Ijumaa, 26 Aprili 2024

WANAFUNZI WA SHULE YA MSINGI BANGWE WAVUTIWA KUSOMA SHERIA

Na Aidan Robert-Mahakama, Kigoma

 Wanafunzi wa Shule ya Msingi Bangwe wamepatiwa elimu kuhusu Sheria na huduma zitolewazo na Mahakama, ambapo wameonesha bashasha isiyo na kifani wakitamani kufahamu sifa za kuwa Hakimu au Jaji.

 

Akitoa elimu ya Mahakama kwa wanafunzi hao waliotembelea Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma leo tarehe 25 Aprili, 2024 Msadizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Elimu kwa Umma, Mhe. Victor Kagina amewaeleza wanafunzi hao kuwa, ili mtu awe Hakimu takwa la msingi ni masomo ya Sheria kwa kiwango cha Shahada.

 

 Amewasihi kuwa, wasome kwa bidii huku kipaumbele chao kiwe nidhamu na utii ili kufikia ndoto zao ili nao waje kuwa Majaji na Mahakimu wa siku zijazo.

 

Aidha, wanafunzi hao waliomba kufahamu kuwa Jaji au Hakimu wanapewa na nani mamlaka ya kutoa hukumu kwa wanadamu wenzao. Akijibu swali hilo, Mhe. Kagina amewajuza Wanafunzi hao kwamba, Majaji na Mahakimu hupata mamlaka ya kutoa hukumu kutoka kwenye Katiba na Sheria, Taratibu na Kanuni mbalimbali za Nchi.

 

Kadhalika, wanafunzi hao walihitaji kufahamishwa juu ya muundo wa Mahakama, ambapo Mhe. Kagina amewafundisha kuwa, kuna Mahakama ya Mwanzo, Mahakama ya Wilaya, Mahakama ya  Hakimu Mkazi, Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani ambapo ameongeza kuwa, Mahakama ya Rufani ndio Mahakama ya juu katika utoaji wa haki nchini Tanzania.

 

 “Shughuli ya msingi ya Mahakama ni pamoja na kusikiliza mashauri na kutoa uamuzi wa haki kwa wakati bila upendeleo kwa mtu yeyote,” amesisitiza Mhe. Kagina.

 

Mmoja kati ya wanafunzi hao alihitaji kufahamu, ni watu gani wanaostahili kupata huduma za kimahakama, ambapo Mhe. Kagina aliwajulisha kuwa, ni mtu yeyote mwenye uhitaji wa huduma hizo kwa matakwa yake ama kwa matakwa ya Jamhuri, huku akitoa mifano ya wanaokuja mahakamani kwa mashauri ya madai na wale wanaoletwa Mahakamani kwa matakwa ya kisheria hususani kwa mashauri ya jinai. 

 

Na kwa upande wake Mwalimu wa shule hiyo, Bw.Alexander Toyi, ameushukuru Uongozi wa Mahakama Kuu Kigoma  kupokea maombi ya kutembelea Mahakama hiyo, kwakuwa wamejifunza na kufahamu huduma zitolewazo na Mahakama.

 

 Vilevile amemshukuru Mkufunzi wa wanafunzi hao, Mhe Victor Kagina, kwa ubora na msingi mkubwa wa elimu aliyoitoa kwa wanafunzi hao kuwa itakuwa chachu kwa maendeleo ya masomo yao shuleni.

 

Msadizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kigoma ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Elimu kwa Umma, Mhe. Victor Kagina akifafanua jambo kwa wanafunzi wa darasa la saba wa shule ya msingi Bangwe-Kigoma waliofika kutembea Mahakama Kuu Kigoma leo tarehe 25 Aprili, 2024 kwa lengo la kujifunza.


 

Picha ya wanafunzi na mwalimu wao wakiwa wameketi katika ukumbi wa Mahakama ya wazi uliopo kwenye jengo la Mahakama Kuu Kigoma wakimsikiliza kwa makini Mhe. Victor Kagina, alipokuwa akifundisha.

 

Picha ya Mwanafunzi, Dorcas Alfonce (kulia) akimuuliza swali Mhe. Victor Kagina, ambaye alikuwa akitoa majibu hapo kwa hapo kwa wanafunzi hao wa darasa la saba katika shule ya msingi Bangwe-Kigoma.


 

Picha ya pamoja ya Msaidizi wa Sheria wa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kigoma ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Elimu kwa Umma, Mhe. Victor Kagina (katikati) na kushoto ni Mwalimu wa Darasa la Saba katika Shule ya Msingi Bangwe, Bw. Alexander Toyi, na kulia ni Mkutubi Msaidizi wa Mahakama Kuu Kigoma, Bi. Magdalena Ndumbili na nyuma yao ni wanafunzi wa Darasa la Saba kutoka Shule ya Msingi Bangwe Kigoma.

 

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama-Dodoma)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni