Na. Francisca Swai, Mahakama - Musoma.
Menejimenti ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, imekutana Wilayani Tarime kwa lengo la kupata tathmini ya utendaji kazi ya mwaka 2023, kujadiliana na kuweka mikakati madhubuti ya utekelezaji kwa mwaka 2024.
Kikao hicho cha Mnenejimenti Kanda ya Musoma, kilifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kiliongozwa na Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo Mhe. Fahamu Mtulya, ambapo aliwapongeza watumishi wote kwa utendaji kazi mzuri uliosaidia kuvuka mwaka 2023 bila kuwa na mashauri mlundikano na kuifanya Kanda ya Musoma kuwa ya pili katika utendaji kazi wake.
Akitoa pongezi hizo Mhe. Fahamu Mtulya alisema kupitia thathmini iliyotolewa kwenye kikao cha Utendaji kazi cha Majaji Wafawidhi kilichofanyika mwezi Februari jijini Arusha, Mahakama Kuu Musoma ilishika nafasi ya pili kwa kuwa na kiwango kikubwa cha umalizaji na uondoshaji wa mashauri.
Sambamba na pongezi hizo Mhe. Fahamu Mtulya alisisitiza watumiaji wa mfumo wa kielektroniki wa kuratibu na kusimamia mashauri Mahakamani (e-CMS), kuutumia mfumo huo vizuri ikiwa ni pamoja na kuondoa mashauri yaliyomalizika kwa wakati.
Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Musoma Mhe. Salome Mshasha aliwasisitiza viongozi wote waliohudhuria kikao hicho kuzingatia maelekezo mbalimbali yanatolewa na viongozi wa juu ili yatusaidie kuboresha zaidi utendaji wa kazi.
Sambamba na pongezi hizo, viongozi hao walisisitiza mambo mbalimbali ikiwemo watumishi wote kutumia vema mifumo iliyopo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ikiwa ni pamoja na mfumo wa kielektroniki wa kuratibu na kusimamia mashauri Mahakamani (e-CMS) kuingia katika barua pepe zao za Ofisi mara kwa mara, matumizi sahihi ya mfumo wa ofisi mtandao (e-office), kutodhamini watu wasio wafahamu kwa undani na mengine mengi.
Aidha, katika kikao hicho taarifa mbalimbali za utendaji kazi wa Mahakama zote zilizoko katika Kanda ya Musoma ziliwasilishwa na kupitia taarifa hizo kamati mbalimbali ziliundwa na mikakati kadhaa ya kuboresha utendaji kazi ilipangwa.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Mtulya (aliyesimama) akifungua kikao cha Menejimenti ya Kanda ya Musoma kilichofanyika Tarime hivi karibuni. Meza Kuu ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Musoma Mhe. Salome Mshasha (wa pili kushoto), Mhe. Monica Ndyekobora (wa kwanza kushoto), Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma Mhe. Erick Marley (wa kwanza kulia) na Mtendaji wa Mahakama Kuu Musoma Bw. Leonard Maufi (wa pili kulia).
Wajumbe wa kikao cha Menejimenti Kanda ya Musoma wakifuatilia kwa makini na kufurahia picha katika wasilisho la taarifa ya utendaji kazi wa Mahakama ya Wilaya Tarime, iliyowasilishwa na Afisa Tawala wa Mahakama hiyo Bw. Herman Lomasi (aliyesimama).
Wajumbe wa kikao cha Menejimenti Kanda ya Musoma wakifuatilia kwa makini taarifa inayowasilishwa na Afisa Mkaguzi wa Ndani wa Kanda ya Musoma Bw. Andala Nyakuwa (aliyesimama).
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma Mhe. Erick Marley (aliyesimama) akifafanua jambo wakati wa kikao cha Menejimenti ya Kanda ya Musoma.
Mtendaji wa Mahakama Kuu Musoma Bw. Leonard Maufi (aliyesimama) akifafanua jambo wakati wa kikao cha Menejimenti ya Kanda ya Musoma.
(Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni