Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma
Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani amewataka Naibu Wasajili wa Mahakama kutofanya kazi kwa hofu kwani kufanya hivyo ni kuendana na kinyume cha kiapo chao.
Mhe. Siyani ameyasema hayo leo tarehe 22 Aprili, 2024 wakati wa hafla fupi ya kumuapisha Mhe. Projestus Kahyoza kuwa Naibu Msajili Mwandamizi Mahakama Kuu ya Tanzania iliyofanyika ofisini kwake Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma.
“Nyie mnafahamu eneo kubwa ambalo limekuwa likiwakwamisha watu ni hofu tu, sasa mtu ambaye anashindwa kutimiza majukumu yake kwa sababu ya hofu amekiuka kiapo chake,” amesema Jaji Kiongozi.
Ameongeza kuwa, hofu anayoizungumzia ni ile hali ya mtu kushindwa kutekeleza jukumu fulani kwa kuhofia kupata malalamiko yatakayompotezea sifa ya kupata nafasi fulani.
“Kama watu wataendelea kufanya kazi kwa hofu tunaweza kujikuta tunadhani tuna Naibu Wasajili kumbe walishaacha kazi siku nyingi wanaendelea tu kuja kazini na sisi tunawaona kumbe wameshaacha kazi siku kwa sababu wamekiuka kiapo chao, hivyo tafuteni namna ya kufanya ya kuhakikisha kuwa wenzetu hawa watimize majukumu yao bila hofu endapo tu wanazingatia sheria hakuna mtu atakayewaingilia,” ameeleza Mhe. Siyani.
Katika mazungumzo yake wakati wa hafla hiyo, Jaji Kiongozi amemtaka Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania aliyemuapisha kushirikiana na Viongozi wake akiwemo Msajili Mkuu na Msajili Mahakama Kuu na wengine ili kujua mahitaji ya Taasisi ya muda mrefu na mfupi pamoja na kupanga mipango stahiki ya kuhakikisha kuwa Mahakama inazidi kusonga mbele.
“Lazima tujue Taasisi inahitaji nini kwa wakati huu na tujue mipango tuliyojiwekea kwahiyo tunamtegemea Naibu Msajili Mwandamizi na wengine kujua mahitaji ya Taasisi kwa wakati. Kwa sasa mahitaji yetu ni nini, yapo mengi lakini nini kipo mbele yetu, ni safari kuelekea matumizi kamili ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwenye kazi zetu za kila siku,” amesisitiza Jaji Kiongozi.
Amesema, suala la matumizi ya TEHAMA halina mjadala, hivyo hatarajii Naibu Msajili Mwandamizi pamoja na Viongozi wengine kurudisha nyuma jitihada za kuelekea katika hatua hiyo bali kukabiliana na changamoto za mifumo zinazojitokeza na hatimaye kufikia ndoto hiyo.
Kadhalika, Mhe. Siyani amekumbusha kuhusu suala la kuzingatia maadili na uadilifu katika kazi huku akisema kuwa, Mtumishi anapokosa uadilifu anavunja imani ya wananchi kwa Mahakama.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Msajili Mkuu, Mahakama ya
Tanzania, Mhe. Eva Nkya, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa,
Mtendaji Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha na baadhi ya Naibu
Wasajili na Watendaji wa Mahakama Kuu Masjala Kuu.
Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher
Mohamed Siyani (kushoto) akimuapisha Mhe. Projestus Kahyoza kuwa Naibu Msajili
Mwandamizi-Mahakama Kuu ya Tanzania (kulia). Hafla ya uapisho imefanyika leo
tarehe 22 Aprili, 2024 katika jengo la Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.
Katikati ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa.
Sehemu ya Viongozi wa Mahakama waliohudhuria wakishuhudia uapisho wa Naibu Msajili Mwandamizi-Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Projestus Kahyoza.
Naibu Msajili Mwandamizi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Projestus Kahyoza akisaini hati ya kiapo mara baada ya kuapa kushika wadhifa huo.
Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher
Mohamed Siyani akisaini hati ya kiapo ya Mhe. Projestus Kahyoza aliyeapishwa kuwa
Naibu Msajili Mwandamizi Mahakama Kuu ya Tanzania.
Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani akimpongeza Mhe. Projestus Kahyoza baada ya kuapishwa kuwa Naibu Msajili Mwandamizi Mahakama Kuu ya Tanzania.
Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya (wa pili kushoto), wa kwanza kushoto ni Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa, wa kwanza kulia ni Mtendaji Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha na wa pili kulia ni Naibu Msajili Mwandamizi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Projestus Kahyoza aliyeapishwa leo kushika nafasi hiyo.
Jaji Kiongozi Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya (wa tatu kushoto) pamoja na Naibu Wasajili wengine walioshiriki katika hafla ya uapisho wa Naibu Msajili Mwandamizi, Mhe. Projestus Kahyoza (wa tatu kulia)
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni