Jumatatu, 22 Aprili 2024

TUTUMIE KWA USAHIHI MIFUMO ILIYOPO KWA USTAWI WA MAHAKAMA

 

Na. Francisca Swai, Mahakama – Musoma.

Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma wamesisistizwa kutumia vema mifumo iliyopo ili kuimarisha ustawi wa Mahakama ya Tanzania. 

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Kumbukumbu na Nyaraka wa Mahakama ya Tanzania Bw. Malimo Manyambula alipofanya kikao kazi na watumishi wa Mahakama Kuu Musoma, Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma na Mahakama ya Wilaya Musoma  mwishoni mwa wiki iliyopita katika ukumbi wa mikutano ulioko Mahakama Kuu Musoma.

Bw. Manyambula ameyasema hayo wakati walipokuwa wakipitia kwa pamoja hali ya matumizi ya mfumo wa Ofisi Mtandao (e- Office) kwa Kanda ya Musoma na kutoa mafunzo elekezi juu ya matumizi sahihi ya mfumo huo na namna mfumo unavyosaidia utunzaji wa kumbukumbu mbalimbali za kiofisi.

Alisema pamoja na mfumo kusaidia utunzaji wa kumbukumbu sahihi faida nyingine za mfumo ni kurahisisha ushughulikiaji wa masuala ya kiofisi kwa wakati, kuokoa muda, kupunguza gharama za uendeshaji ikiwemo manunuzi ya karatasi, wino, stempu, bahasha, madokezo, vikiwemo vifaa vingine vilivyokuwa vikitumika kwa wingi hapo awali kabla ya kuanza matumizi ya mfumo huo.

Katika mafunzo hayo elekezi yaliyofanywa na Mkurugenzi huyo pamoja na Afisa Kumbukumbu Bw. Kelvin Mayala watumishi hao wa Kanda ya Musoma walipata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika matumizi ya mfumo huo na kukubaliana kwa pamoja kuutumia kwa usahihi kama inavyotakiwa.

Mkurugenzi wa Kumbukumbu na Nyaraka wa Mahakama ya Tanzania Bw. Malimo Manyambula akisisitiza jambo wakati wa tathmini ya utumiaji wa mfumo wa ofisi mtandao na mafunzo elekezi yaliyofanyika Mahakama Kuu Musoma.

Watumishi wa Mahakama Kuu Musoma, Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Musoma wakifuatilia kwa makini maelekezo yanayotolewa kuhusu mfumo wa Ofisi mtandao na Afisa Kumbukumbu Bw. Kelvin Mayala (aliyenyoosha mkono mbele kushoto).

Mtendaji wa Mahakama Kuu Musoma bw. Leonard Maufi (katikati) akifungua akaunti yake ya Ofisi mtandao kwa ajili ya tathmini ya matumizi ya mfumo huo.

Mtumishi wa Mahakama Kuu Musoma Bw. Thobias Edward aliyesimama akiuliza swali wakati wa tathmini ya utumiaji wa mfumo wa ofisi mtandao na mafunzo elekezi yaliyofanyika Mahakama Kuu Musoma.


Afisa Kumbukumbu Bw. Kelvin Mayala (wa kwanza kushoto) akitoa maelezo mbalimbali juu ya matumizi ya mfumo wa Ofisi Mtandao kwa watumishi wa Mahakama Kuu Musoma, Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Musoma (hawako pichani).

Mkurugenzi wa Kumbukumbu na Nyaraka wa Mahakama ya Tanzania Bw. Malimo Manyambula (aliyesimama) akimsikiliza kwa makini Bw. Thobias Edward (wa pili kulia) akielezea  changamoto wanazokutana nazo katika matumizi ya ofisi mtandao.

(Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo-Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni