Jumatano, 10 Aprili 2024

MAAFISA MAGEREZA WA DAR ES SALAAM NA PWANI WAPIGWA MSASA KUHUSU MFUMO WA e-CMS

Na Eunice Lugiana, Mahakama-Dar es Salaam

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika Kanda hiyo, Mhe. Anorld Kirekiano jana tarehe 09 Aprili, 2024 alifungua mafunzo ya Mfumo wa Ki-elektroniki wa Usimamizi wa Mashauri (e-CMS) kwa Maafisa Magereza kutoka Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.

Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Kinondoni, Mhe. Kirekiano alisema Mahakama ya Tanzania inatekeleza Mpango Mkakati ambao una nguzo tatu ambazo ni Utawala, Uwajibikaji na Usimamizi wa Rasilimali, Upatikanaji Haki kwa wakati  na Kurejesha Imani ya  Wananchi na Ushirikishwaji wa Wadau.

“Katika kutekeleza hayo Mahakama imeweka mifumo mbalimbali ambayo inasaidia kutekeleza hizo nguzo tatu moja ya maeneo ambayo Mahakama imejitanabaisha sana ni kuimarisha matumizi ya TEHAMA kwa ajili ya kusaidia upatikanaji haki kwa haraka na kwa nafuu lakini pia kuweka mifumo ambayo itapunguza gharama katika kutoa haki kwa wananchi na kwa yule anayetaka kuifikia Mahakama aweze kusaidika,” alisema Jaji Kirekiano.

Aidha, Mhe. Kirekiano alisema kuwa, Mfumo wa kusajili na kusilikiza mashauri kwa njia ya mtandao ambao unatumika ni moja ya maeneo ambayo yamefanyika kwa ajili ya kuhakikisha kwamba haki inapatikana kwa unafuu na kwa wakati.

“Nashukuru kumuona mwenzetu kutoka Mafia ambapo kwa hali ilivyo ingekuwa  kwamba lazima kusafiri kutoka Mafia kuleta nyaraka za rufaa lakini kwa kuwepo kwa mifumo  hii ya TEHAMA itasaidia  kurahisisha kwa maana ya kupunguza gharama lakini pia ule muda ambao ungetumika kwa mwananchi ambaye kwa muktadha wa nyie washiriki tunamzungumzia mfungwa aliye Magereza kwa ajili ya rufaa yake.” Alieleza Mhe. Kirekiano.

Alibainisha kuhusu chimbuko la mafunzo hayo kuwa ni, maboresho ambayo Mahakama inaendelea nayo lakini pia, yametokana na ziara ya Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi alipotembelea Gereza la Ubena Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani ambapo aligundua changamoto ya upatikanaji haki na hivyo akaona ili kuwa na jibu la pamoja ni vema waandae mafunzo hayo kwa Maafisa wa Magereza.

Mafunzo hayo yameratibiwa na Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Sundi Fimbo na kuwezeshwa na Afisa TEHAMA wa Kanda hiyo, Bi. Elisia Meena na Delfina Mwakyusa kutoka Kituo Jumuishi Kinondoni (IJC). 

Yamehudhuriwa na Maafisa kutoka Magereza ya Keko, Segerea na Ukonga, Mkoa wa Dar es Salaam na Mkuza, Kibiti, Ubena, Kigongoni, Utete na Mafia mkoani Pwani. 


Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam ambaye pia Mwenyekiti wa Kamati ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Mhe.Anorld Kirekiano (katikati) akifungua Mafunzo ya Maafisa Magereza. Kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda Ya Dar es Salaam, Mhe. Sundi Fimbo, kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni, Mhe.  Isihaka Kuppa.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati ya TEHAMA Kanda hiyo, Mhe. Anorld Kirekiano akijiandaa kuzungumza na washiriki wa Mafunzo ya Ki-elektroniki wa Usimamizi wa Mashauri (e-CMS) ambao ni Maafisa wa Magereza kutoka Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mwenyekiti wa Kamati ya TEHAMA akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo.

Afisa TEHAMA kutoka Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Kinondoni, Bi. Delfina Mwakyusa akisikiliza wwali kutoka kwa Mshiriki wa Mafunzo hayo.

Afisa TEHAMA Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Bi. Elisia Meela akitoa mada kwa washiriki-Maafisa Magereza walioshiriki katika mafunzo ya Mfumo wa Ki-elektroniki wa Usimamizi wa Mashauri (e-CMS).

(Habari Hii Imehaririwa na Mary Charles Gwera -Mahakama, Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni