Jumanne, 9 Aprili 2024

MAHAKAMA MBEYA YAPANGA MKAKATI WA ZERO MASHAURI MLUNDIKANO

Na Mwinga Mpoli – Mahakama, Mbeya

Menejimenti ya Mahakama Kanda ya Mbeya jana tarehe 08 Aprili, 2024 ilikutana mkoani Mbeya kwenye kikao cha robo mwaka ikiwa ni kwa ajili ya kufanya tathmini ya utendaji kazi na pia kujiwekea mikakati ya namna bora ya kuhakikisha uondoshaji wa mashauri ya mlundikano mahakamani.

Akizungumza katika kikao hicho kilicho fanyika katika ukumbi wa mikutano Mahakama Kuu Mbeya, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Mhe. Dunstan Ndunguru mara baada ya kupokea taarifa za mashauri pamoja na za kiutendaji aliwataka Mahakimu Wafawidhi wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha wanasimamia vyema vituo vyao kwa ufanisi mkubwa na kuhakikisha wanafanya kazi kwa nidhamu ya hali ya juu.

“Kwa kushirikiana pamoja tunaweza kuhakikisha tunaondoa mlundikano wa mashauri mahakamani na kuwasaidia wananchi kupata huduma ya haki kwa wakati bila kuchelewa na hivyo kutimiza lengo la Mahakama kwa asilimia 100...

Nawaomba mjitahidi kuwatembelea Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo na nimatumaini yangu kufikia Juni, 2024 hatutakuwa na mashauri ya mlundikano wala mashauri yanayokaribia kuwa ya mlundikano, tujitahidi kutotengeneza mashauri ya mfanano huo”, alisisitiza Jaji Ndunguru.

Kwa upande wake, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Bi. Mavis Miti alisisitiza utunzaji wa rasilimali za Mahakama ikiwa ni pamoja na Majengo, vifaa vya ofisi, magari ya ofisi kwani ndiyo sehemu ya nyezo zitakazo tumika kufikia lengo la kuondoa mlundikano wa mashauri mahakamani vilevile matumizi sahihi ya rasilimali hizo ni sehemu ya nidhamu ya kazi.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya Mhe. Dunstan Ndunguru akisisitiza jambo wakati wa kikao hicho cha menejimenti cha robo mwaka kilichofanyika jana tarehe 8 Aprili katika ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu Mbeya

Wajumbe wa Menejimenti Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya wakifuatilia kwa karibu taarifa zilizokuwa zikitolewa katika kikao kazi hicho.

Wajumbe wa Menejimenti Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya wakifuatilia kwa karibu taarifa zilizokuwa zikitolewa katika kikao kazi hicho.

Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu Mbeya Mhe. Aziza Temu akitoa ufafanuzi wa  taarifa ya mashauri kwa wajumbe wa kikao hicho.

Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya Bi. Mavis Miti akisoma taarifa ya utendajji kazi wakati wa kikao hicho.

(Habari Hii Imehaririwa na Innocent Kansha -Mahakama)


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni