Ijumaa, 19 Aprili 2024

JAJI MKUU WA TANZANIA AHIMIZA MAZINGIRA BORA KAZINI

  •      Asema udanganyifu, kukosa umakini kunafilisi mifuko ya jamii

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Kigoma

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewahimiza waajiri nchini kuhakikisha maeneo ya kazi hayatoi mazingira ya ajali wala vifo kwa wafanyakazi.

Mhe. Prof. Juma ametoa rai hiyo leo tarehe 19 Aprili, 2024 alipokuwa anafungua Kikao Kazi kujadili sheria za kazi ambacho kimewaleta pamoja mkoani hapa Majaji na watumishi wengine wa Mahakama pamoja na Menejimenti ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi na Tume ya Uamuzi na Usuluhishi. 

“Mfuko huu unalindwa na sisi kwa kuangalia mazingira ya kazi. Tupunguze visababishi ambavyo vinaweza kuleta vifo, ajali katika maeneo ya kazi. Hilo ni somo ambalo ni muhimu, tukirudi tuanze kuangalia maeneo yetu ya kazi kama ni rafiki,” amesema.

Jaji Mkuu amebainisha kuwa amepata bahati ya kupitia Sheria ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, kifungu cha 3 (f), ingawa watekelezaji wakubwa ni mfuko, inawataka waajiri kuhakikisha maeneo ya kazi hayatoi mazingira ya ajali wala vifo kwa wafanyakazi.

Mhe. Prof. Juma amesema uwepo wa Kikao Kazi hicho ni muhimu kwani kitawafanya kuyaelewa vizuri mazingira ya kazi na kuleta uelewa wa pamoja wa sheria kati ya wafanyakazi na Watanzania kwa ujumla.

“Kikao kazi hiki pia ni nafasi kwa wadau kujadiliana kwa sababu sheria ni moja, lakini huwa kunakuwa na uelewa unaotofautiana, hivyo ikipatikana fursa ya kujadiliana kati ya mfuko na Majaji, Wasajili, Watendaji husaidia kufahamu sheria kwa undani zaidi,” amesema.

Jaji Mkuu amebainisha kuwa kazi ya mfuko itakuwa rahisi kama kutakuwepo na uelewa unaofanana na kuepusha matumizi ya kanuni za kiufundi zinazolenga kumnyima mfanyakazi haki zake na pia kuweka uwiano mzuri katika malipo.

Mhe. Prof. Juma amesema kuwa ukisoma sheria ya mfuko wa fidia kwa wafanyakazi inaeleza malipo yanayotolewa yasilenge kufilisi mfuko. Amesema mifuko mingi hufilisika kama kutajengekaa tabia za udanganyifu. 

“Ukosefu wa umakini, udanganyifu vyote vimechangia kuua mifuko ambayo ilikuwa na malengo mazuri sana. Tusipokuwa waangalifu, mfuko huu vile vile unaweza kukumbana na tatizo hili. Tukielewa vizuri mantiki ya kuanzishwa mfuko huu tutaufanya uwe endelevu na himilivu,” amesema.

Jaji Mkuu ametumia nafasi hiyo kuhimiza pia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika shughuli zote za kiutendaji ili Taasisi za kimahakama na Wadau wote ziweze kusomana, hatua itakayosaidia kuziba udanganyifu na kuufanya mfuko kuwa himilivu na fidia kupatikana kwa haraka.

Awali, akizungumza kabla ya kumkaribisha Jaji Mkuu kufungua Kikao Kazi hicho, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambia alisema kuwa kumekuwa na vikao kazi vitano ambavyo vimefanyika baina ya Mahakama na Wadau wake Bagamoyo, Mwanza, Arusha, Songea na Kigoma.

Alibainisha kuwa jumla ya Viongozi na watumishi 290 wameshiriki katika Vikao Kazi hivyo, wakiwemo Majaji 70, Naibu Wasajili 33, Watendaji 11, Wadau 48, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi 32 na zaidi ya watumishi wa Mahakama 96.

Alibainisha kuwa katika Kanda ambazo wamefanya mafunzo, kuna mambo ambayo yamekuwa yakiibuliwa na washiriki kwa lengo la kuboresha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi na baadhi ya mapendekezo yaliyoibuliwa yameshaanza kufanyiwa kazi na mfuko.

Mhe. Dkt. Mlyambia alitola mfano suala la mtu ambaye anakuwa hajaridhika na uamuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kukata rufaa kwa Waziri na baadae kwenda katika Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.

“Katika mafunzo yaliyopita imependekezwa kwamba katika kufupisha mlolongo wa kudai fidia, kuanzishwe Baraza (Tribunal) litakaloshughulikia rufaa zinazotokana na maamuzi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia na mifuko mingine ya jamii,” alisema.

Jaji Mfawidhi alibainisha kuwa baada ya mzunguko wa awali wa mafunzo hayo, atawasilisha taarifa jumuishi ikionesha mapungufu na mapendekezo yaliyoibuliwa na washiriki wa mafunzo.

Alibainisha pia kuwa mafunzo hayo yamekuwa na upekee kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kuwa mafunzo ya kwanza kuendeshwa na Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi na Mfuko wa Fidia kwa wafanyakazi na pia kuwa na sura ya muungamo ambapo Jaji mwenye dhamana kutoka Zanzibar amehudhuria.

Alisema kuwa mafunzo hayo yamekuwa na washirikin wengi zaidi wakiwemo Majaji wasioungua 20 kutoka Kanda za Morogoro, Iringa, Songea, Dodoma, Tabora, Shinyanga na Kigoma.

Jaji Mfawidhi alieleza pia kuwa washiriki wamejifunza mambo mengi nje ya jamii ya Kigoma, ikiwemo kujua Ziwa Tanganyika limeundwa na sam aki wawili ambao ni Tanga mwenye uwezo wa kuruka juu zaidi na Nyika mwenye shoti za umeme ambaye ili kuweza kumwanda kama kitoweo ni lazima achunwe Ngozi yake.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (juu na chini) akisisitiza jambo alipokuwa anafungua Kikao Kazi kujadili sheria za kazi leo tarehe 19 Aprili, 2024 mkoani Kigoma.



Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambia akibainisha mambo fulani kabla ya kumkaribisha Jaji Mkuu kufungua Kikao Kazi hicho.


Sehemu ya Majaji kutoka Kanda mbalimbali za Mahakama Kuu ya Tanzania (juu na chini) wakiwa katika Kikao Kazi hicho.

 

 Mwenyekiti wa Mahakama Kuu Zanzibar, Divisheni ya Kazi, Mhe. Aziza Idd Sued (kushoto) akiwa na Majaji wa Mahakama ya Tanzania kwenye Kikao Kazi hicho.


 

Sehemu ya Viongozi wa Mahakama na Wadau (juu na chini) wakishiriki kwenye Kikao Kazi hicho.

Wadau na watumishi wa Mahakama (juu na chini) wakifuatilia kilichokuwa kinajiri wakati wa ufunguzi wa Kikao Kazi uliofanywa na Jaji Mkuu wa Tanzania.

Picha na Aidan Robert-Mahakama Kigoma

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni