Jumatano, 17 Aprili 2024

KLINIKI ZA SHERIA KUKUZA UPATIKANAJI HAKI – JAJI MKUU

Na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma

Rai imetolewa kwa Vyuo Vikuu nchini vinavyotoa Elimu ya Sheria kupitia Shule Kuu za Sheria katika Vyuo hivyo kuimarisha Kliniki za Sheria ili kukuza na kupanua wigo wa upatikanaji wa haki kwa Watanzania.


Rai hiyo ilitolewa jana tarehe 15 Aprili, 2024 na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma katika hafla ya Siku ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Shule Kuu ya Sheria iliyofanyika katika ukumbi wa ‘CIVE Auditorium’ uliopo chuoni hapo.

 

“Mwananchi akifahamu mipaka ya sheria itamsaidia sana, msaada wa sheria ni huduma yenye umuhimu mkubwa sana, hivyo tutoe elimu pana ya kumuwezesha mwananchi wa kawaida kupata haki zake hata katika Ofisi za Umma,” alisema Jaji Mkuu.

 

Alisema, uwepo wa huduma za msaada wa kisheria kutoka kwa wadau mbalimbali kama Kliniki ya Msaada wa Kisheria unatoa fursa kwa wanachi wa kipato cha chini ambao wameshindwa kumudu gharama za kumuajiri Wakili, kupata haki zao na hivyo kuongeza utulivu na amani katika jamii na Nchi kwa ujumla. 

 

Mhe. Prof. Juma alisema kwamba, Kliniki za Sheria zina faida kubwa kwa wanafunzi wanaotoa huduma kwakuwa zinawapa nafasi ya kujifunza kusaili ili wapate undani wa tatizo; inawajengea uwezo wa kuchambua na kuacha yasiyo na maana; wanaona namna Taasisi za Kisheria zinavyofanya kazi; zinawawezesha kuwaelewa wananchi wanavyotafsiri dhana na maana ya wanavyoelewa haki, inawasaidia kujenga mahusiano ya kitaaluma ambayo itawasaidia baadaye watakapojiunga na soko la ajira. 


Alisisitiza kuhusu umuhimu wa elimu ya sheria kwa umma katika maeneo yenye shida hapa nchini ambayo ni pamoja na Elimu ya uraia (civic education), Ukatiba (Constitutionalism)Uwajibikaji (accountability)Unyanyasaji/Ukatili wa kijinsia (gender-based violence).

Maeneo mengine ni Haki za mtoto na binadamu kwa ujumlaHaki ardhiMigogoro ya ardhi, Haki na ulinzi wa mlajiMirathi, kuepuka matumizi mabaya ya mapingamizi mahakamani na matumizi ya sababu za kiufundi kuchelewesha haki, umuhimu wa kutumia njia za Usuluhishi kutatua migogoro nje ya Mahakama, kusimamia Maadili ya Mawakili na Watumishi wa Umma na mengine.

 

Aidha, Mhe. Prof. Juma aliwakumbusha Wanafunzi wa Taaluma ya Sheria, kuwa, Karne hii ya 21 ina mabadiliko makubwa na ushindani wa kupindukia, hivyo Elimu ya Sheria (Legal Education), Taaluma ya Sheria (Legal Profession), Upatikanaji Haki mahakamani (Access to Justice in courts) na hata Kliniki za Sheria ni lazima pia zibadilike ili ziende sambamba na ushindani wa karne hiyo

 

Ndio maana, nimewaomba waandaaji wa Siku hii ya Sheria, wamruhusu Mkuu wa Idara ya TEHAMA ya Mahakama ya Tanzania, atoe wasilisho fupi, kuhusu Matumizi makubwa ya Teknolojia, ikiwemo matumizi ya Akili Mnemba (Artificial Intelligencekatika utoaji haki katika Karne ya 21,” alisema Jaji Mkuu

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Prof. Lugano Kusiluka alimshukuru Jaji Mkuu kwa kushiriki katika Siku hiyo huku akisema kuwa, Shule Kuu ya Sheria ilianzishwa mwaka 2009 kama Idara ikiwa na programu moja ya shahada ya awali ya Sheria. 

“Leo ikiwa ni takribani miaka kumi na tano tangu kuanzishwa kwake, Shule hii inatoa shahada ya awali ya sheria, shahada ya umahiri katika sheria za mashirika (Masters of Laws in Coorporate Law), Shahada  ya umahiri katika sheria za haki ya binadamu (Masters of Laws in Human Rights law) na shahada ya uzamivu katika sheria,” alieleza Prof. Kusiluka.

Aidha, Mkuu huyo wa Chuo alifikisha ombi kwa Jaji Mkuu juu ya Shule ya Sheria Tanzania (LST) kuanzisha matawi nchi nzima ili kuwawezesha wanafunzi wasio na uwezo kusoma wakiwa katika maeneo/Mikoa yao.


Kadhalika, Mkuu huyo wa Chuo aliomba pia kupatikana kwa ukumbi mkubwa zaidi wa studio ya kuendesha Mahakama kwa vitendo.


Katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Bw. Kalege Enock alitoa mada kuhusu Safari ya Mahakama ya Tanzania kuelekea Mahakama inayotoa huduma kwa njia za Kidijitali (Judiciary of Tanzania Digital Transformation Journey).  

 

Katika wasilisho lake, Bw. Kalege alibainisha kuwa, Mahakama ya Tanzania imefanikiwa kwenye matumizi ya TEHAMA kutokana na mambo makuu matatu (3) nayo ni pamoja na Uongozi imara na thabiti ambao umetoa ushirikiano katika eneo hilo, Mpango Mkakati wa Mahakama na Utoaji huduma kwa wananchi.


Maadhimisho hayo ni ya tatu (3) tangu kuanzishwa kwa Siku ya Sheria katika Chuo hicho. Siku ya Sheria ya Chuo hicho kwa mwaka huu imebebwa na Kaulimbiu isemayo; Uimarishaji wa Kliniki za Sheria Vyuo Vikuu katika kukuza na kupanua wigo wa upatikanaji haki Tanzania.



Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na sehemu ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (hawapo katika picha) wakati wa hafla ya Siku ya Sheria ya Chuo hicho iliyofanyika tarehe 15 Aprili, 2024 chuoni humo.

Sehemu ya wanafunzi wanaosoma Kozi ya Sheria na wengine, Watumishi wa Chuo Kikuu cha Dodoma pamoja na baadhi ya Wageni waalikwa wakimsikiliza Mgeni Rasmi Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika picha) alipokuwa akitoa hotuba yake wakati wa hafla ya Siku ya Sheria ya Chuo hicho iliyofanyika tarehe 15 Aprili, 2024.

 

Makamu Mkuu wa Chuo cha Dodoma, Prof. Lugano Kusiluka (kushoto) akimkabidhi Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma zawadi ya kikombe wakati alipowasili chuoni hapo tarehe 15 Aprili, 2024 kwa ajili ya kushiriki katika hafla ya Siku ya Sheria ya Chuo hicho kama Mgeni Rasmi.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa tatu kushoto) katika picha ya pamoja na mwenyeji wake (kushoto kwake) wakati alipowasili Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa ajili ya kushiriki katika hafla ya Siku ya Sheria ya Chuo hicho iliyofanyika tarehe 15 Aprili, 2024.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa amesimama nje ya Mahakama ya Maigizo ya Chuo Kikuu cha Dodoma wakati alipowasili katika Chuo hicho kushiriki katika hafla ya Siku ya Sheria ya Chuo hicho iliyofanyika tarehe 15 Aprili, 2024.

Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Kitengo cha Maktaba, Mhe. Kifungu Mrisho akizungumza jambo wakati wa hafla ya Siku ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dodoma iliyofanyika tarehe 15 Aprili, 2024.


Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Mahakama ya Tanzania, Bw. Kalege Enock akitoa mada kuhusu matumizi ya TEHAMA mahakamani kwa Watumishi na Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma waliohudhuria katika hafla ya Siku ya Sheria ya Chuo hicho iliyofanyika jana tarehe 15 Aprili, 2024.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Wanafunzi wanaosoma Kozi ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM). Wa tatu kulia ni Makamu Mkuu wa Chuo cha Dodoma, Prof. Lugano Kusiluka, wa pili kulia ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Masabo, wa tatu kushoto ni Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Mkanachi Khamis na Watumishi wengine wa Chuo hicho.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wadau wa hicho walioshiriki katika hafla ya Siku ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akipokea zawadi ya picha aliyochorewa na mmoja wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma.


(Picha na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni