Ijumaa, 19 Aprili 2024

MAJAJI WASHAURI SHERIA KUPANUA UWIGO WA MAFAO KWA WAFANYAKAZI

Na Aidan Robert-Mahakama, Kigoma

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Dkt. Eliamani Laitaika ameshauri sheria inayosimamia fidia kwa wafanyakazi kuongeza uwigo wa mafao, ikiwemo kutoa fidia kwa wale wanaoathirika kiakiri wanapotekeleza majukumu yao.

 

Mhe. Laitaika ametoa ushauri huo leo tarehe 19 Aprili, 2024 alipokuwa akichangia mada kwenye Kikao Kazi kujadili sheria za kazi kinachofanyika kwenye Ukumbi wa Lake Tanganyika mkoani hapa.

 

“Ni vyema sheria ikatambua kulipa fidia kwa mtu ambaye anapata athari za kiakili kwani ni kiungo ambacho kinaathirika kwa kiwango kikubwa na hakionekani kwa mhanga, lakini uwezo wake kupungua au kufa kabisa na kukosa ufanisi katika kazi kutokana adha ya vifaa vya kielekroniki vinavyotumika mahala pa kazi na kutumia kwa muda mrefu,” amesema.

 

Amebainisha kuwa sheria ya fidia kwa wafanyakazi imetoa fidia pekee kwa mfanyakazi ambaye atapata ajali au kifo au ugonjwa pekee, wakati kwa maisha ya sasa wafanyakazi wengi wanatumia asilimia kubwa kwenye akiri.

 

Kwa upande wake, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Majadiliano katika kikao hicho, amesema sheria ya sasa inayosimamia fidia kwa wafanyakazi inatoa changamoto kadhaa kwa baadhi ya vifungu hasa pale inapotekelezwa katika maamuzi mbalimbali.

 

Akiwasilisha mada yake katika kikao kazi hicho, Mkuu wa Huduma za Sheria wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Bw. Ibrahimu Siyovelwa, amesema kuwa Mfumo ni Tasisi ya Hifadhi ya Jamii iliyoundwa kwa mujibu wa Sheria kwa lengo la kushughulikia masuala ya fidia kwa wafanyakazi waliopo katika sekta ya umma na binafsi ambao wataumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi wanazozifanya kwa mujibu wa mikataba ya ajira zao na wategemezi wa mfanyakazi atakayefariki dunia kutokana na ajali au ugonjwa uliotokana na kazi.

 

Amesema kuwa ulipwaji wa mafao ya fidia unahusisha matukio ya ajali, ugonjwa au kifo yaliyotokea kuanzia tarehe 01, Julai 20216 na mpaka sasa. Bw. Siyovelwa amebainisha kuwa madai ya fidia yanapaswa kuwasilishwa ndani ya siku au kipindi kisichozidi miezi 12 tokea tukio husika lilipotokea au kugundulika. 


Aidha alibainisha kuwa Mfuko huo unatoa mafao ya huduma ya matibabu, fidia ya ulemavu wa muda, fidia ya ulemavu wa kudumu, malipo ya anayemhudumia mgongwa, huduma za utegemezi, msaada wa mazishi na malipo kwa wategemezi.

 

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tathimini Mfuko wa Hifadhi ya Jamii, Dkt. Abulsaalam Omary amesema wanafanya tathimini ya fidia kwa madhara ili kutoa fidia stahiki katika ulemavu wa kudumu na fao hilo pia hulipwa kwa mfanyakazi aliyepata ulemavu kwa kiasi ambacho kimeathiri uwezo wake wa kutimiza majukumu yake kazini.

 

Naye Bw. Rashidi Wabhike, Mkazi wa Kigoma ambaye ni mnufaika amesema hakika Mfuko huo umekuwa mkombozi wa maisha yake  baada ya kupata ajali ya shoti ya umeme alipokuwa akitekeleza majukumu wake kule mkoani Arusha alipopata ulemavu wa kudumu wa mguu wake wa kushoto.

 

Ameeleza kuwa aliondolewa kazini na baadaye Mfuko huo kuchukuwa jukumu baada ya kupokea taarifa ya mfanyakazi huyo kupata ajali, ambapo matibabu yake yote yalisimamiwa na Mfuko na hivi sasa anaendelea vyema baada kumwezesha kupata mguu wa bandia baada ya mguu wake halisi kuondolewa kutokana na kuharibiwa na shoti ya umeme.

 

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Dkt. Eliamani Laitaika, akisikiliza kwa makini maelezo ya muwasilisha mada mara baada ya kutoa ushauri kuhusu Sheria ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi katika kikao kazi cha kujadili sheria za kazi leo tarehe 19 Aprili, 2024 kinachafanyika katika ukumbi wa Lake Tanganyika Kigoma.


 

Mkurugenzi wa Huduma za Tathimini Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Dkt. Abulsalaam Omary, akiwasilisha mada katika kikao kazi hicho.





Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Bw. Abraham Siyovelwa, akisisitiza japo wakati akiwasilisha mada.


Naibu Msajili wa mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro, Mhe. Fadhili Mbelwa akiwasilisha hoja. Kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma, Mhe. Gadiel Mariki na kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, Mhe. Pamela Mazengo.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Kigoma)

 

  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni