Ijumaa, 19 Aprili 2024

MAHAKAMA YA TANZANIA KIMBILIO LA WANANCHI

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Kigoma

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Bw. Emanuel Humba ameupongeza uongozi wa Mhimili wa Mahakama, chini ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, kwa mageuzi makubwa ambayo yameifanya Mahakama ya Tanzania kuwa kimbilio la Wananchi.

Bw. Humba ametoa pongezi hizo leo tarehe 19 Aprili, 2024 alipokuwa anawasilisha salamu zake kwenye Kikao Kazi kujadili sheria za kazi kinachofanyika katika Ukumbi wa Lake Tanganyika mkoani hapa.

Kikao Kazi hicho ambacho kimeratibiwa na Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi kwa kushirikiana na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kinawaleta pamoja Majaji wa Mahakama Kuu kutoka Kanda mbalimbali na Mahakama Kuu Zanzibar na Wadau kutoka Mfuko huo na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi. 

Akizungumza wakati wa kutoa salamu zake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko amesema uongozi wa Mahakama umeipa heshima kubwa Mahakama ya Tanzania kiasi cha kuwafanya Wananchi kukimbilia mahakamani ili kupata haki stahiki wanapokabiliana na changamoto mbalimbali.

“Tunapenda, kwa kweli kukupa heshima ya hali ya juu. Mahakama kwa sasa hivi inaonesha ushirikiano mzuri sana. Huko nyuma kulikuwa na mashaka mashaka, raia walikuwa wanaiogopa Mahakama, Mahakama zenyewe zilikuwa zinatisha…

“…Lakini sasa ni tofauti sana, kwa malezi yako, Mahakama na Wananchi wanavuna mbivu na wanapenda kukimbilia mahakamani. Binafsi, nakushukuru sana,” Bw. Humba alimweleza Jaji Mkuu ambaye aliyekuwa Mgeni Rasmi kwenye ufunguzi wa Kikao Kazi hicho.

Katika salamu zake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ameeleza kuwa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi ni Taasisi ya Hifadhi ya Jamii ulioanzishwa chini ya Kifungu cha 5 cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi kwa lengo la kushughulikia masuala ya fidia kwa wafanyakazi wanaoumia au kufariki katika utekelezaji wa majukumu yao ya ajira.  

Amesema kwamba Mfuko huo ulianza kutekeleza majukumu yake tarehe 01 Julai, 2015 na ulipewa kipindi cha mpito cha mwaka mmoja kwa ajili ya maandalizi ya kulipa fidia na hivyo kuanza kulipa fidia rasmi tarehe 01 Julai 2016.

“Napenda kukuhakishia kuwa Mfuko unaendeshwa kwa ufanisi mkubwa na umepata mafanikio makubwa katika kutekeleza malengo yake. Tulipoanza mwaka 2016, tulilipa fidia kwa Wafanyakazi ya Shilingi za Kitanzania Bilioni 3.88. Mpaka kufikia mwaka 2016/2017 mfuko umelipa mafao ya Shilingi za Kitanzania Bilioni 23.58,” Bw. Humba alimweleza Jaji Mkuu.

Amebainisha pia kuwa michango ya Waajiri iliyokusanywa imeongezeka kutoka Shillingi za Kitanzania 68.40 bilioni kwa mwaka 2015/2016 hadi kufikia Shillingi za Kitanzania 86. 48 bilioni kwa mwaka 2022/2023.  

Kdhalika, Mwenyekiti wa Bodi ameeleza kuwa pamoja na mafanikio hayo, tathmnini ya uhai na uendelevu wa Mfuko iliofanywa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) inaonesha kwamba Mfuko unauhimilivu kwa kipindi cha miaka 30 ijayo.

“Hiki ni kitu cha kukilinda, Mifuko mara kwa mara inaanza vizuri, isipolindwa inapoteza njia,” alisema. Amebainisha pia kuwa Mfuko umekuwa na utaratibu wa kushughulikia madai ya wanufaika kwa wakati uliowekwa kisheria.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Dkt. John Mduma, akizungumza wakati wa Kikao Kazi, hicho alieleza kuwa shughuli za Mfuko haziwezi kukamilika bila kupata ushirikiano kutoka mahakamani.

Alieleza kuwa kwa sasa maamuzi wanayoyatoa yanaangaliwa na Waziri mwenye dhamana pale ambapo kunakuwepo na kutokuridhika kwa upande mmoja na suala hufikishwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi kama mhusika asiporidhishwa na maamuzi ya Waziri.

“Kwa hiyo, unaweza kuona jinsi Mahakama ya Tanzania inavyoingia katika masuala ya fidia. Pia huwa tunakutana katika kuamua masuala ya mirathi ambapo tunategemea maamuzi yanayotokewa na Mahakama,” alisema.


Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Bw. Emanuel Humba akizungumza katika Kikao Kazi kinachofanyika mkoani Kigoma leo tarehe 19 Aprili, 2024.


Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Dkt. John Mduma akieleza jambo wakati wa Kikao Kazi hicho.


Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati). Wengine ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina (wa pili kushoto), Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Dkt. John Mduma (wa pili kulia), Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu, Kanda ya Kigoma, Mhe. Augustine Rwizile (wa kwanza kushoto) na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Bw. Emanuel Humba (wa kwanza kulia).


Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu kutoka Kanda mbalimbali na Mwenyekiti wa Mahakama Kuu Kazi Zanzibar.

Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu kutoka Kanda mbalimbali na Mwenyekiti wa Mahakama Kuu Kazi Zanzibar wanaohudhuria Kikao Kazi hicho.


Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Viongozi na Watumishi wa Mahakama wanaohudhuria Kikao Kazi hicho.



Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Menejimenti ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi na Tume ya Uamuzi na Usuluhishi.

Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na watumishi kutoka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni