Ijumaa, 19 Aprili 2024

WANAFUNZI SHULE YA SEKONDARI MOROGORO WASHANGAZWA NA MABORESHO MAHAKAMANI


Na Evelina Odemba – Mahakama, Morogoro

 

Hivi karibuni Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Morogoro walitembelea Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro ili kujifunza maboresho yaliyofanywa na Mahakama ya Tanzania katika kurahisisha shughuli za utoaji haki.

 

Wanafunzi hao walipokelewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Morogoro, Mhe. Mary Kallomo, ambaye aliwapa elimu ya muundo wa Mahakama na namna unavyoshirikiana katika kufanya kazi.

 

Mhe. Kallomo aliwaeleza wanafunzi hao namna Mahakama ya Tanzania imefanya maboresho katika miundombinu ya majengo, mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na namna huduma kwa mteja inavyotolewa.

 

“Nawapa elimu hii kwa manufaa yenu na kwa jamii nzima, ni imani yangu kuwa wote mliopata ufafanuzi huu mtaenda kuwa mabarozi wazuri katika jamii kuhusiana na namna ambavyo maboresho yaliyofanywa na Mahakama ya Tanzania yanavyomrahisishia mwananchi kupata haki” alisema.

 

Naye Kaimu Afisa TEHAMA wa Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Bw. Tofiki Sumbuo aliwapitisha wanafunzi hao katika mifumo ya inayotumiwa na Mahakama, jambo lililowavutia namna usikilizaji wa mashauri kwa njia ya mtandao unavyofanyika.

 

Kwa upande wake, Kiongozi wa Wanafunzi hao, Bi. Khadija Mrisho alisema kuwa wamevutiwa na namna ambavyo Mahakama ya Tanzania inavyofanya kazi na wamejifunza kuhusu mambo mengi na mazuri ambayo hapo kabla hawakuwahi kuyajua. 

 

Aliongeza kuwa wamevutiwa siku moja watakuwa sehemu ya mnyororo wa watoa huduma ya haki kwa wananchi mara watakapohitimu elimu yao.

 

Mwanafunzi mwingine, Nasma Wenzi alisdhangazwa na ukarimu ulioneshwa na watumishi kuanzia katika lango la kuingilia hadi katika maeneo mbalimbali waliyotembelea mahakamani hapo.

 

“Kipindi tunaingia getini tulikuwa na hofu ,tukidhania kila mtu ndani ya jengo hili ni mkali, lakini baada ya kupokelewa tumegundua kuwa watumishi ni wakarimu na wametuelekeza kwa upendo mpaka hofu tuliyokuwa nayo ikayeyuka na tukawa huru kuuliza maswali,” alisema.

 

Wakiwa kituoni hapa wanafunzi hao walipata fursa ya kutembelea Mahakama ya Watoto, Mahakama ya Wazi, Ofisi za wadau wa Mahakama pamoja na Ofisi ya TEHAMA.

 


 Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Morogoro, Mhe. Mary Kallomo akiwa katika picha ya Pamoja na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Morogoro ambao walitembelea Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki ili kujifunza.


 

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Morogoro, Mhe. Mary Kallomo akitoa elimu kwa Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Morogoro.


 

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Morogoro, Mhe. Mary Kallomo akiwaonesha Wanafunzi hao ofisi mbalimbali zilizopo ndani ya Jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki.


 

Kaimu Afisa TEHAMA wa Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Bw. Tofiki Sumbuo akiwaonesha Wanafunzi hao baadhi ya mifumo inayotumiwa na Mahakama ya Tanzania.


 

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Morogoro wakiwa katika ukumbi wa Mahakama ya Wazi.


 


Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Morogoro wakisikiliza kwa makini elimu iliyokuwa ikitolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Morogoro, Mhe. Mary Kallomo walipotembelea jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Kigoma)

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni