Jumamosi, 20 Aprili 2024

KIKAO KAZI KUJADILI SHERIA ZA KAZI CHAHITIMISHWA

·      Mafanikio lukuki yabainishwa

·      Waziri mwenye dhamana ahimiza ushirikiano endelevu

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Kigoma

 

Kikao Kazi kilichowaleta pamoja Majaji na Watumishiwa Mahakama ya Tanzania na Menejimenti ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi kujadili sheria za kazi, kilichokuwa kinafanyika katika Ukumbi wa Lake Tanganyika mkoani hapa, kimehitimishwa leo tarehe 20 Aprili, 2024.

 

Akihitimisha Kikao Kazi hicho, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina ameushukuru Uongozi wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi(WCF) kwa kuwezesha kikao kazi hicho ambacho kimekuwa na manufaa makubwa katika kujadili Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi kwa nia ya kuiboresha kwa ustawi wa Waajiri na Wafanyakazi.

 

“Nichukue fursa hii pia kumshukuru Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kutokana na majukumu makubwa aliyokuwa nayo katika kuijenga Mahakama ya Tanzania lakini aliweza kutenga muda wa kujumuika nasi na kukubali ombi letu la kutufungulia mafunzo haya yaliyohusu kuelimisha zaidi kuhusu sheria ya fidia kwa wafanyakazi na kazi za mfuko wa fidia kwa wafanyakazi,” amesema.

 

Jaji Mfawidhi ameeleza kuwa mfululizo wa vikao kazi hivyo umekuwa wa mafanikio makubwa ambapo jumla ya washiriki 290, wakiwemo Majaji 70, Naibu Wasajili 33, Watendaji 11, Wadau wengine wa kazi 48, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) 32 na Watumishi wa Mahakama 96 wa kada mbalimbali wameweza kupata mafunzo hayo. 

 

Aidha, Mhe. Dkt. Mlyambina ametaja mafanikio mengine ni pamoja na baadhi ya mambo yaliyoibuliwa yameanza kufanyiwa kazi kama vile mchakato wa kuanzishwa kwa baraza la kushugulikia masuala ya fidia (Tribunal).

 

Wakati wa Kikao Kazi hicho, mada mbalimbali ziliwasilishwa, ikiwemo iliyowasilishwa na Mkuu wa Kitengo cha Sheria cha Mfuko kuhusu Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi, taratibu za kuwasilisha na kushugulikia madai ya fidia na tathmini za madai ya fidia. 

 

Katika mada ya pili iliyotolewa na Mkurugenzi wa Uendeshaji wa mfuko, Bw. Hashim Peter alifahamisha dhima ya mfuko ambayo ni kuwepo muda wote kutoa huduma za fidia kwa mdai. 

 

Pia alielezea ufanisi wao katika kutekeleza majukumu ya mfuko, ikiwemo kutoa elimu ya sheria, taratibu na mfumo, ushirikiano na taasisi nyingine zinazotoa huduma za fidia kwa wateja, kumpatia matibabu kwa wakati mwajiriwa ili arudi kazini kwa haraka na kuhakikisha ulipwaji wa fidia unalingana na athari.

 

Katika uwasilishaji wa madai ya ajali kama sheria inavyoelekeza inatakiwa mfanyakazi atoe taarifa kwa mwajiri ndani ya siku mbili, mwajiri atoe taarifa kwenye Mfuko ndani ya siku saba za kazi, ikiwa ukomo wake ni miezi 12 na wakati matibabu yakiendelea Mfuko wataendelea na uchunguzi wa ajali.

 

Mada ya tatu ilitolewa na Mkurugenzi wa Tathmini wa Mfuko, Dkt. Omary…..ambaye, pamoja na mambo mengine, aliwafahamisha washiriki kuwa kuna kufariki kazini na kufariki kutokana na kazi na kwamba Mfuko wanashugulika na kufariki kutokana na kazi. 

 

Pia alielezea tofauti kati ya ulemavu wa muda na ulemavu wa kudumu na kueleza kuwa hata fidia zake hutofautiana na kisha akaelezea thamani ya kila kiungo endapo kitakuwa kimekatika au kukatwa kutokana na ajali iliyosababishwa na kazi kama vilivyoainishwa kwenye sheria.

 

Pia kulikuwepo na mada kuhusu Mikataba ya Kimataifa inayohusiana na Masuala ya Fidia kwa Wafanyakazi na ile inayohusiana na usalama na fidia kwa wafanyakazi ambayo inataka mwajiri kuwakinga waajiriwa ili wawe salama na inapotokea mwajiriwa amepata ugonjwa au ajali kutokana na kazi, aweze kufidiwa yeye na au wategemezi wake.

 

Kikao Kazi hicho kilifunguliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ambaye, pamoja na mambo mengine, alisisitiza umuhimu wa kuulinda mfuko huo kwa waajiri kuangalia mazingira ya kazi na kupunguza visababisho vya ajali kazini.

 

Hatua hiyo itaimarisha uhimilisho wa Mfuko kwani ajali kwenye maeneo ya kazi zikipungua itafanya utoaji wa fidia pia kupungua, hivyo kuimarisha mfuko na wenyewe utatoa huduma bora kwa wahanga. 

 

Jaji Mkuu alitoa rai pia kwa washiriki kuhakikisha mazingira ya kazi hayasababishi ajali na kwamba pesa za mfuko hazipotei kwa kulipa fidia kwa mazingira yaliyoshindwa kuwekwa vizuri.

 

Kikao Kazi hicho kimefungwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Deogratius Ndejembi ambaye, pamoja na mambo mengine, ameagiza Mfuko uendelee kutoa mafunzo kwa Mahakama kwa lengo la kujenga uelewa wa pamoja katika kutekeleza Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi.

 

Kadhalika, Waziri Ndejembi amesisitiza Mfuko na Mahakama kuendelea kushirikiana katika kuhudumia Wananchi na alionesha utayari wake wa kupokea maoni yatakayotolewa katika Kikao Kazi hicho na kuyafanyia kazi.


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina (juu na chini) akizungumza vacati wa kuhitimisha kikao kazi kujadili sheria za kazi kilichokuwa kinafanyika mkoani Kigoma.



Sehemu ya Majaji na watumishi wa Mahakama pamoja na Wadau wa masuala ya kazi wakimsikiliza Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina (hayupo kwenye picha).


Sehemu ya washiriki wa Kikao Kazi hicho (juu na chini) wakimsikiliza Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina (hayupo kwenye picha).



Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Bw. Emanuel Humba (kushoto) akimkabidhi zawadi Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina.


Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Dkt. John Mduma (katikati) akimkabidhi zawadi Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina. Anayeshuhudia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Bw. Emanuel Humba.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni