Jumatatu, 8 Aprili 2024

MKAZI WA PERAMIHO SONGEA AHUKUMUMIWA KIFO

Na Hasani Haufi- Mahakama Kuu, Songea

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, imemhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa mkazi wa Peramiho Songea, Richard Mgina (32) kwa kosa la mauaji ya mtoto Paul Haule mwenye umri wa miaka sita.

Adhabu hiyo imetolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha baada ya kumtia hatiani Mgina kwa kosa hilo alilotenda tarehe 25 Februari, 2023 chini ya Kifungu 197 cha Kanuni ya Adhabu.

Akisoma hukumu kwenye kesi dhidi ya Mgina, Mhe. Karayemaha alisema kwamba Mahakama imefikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka na utetezi na kuthibitisha pasi na shaka kuwa Mshitakiwa alitenda kosa hilo.

Alielezwa kuwa baada ya kutekeleza mauaji hayo, Mshitakiwa alimweka mtoto huyo kwenye mfuko na kwenda kumzika katika shimo la taka ambalo lipo jirani na nyumba waliyokuwa wakiishi.

Aidha, Jaji Karayemaha alieleza kuwa mwanzo mtoto huyo alipotea katika mazingira ya kutatanisha tokea tarehe 21 Februari, 2023 na kisha tarehe 23 mwezi huo huo taarifa zikasambaa kuhusu kupotea kwake.

Aliendelea kueleza kuwa baada ya kukamatwa, Mshitakiwa aliwaongoza polisi kwenda alipomzika mtoto huyo kwenye shimo ambapo awali alidanganya kwa kusema alikuwa amemtupa kisimani.

Jaji Mfawidhi alieleza pia kuwa taarifa ya Daktari inaonesha chanzo cha kifo cha mtoto huyo ni kukosa pumzi kufuatia jeraha kubwa alilokuwa kichwani.


Jengo la Mahakama Kuu Songea.


(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

         


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni