Jumamosi, 20 Aprili 2024

MAJAJI WASHAURI MIKATABA YA KIMATAIFA IZINGATIWE KUBORESHA MAZINGIRA YA KAZI

Na Aidan Robert-Mahakama, Kigoma

 

Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Biswalo Mganga amewashauri Waajiri kuzingatia mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia ili kuboresha mazingira ya kazi.

 

Akichangia hoja kwenye Kikao Kazi kujadili sheria za kazi leo tarehe 20 Aprili, 2024 katika ukumbi wa Lake Tanganyika mkoani hapa, Mhe. Mganga alibainisha kuwa kuna jumla ya mikataba 88 ya Kimataifa inayohusiana na kazi na mifuko ya Jamii.

 

Alisema kwamba jumla ya mikataba 10 iliyoridhiwa na Tanzania inamtaka mwajiri kuhakikisha mazingira ya kazi katika taasisi za umma inakuwa rafiki ili kupunguza kutokea kwa ajali na magonjwa kwa wafanyakazi na kwamba Mifuko wa Hifadhi ya Jamii itabeba mzigo mkubwa kama mikataba hii haitazingatiwa.

 

Aidha, Mhe. Mganga alisema kuwa mkataba wa usalama na afya kazini unawahusu wafanyakazi wote wa umma ambao unamtaka mwajiri kuweka mazingira wezeshi na salama kwa kazi.

 

“Kama mikataba ya kimataifa ikizingatiwa itasaidia Majaji kuboresha maamuzi yao katika migogoro mingi ya kazi inayofikishwa mahakamani,” alisema.

 

Kwa upande wake, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Silvia Lushasi alishauri utekelezaji wa maamuzi ya Tume ya Usuluhishi na Uamuzi urudishwe katika mamlaka hiyo ili kupunguza mlolongo wa kupeleka katika ofisi ya Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania. 

 

Alibainisha kuwa hatua hiyo itaongeza ufanisi wa utekelezaji wa maamuzi ya Tume hasa katika migogoro ya kazi.

 

Naye Kamishina wa Kazi Tanzania Bara, Bi. Suzan Mkangwa alijulisha kikao hicho kuwa Serikali inakusudia kuridhia mikataba ya kimataifa sita ya sheria za kazi ambayo itasaidia kuboresha mazingira ya kazi pamoja na kutoa maelekezo ya kazi katika kutimiza wajibu wa mwajili na mwajiliwa mahali pakazi.

 

 Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Bw. Usekelege Mpulla alieleza kuwa sheria ya kazi ya mwaka 2004 ambayo imerejelewa mwaka 2019 imeanzisha taasisi ya kazi fungamanishi yenye mikakati mahsusi ya kutunga sheria, dira na usimamizi wa utatuzi wa migogoro ili kuhakisha taasisi zilizoanzishwa na sheria hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano na kusomana katika kutoa huduma za kazi kwa wananchi.

 


Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Biswalo Mganga, akifafanua jambo wakati wa kikao kazi hicho kilichohitimishwa leo tarehe 20 Aprili, 2024 katika ukumbi wa Lake Tanganyika mkoni Kigoma.


Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Silvia Lushasi, akitoa ushauri katika kikao kazi hicho.


Kamishina wa Kazi Tanzania Bara, Bi. Suzan Mkangwa, akitoa mchango wake juu ya mikataba ya sheria za kazi na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii.


Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Bw. Usekelege Mpulla, akifafanua jambo wakati akiwasilisha mchango wake katika kikao kazi hicho.


Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Dkt. Eliamani Laitaika, akiteta jambo na Mwakilishi wa Habari Mahakama Kanda ya Kigoma mara baada ya kumalizika kwa kikao kazi hicho.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Kigoma)

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni