Jumanne, 23 Aprili 2024

MTENDAJI MAHAKAMA SONGEA AWAKUMBUSHA WATUMISHI KUZINGATIA KANUNI, MIONGOZO, TARATIBU ZA KIUTUMISHI

Na Hasani Haufi – Mahakama, Songea.

Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Bw. Epaphras Tenganamba amewakumbusha watumishi wa Mahakama Songea kuzingatia miongozo na taratibu mbalimbali za kiutumishi ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na tija.

Bw. Tenganamba aliyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa Mahakama Kuu Songea hivi karibuni katika ukumbi wa wazi.

“Tukiwa kama watumishi wa umma, tunapaswa kuzingatia miongozi na taratibu mbalimbali za kiutumishi ili kupata matokeo yenye tija na mazuri wakati wa kutekeleza majukumu,” alisema.

Mtendaji huyo aliwasisitiza kujenga familia moja kama watumishi wa Mahakama ya Tanzania badala ya kufanya kazi kwa makundi na vinyongo, kwani hakuna aliyeajiwa kwa kupitia mtu fulani.

“Tunavyozijenga familia zetu nyumbani na kuishi nazo kwa wema, basi vivyo hivyo tunatakiwa tujenge familia tukiwa kazini na kuishi kwa wema. Tusiwe na makundi kwani hujuwi nani atakuja kukusaidia maishani, hata kama umepata ajira hujui la mbele, kwakuwa tupo taasisi moja basi sisi ni familia,” alisema.

Sambamba na hilo, Bw. Tengamba aliwasisitiza watumishi hao kutimiza majukumu yake ya kila siku kwa kuzingatia muda, mipaka pamoja na kuheshimiana katika mazingira ya kazi ili kuepuka kuwajibishwa.

“Ukijitambua kuwa wewe ni mtumishi wa umma ni lazima ujuwe umeajiriwa kwasababu ipi, kwa maana kutekeleza majukumu ya kila siku. Lazima utambue majukumu yako,” alisema.

Mtendaji huyo aliwahimiza watumishi kujiendeleza kielimu kwa ajili ya kuongeza ujuzi katika nyanja mbalimbali ili kwenda na kasi ya mabadiliko yanayoendelea katika Mahakama ya Tanzania na Ulimwenguni kwa ujumla.

“Pamoja na kutekeleza majukumu ya kila siku kwa kuzingatia miongozo na taratibu mbalimbali za kitumishi, tunapaswa kuongeza ujuzi kwa kwenda shule kwani itafikia pahala kama huna ujuzi wa kitu fulani hautahitajika katika ,” Bw. Tengamba alisema.


Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Songea, Bw. Epaphras Tengamba, akizungumza na watumishi wa Mahakama Kuu Songea.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)


 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni