Jumamosi, 20 Aprili 2024

CHOMBO MAALUM CHANUKIA KUSHUGHULIKIA RUFAA ZA WAFANYAKAZI KUHUSU FIDIA

  • Waajiri ambao hawajasajiliwa, kuwasilisha michango kwa wakati kukiona

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Kigoma

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Deogratius Ndejembi ameridhia kuanzishwa kwa chombo maalumu kitakachokuwa kinashughulikia rufaa za wafanyakazi baada ya maamuzi ya fidia yanayotolewa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

 

Mhe. Ndejembi ametoa ridhaa hiyo leo tarehe 20 Aprili, 2024 alipokuwa akifunga Kikao Kazi kujadili sheria za kazi kilichokuwa kinafanyika kwenye Ukumbi wa Lake Tanganyika mkoani hapa kilichowaleta pamoja Majaji na Watendaji wa Mahakama na Menejimenti ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi.

 

 “Nimesikia kilio hiki cha kuwa na chombo maalum kwa ajili ya kushughulikia masuala haya ya fidia hasa kwa wale ambao watakuwa hawajaridhika na maamuzi yanayotolewa. Naamini kwenye kikao kichacho tutakapokutana tutakuwa tumeanza kupiga hatua kuelekea kuwa na chombo hiki,” amesema.

 

Waziri Ndejembi amebainisha kuwa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, kwa kushirikiana na Kurugenzi ya Hifadhi ya Jamii iliyochini ya Wizara anayoisimamia, wanaendelea na uchambuzi wa maboresho ya Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi.  

 

Amesema kuwa uchambuzi huo unatarajiwa kuja na andiko kuhusu kuanzishwa kwa chombo maalum cha kusimamia rufaa zinazotokana na masuala ya hifadhi ya jamii badala ya utaratibu wa sasa wa rufaa hizo kuwasilishwa kwa Waziri mwenye dhamana ya masuala ya kazi.  

 

“Ni matumaini yangu kuwa katika kikao kazi hiki, mmepata fursa ya kutoa maoni zaidi kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utekelezaji na uboreshwaji wa Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi,” amesema.

 

Mhe. Ndejembi ameeleza pia kuwa Serikali kupitia Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi imefikia uamuzi wa kutoa mafunzo kutokana na kutambua umuhimu na nafasi ya Majaji na Watendaji wengine wa Mahakama katika mchakato wa kutoa haki. 

 

Amesema kwamba mchakato huo, pamoja na mambo mengine, unahusisha namna ya kushughulikia madai ya fidia kwa wafanyakazi wanaogua au kuumia wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao ya kazi kwa mujibu wa mikataba yao. 

 

Aidha, Waziri huyo ameeleza kuwa mchakato huo pia unahusisha namna ya kupata haki katika mamlaka ya rufaa pale mfanyakazi hatakuwa ameridhika na maamuzi ya fidia kwa mujibu wa Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi.

 

Hivyo, akabainisha kuwa pamoja na gharama zinazotumika katika kuendesha kikao kazi hicho ilikuwa ni lazima kifanyike ili kuimarisha ushirikiano na kujenga uelewa wa pamoja katika kusimamia madai yanayohusiana na fidia kwa wafanyakazi.  

 

“Nimefurahi kwa jinsi mlivyotumia kikao hiki pamoja na vilivyofanyika awali kufanya uchambuzi wa sheria za kazi, hususani ile ya Fidia kwa Wafanyakazi na kutoa maoni ya kuboresha sheria hiyo,” amesema.

 

Mhe. Ndejembi alitumia fursa hiyo kuushukuru Uongozi wa Mahakama kwa kukubali na kuwaruhusu Majaji na Watendaji wa Mahakama kushiriki kikao kazi hicho muhimu kinacholenga kujengeana uwezo pamoja na kubadilishana uzoefu katika masuala ya fidia kwa wafanyakazi na sheria za kazi kwa ujumla wake.

 

Hata hivyo, Waziri huyo aliusisitiza Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kuongeza bidii na kasi zaidi katika kushughulikia madai kwa wateja wao ili waendane na ile kauli mbiu ya Mfuko ya “Fidia Stahiki na kwa Wakati.” 

 

Kadhalika, aliwataka kuongeza bidii katika kuwabana na kuwashughulikia Waajiri wote wanaokaidi matakwa ya Sheria kwa kutojisajili na kutowasilisha michango kwa wakati. 

 

Awali, akimkaribisha Waziri kufunga Kikao Kazi hicho, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina, alieleza kuwa jukwaa hilo alimekuwa la daraja la juu kuliko yote ambayo yamewahi kufanyika.

 

Alisema kuwa kikao cha kwanza kilifanyika Bagamoyo kwa kuhusisha Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi pamoja na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi Kanda ya Dar es Salaam na Pwani na kufuatiwa na kikao cha pili kilichofanyika Mwanza kwa kuhusisha Kanda zote zinazotoka Kanda ya Ziwa, yaani Shinyanga, Musoma, Mwanza na Bukoba.

 

Mhe. Dkt. Mlyambina alimweleza Waziri kuwa baada ya kikao cha Mwanza walielekea Arusha na kuhusisha Mikoa ya Tanga, Manyara, Kilimanjaro na Arusha kabla ya kuelekea Songea ambapo Kanda za Sumbawanga, Mbeya, Iringa na Songea yenyewe zilihusishwa.

 

“Leo tupo hapa Kigoma na tumewaleta wenzetu kutoka Morogoro, Dodoma, Tabora na Majaji wenzetu ambao hawakushiriki kwenye vikao vilivyopita kutoka Shinyanga, Iringa na Sumbawanga,” amesema.

 

Amebainisha pia kuwa Kikao Kazi hicho kimekuwa, kwa namna ya kipekee, na sura ya muungano kufuatia ushiriki wa Jaji wa Mahakama Kuu na Mwenyekiti wa Mahakama ya Kazi Zanzibar, Mhe. Aziza Idd Sued, ambaye ametoa uzoefu mzuri kuhusu masuala ya kazi na wamejisikia kuwa Taifa moja.

 

Jaji Mfawidhi alimweleza Waziri kuwa uwepo wa vikao kazi kama hivyo ni muhimu kwani vinawajengea uwezo zaidi katika kuelewa vema kuhusu maeneo ambayo mfanyakazi anaweza kulipwa fidia, vigezo vinavyotumika, hatua stahiki na taratibu mahsusi katika ufuatiliaji wa madai ya fidia kwa wafanyakazi.

 

“Pia vinatusaidia kuainisha baadhi ya mapungufu yaliyopo katika sheria husika. Mahakama na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi ndiyo wanaotafsiri sheria. Hivyo, tunapowakusanya watumishi hawa kwa pamoja inakuwa rahisi kujua sheria hii katika kuipima inakuwa na mapungufu yapi na namna gani ya kuondokana nayo,” amesema.

 

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Bw. Emanuel Humba, alimweleza Waziri kuwa jambo kubwa moja lililosisitizwa na washiriki wakati wa majadiliano ni kuanzishwa kwa chombo mahususi cha kushughulikia rufaa zinazotokana na maamuzi yanayofanywa na taasisi za hifadhi ya jamii.

 

“Suala hili limejitokeza katika vikao kazi vyote vilivyofanyika. Sisi kama Bodi ya Wadhamini tumepokea ushauri huu na tayari tuliuwasilisha katika Wizara yako kwa hatua zaidi za utekelezaji ambapo mtangulizi wako aliagiza Kurugenzi ya Hifadhi ya Jamii kuanza kuaanda andiko la mapendekezo ya utekelezaji wake,” alisema.

 

Bw. Humba alisema kuwa yeye kama Mwenyekiti wa Bodi anaahidi kuendeleza ushirikiano na Mahakama na Taasisi nyingine zenye dhamana ya kutekeleza sheria za kazi kwa lengo la kuimarisha utoaji huduma kwa wananchi.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Deogratius Ndejembi akisisitiza jambo alipokuwa anafunga Kikao Kazi kilichowaleta pamoja Majaji na Wadau mbalimbali kujadili sheria za kazi.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina akiwasilisha salamu za Mahakama kwenye Kikao Kazi hicho.


Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Bw. Emanuel Humba akifafanua jambo wakati wa hafla hiyo.


Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Dkt. John Mduma akieleza jambo wakati wa Kikao Kazi hicho.

 

Mwenyekiti wa Mahakama Kuu Zanzibar, Divisheni ya Kazi, Mhe. Aziza Idd Sued (kushoto) akiwa na Majaji wa Mahakama ya Tanzania kwenye Kikao Kazi hicho.




Sehemu ya Majaji kutoka Kanda mbalimbali za Mahakama Kuu ya Tanzania (juu na chini) wakiwa katika Kikao Kazi hicho.



Sehemu ya Viongozi wa Mahakama na Wadau (juu na chini) wakishiriki kwenye Kikao Kazi hicho.


Meza Kuu inayoongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Deogratius Ndejembi (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu kutoka Kanda mbalimbali na Mwenyekiti wa Mahakama Kuu Kazi Zanzibar.


Meza Kuu inayoongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Deogratius Ndejembi (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu kutoka Kanda mbalimbali na Mwenyekiti wa Mahakama Kuu Kazi Zanzibar.


Meza Kuu inayoongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Deogratius Ndejembi (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Viongozi na watumishi wa Mahakama waliokuwa wanahudhuria Kikao Kazi hicho.


Meza Kuu inayoongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Deogratius Ndejembi (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Menejimenti ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi.


Meza Kuu inayoongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Deogratius Ndejembi (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya watumishi wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni