Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameongoza kikao cha Tume ya Utumishi wa Mahakama kilichojadili na kufanya Uamuzi juu ya masuala mbalimbali yanayohusu Uendeshaji wa Mahakama na Tume hiyo.
”Wajumbe wa
Kikao hiki walipata wasaa wa kujadili taarifa za utekelezaji wa bajeti za Tume
ya Utumishi wa Mahakama pamoja na Mahakama ya Tanzania kwa kipindi cha Julai
2023 hadi Machi, 2024’’alisema Mtendaji Mkuu na Katibu wa Tume.
Akifafanua
kuhusu Taarifa hizo, Prof. Ole Gabriel alisema, Tume kwa upande wake imeendelea
na mikakati ya kuimarisha utendaji wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama za
Mikoa na Wilaya pamoja na kuandaa Mwongozo na Kanuni za Uendeshaji wa Kamati
hizo.
”Kuhusu maendeleo ya TEHAMA mahakamani, hadi kufikia Machi, 2024 Mahakama tayari imeanzisha Mifumo mbalimbali ya Kielektroniki ukiwemo ule wa wa Unukuzi na Tafsiri kwenye Mahakama 11 nchini pamoja na kuifanyia maboresho mifumo iliyopo”, alisema.
Alibainisha kuwa Mahakama ya Tanzania kwa kutumia
Akili Mnemba (Artifial Intelligence) na mifumo mingine ya kisasa ya TEHAMA
imekuwa kivutio kwa Mahakama duniani na sasa Viongozi wengi wa Mahakama za
Afrika na Nje ya Afrika wanatembelea Mahakama ya Tanzania. Hii imewezesha pia utalii
wa Mahakama (Judicial Tourism) na hivyo kuchangia pato la Taifa.
Kuhusu
usikilizwaji wa mashauri mahakamani, alisema Tume ilipokea taarifa hiyo ambapo
idadi ya mashauri ya mlundikano imeendelea kupungua kutoka asilimia sita mwaka
2021 na kufikia asilimia 3 Desemba mwaka 2023.
Alisema
Serikali imeendelea kutoa ushirikiano mkubwa katika kuiwezesha Mahakama
kutekeleza majukumu yake pamoja na maboresho katika miundombinu yake.
Tume ya
Utumishi wa Mahakama iliyoundwa na ibara ya 112(1) ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 katika kutekeleza majukumu yake iliyopewa na
Sheria, ilikutana katika kikao chake cha kawaida kwa ajili ya kujadili na
kufanya uamuzi kuhusu masuala mbalimbali.
Pamoja na Mwenyekiti wa kikao hicho,
wajumbe wengine waliohudhuria ni Mhe. Dkt. Gerald Ndika (Jaji wa Mahakama ya
Rufani), Mhe. Mustapher Siyani (Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania),
Jaji Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi (Mwanasheria Mkuu wa Serikali), Bw. Bahame Tom
Nyanduga (Wakili) na Bi. Dosca Mutabuzi (Wakili).
Wengine waliohudhuria ni Prof. Elisante
Ole Gabriel (Katibu wa Tume), Bi. Enziel Mtei (Naibu Katibu wa Tume-Ajira) na
Bi. Alesia Mbuya (Naibu Katibu wa Tume-Maadili na Nidhamu). Aidha Mhe. Eva Nkya
(Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania) alialikwa kuhudhuria kikao hicho.
Jaji Mkuu na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa
Mahakama Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyesimama) akitoa mada katika Kikao cha Tume kilichofanyika jana tarehe 09 April, 2024 jijini Dar es salaam. Katikati ni Jaji Mkuu na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Prof. Ibrahim Hamis Juma pamoja na wajumbe wangine.
Jaji Mkuu na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa
Mahakama Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) pamoja na wajumbe wa kikao cha
Tume ya Utumishi wa Mahakama wakimsikiliza Katibu wa Tume hiyo Prof. Elisante
Ole Gabriel (hayupo pichani) akitoa mada katika Kikao hicho kilichofanyika jana tarehe 09 April, 2024 jijini Dar es salaam.
Jaji wa Mahakama ya Rufani na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Dkt. Gerald Ndika (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamishna wa Tume Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi (kushoto) na Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya mara baada ya kikao cha Tume.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni