazuri baina yao.
“Hii ni kwa sababu kila mmoja bado anamuhitaji mwingine katika ujenzi na ukuaji wa uchumi katika Taifa letu. Hivyo, suluhu ndio silaha nzuri ya kuibeba katika utekelezaji wa majukumu yenu,” Mhe. Dkt. Mlyambia alisema.
Jaji Mfawidhi aliendelea kusisitiza kuwa katika kutekeleza majukumu yao ni vyema wakatumia ushawishi wao ili wateja waweze kumaliza migogoro kwa njia ya suluhu, kwani kitendo hicho huwaacha wakibaki na furaha.
Alisema hatua hiyo inawafanya wateja kutimiza matakwa ya sheria kwa ajili ya kukuza uchumi wao binafsi na wa Nchi kwa ujumla kwakuwa kila mmoja atarejea katika majukumu yake mapema.
Awali akimkaribisha Jaji Mfawidhi kufungua kikao hicho, Mwenyekiti wa Mwakilishi Binafsi, Bw. Sammy Kateregga alisema kuwa kwa sasa wanasubiri utaratibu wa kurasimishwa kwa kuweka kanuni na miongozi ili kukamisha sheria ya Uwakilishi Binafsi.
Alibainisha kuwa hadi kufika hapo wamepitia katika vipindi vigumu ambapo baadhi ya Wawakilishi Binafsi walikosa nidhamu na kufanya au kutenda vitendo ambavyo vilikuwa vinadharirisha taaluma hiyo.
“Jambo hili lilichochea chuki na kuwekewa vizingiti kutoka sehemu mbalimbali. Tuligundua si Wawakilishi tu wenye tabia mbovu bali inatokana na hulka ya mtu mwenyewe, anaweza akawa ni Wakili kahitimu lakini hafanyi kazi kwa weledi,” alisema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni