Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam
Mahakama ya Tanzania imefanya marekebisho kadhaa katika Kanuni za Mahakama ya Rufani ili kurahisisha utoaji haki, kuimarisha utawala wa sheria na utoaji haki kwa haraka nchini.
Marekebisho hayo yanayoitwa, “Kanuni za Mahakama ya Rufani ya Tanzania (Marekebisho) ya Mwaka 2024 Tangazo la Serikali Na. 188” yaliyotolewa Machi 22, 2024 yanasisitiza juhudi madhubuti za kuleta ufanisi ndani ya mfumo wa Mahakama na kuimarisha usimamizi wa haki.
"Kwa kuzingatia kwa kina katika kurahisisha shughuli za mahakama, matumizi ya teknolojia na kufafanua utata wa kisheria, Kanuni hizi zinasimama kama mwanga wa maendeleo ya Tanzania katika kuzingatia ubora wa Mahakama," Katibu Mwenza wa Kamati ya Kanuni za Mahakama, Mhe. Kifungu Mrisho Kariho amesema katika taarifa yake aliyoitoa jijini Dar es Salaam leo tarehe 9 Aprili, 2024.
Mhe. Kariho, ambaye pia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu alitaja moja ya mambo muhimu ya marekebisho hayo kuwa ni Kanuni kutambua na kuruhusu rejea ya Maamuzi yanayochapishwa kwenye mfumo rasmi wa Sheria na Maamuzi (TanzLII) unaosimamiwa na Mahakama ya Tanzania.
"Hatua hii ina umuhimu mkubwa kwani inarahisisha ufikiaji rahisi wa Maamuzi na Sheria, na hivyo kuimarisha ukuaji wa sheria na namna ya kunukuu Sheria na Maamuzi hayo. Mahakama inadhihirisha dhamira ya kutumia teknolojia ili kutoa haki ipasavyo katika enzi ya kidijitali,” alisema kwenye taarifa hiyo.
Alisema marekebisho hayo ya Kanuni yanaashiria hatua kubwa katika safari ya kisheria ya Tanzania, na hivyo kuweka mazingira ya kuwepo kwa mfumo wa kimahakama unaozingatia uwajibikaji, uwazi na ufanisi zaidi unaokidhi mahitaji ya wananchi.
“Uongozi wa Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwenye mageuzi haya unastahili pongezi kwa kuongeza ufanisi na ufikiwaji rahisi kupitia uvumbuzi wa kiteknolojia. Marekebisho haya yanaashiria hatua kubwa kuelekea mfumo wa Mahakama unaofikika zaidi na mwepesi, unaothibitisha dhamira ya Tanzania katika utawala wa sheria na ubora wa Mahakama,” alisema.
Katibu mwenza huyo amebainisha baadhi ya marekebisho ambayo yamefanywa na Kamati inayoongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Rehema Mkuye kama kuondoa mahitaji ya malipo ya ada kwa ajili ya maombi ya msamaha.
Marekebisho mengine ni kutambua Maamuzi yaliyochapishwa kwenye mfumo rasmi unaosimamiwa na Mahakama ya Tanzania ili kurahisisha upatikanaji wa Sheria na Maamuzi na kurahisisha nukuu zake.
Marekebisho yaliyofanywa pia yanafafanua matumizi ya jina la Jaji kwa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani na kumpa Jaji mmoja mamlaka ya kusikiliza maombi ya awali ya upande mmoja na baina ya wadaawa katika naombi ya kusitisha utekelezaji wa hukumu kwa lengo la kuokoa muda, kupunguza mzigo wa kazi na kuharakisha umalizaji wa shauri husika.
Mhe. Kariho alitaja marekebisho mengine kuwa ni kupunguza gharama zisizo za lazima kwa kufungua mashauri, kutoa ufafanuzi wa taratibu za maombi ya masahihisho mbele ya jaji mmoja dhidi ya maamuzi ya Msajili na kuwapa mamlaka Wasajili kutoa amri kadhaa za awali kabla ya shauri kupangwa kusikilizwa.
Pia kuna kuhusisha sera ya Mahakama ya Tanzania ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia inayokusudia kupunguza wingi wa kumbukumbu za Mahakama na kuweka miongozo ya kuzuia matumizi mabaya ya taratibu za Mahakama katika maombi ya idhini kwa mara ya pili.
Marekebisho yaliyofanywa pia ni kuwapa Wasajili uwezo wa kushughulikia maombi ambayo hayajapingwa ya idhini ya kurekebisha hati na kutoa mamlaka kwa jaji mmoja kuamua maombi yanayopingwa ili kuharakisha umalizaji wa mashauri.
Marekebisho yanaondoa mahitaji ya malipo ya ada kwa ajili ya maombi ya msamaha, kutoa haki kwa pande zisizo na uwakilishi ya kudai gharama, kufafanua muda wa uwasilishaji wa maombi ya gharama na kuwapa Wasajili uwezo wa kuongeza muda na kurekebisha ada na mizani ya gharama.
Mhe. Kariho alisema kuwa marekebisho hayo yameleta ufafanuzi juu ya taratibu nyingi mbele ya jaji mmoja dhidi ya maamuzi ya Msajili bila kujali vikwazo vya kifedha.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni za Mahakama, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Rehema Mkuye.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni