Jumatatu, 8 Aprili 2024

MENEJIMENTI MAHAKAMA PWANI YAKUTANA KISARAWE

Na Eunice Lugiana-Mahakama, Pwani

 

Menejimenti ya Mahakama Mkoa wa Pwani hivi karibuni ilikutana wilayani Kisalawe kwenye kikao cha robo mwaka kufanya tathmini ya utendaji kazi.

 

Kikao hicho ambacho kiliongozwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi kilifanyika katika ukumbi wa wazi wa Mahakama ya Wilaya Kisarawe.

Akizungumza wakati anafungua kikao hicho, Mhe. Mkhoi aliwataka Mahakimu   Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya kusimamia vyema Mahakama za Mwanzo na kufanya vikao na Mahakimu ili kupanga mikakati ya kuepuka mlundikano wa mashauri.

Alisema kuwa Mahakama za Mwanzo zinapaswa kupewa jicho la karibu ili wananchi wapate haki zao kwa wakati. “Tukizembea tutajikuta tuna mlundikano wa mashauri na jambo hili halikubaliki hata kidogo,” alisema. 

Hakimu Mfawidhi huyo, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kikao hicho, aliwakumbusha Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo kuingiza mashauri kwenye mfumo (MOBILE APP).

Aidha, Mhe. Mkhoi aliwaomba Mahakimu Wafawidhi kuongea na wa Wakuu wa Vituo vya Polisi kuwa wasipeleke kesi mahakamani kama upelelezi haujakamilika.

 

Akawawashauri pia kuwabana Waendesha Mashtaka ili walete mashahidi kwa wakati, hatua itakayowezesha mashauri kusikilizwa kwa wakati. 

 

Awali, akimkaribisha Mwenyekiti wa kikao hicho, Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Pwani, Bw. Moses Minga aliomba Mahakama zote zinapotoa elimu ya sheria kila wiki kuhifadhi maudhui ya somo linalofundishwa kwa ajili ya kumbukumbu.

 

  

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi akiongea wakati wa kikao cha menejimenti katika ukumbi wa Mahakama ya Wilaya Kisarawe.



 Wajumbe wa Kikao cha Menejimenti ya Mahakama Mkoa wa Pwani wakimsikiliza Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mhe. Joyce Mkhoi.



Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha, Mhe. Emmael Lukumai (katikati) akifuatilia Kikao cha Menejimenti. Kulia Ni Mhe.  Emmy Nsangalufu wa Mahakama ya Wilaya Kisarawe na Kushoto ni Afisa Utumishi wa Mahakama ya Wilaya Kibaha, Bi. Malkia Nondo.

 


Mtendaji wa Mahakama ya Mkoa wa Pwani, Bw. Moses Minga akimkaribisha Mwenyekiti wa Kikao, ambaye ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani.

 



Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Mafia, Mhe. Lazaro Magai (wa pili kulia) akifuatilia mjadala wakati wa kikao hicho.


Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama Pwani wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kikao.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni