Ijumaa, 26 Aprili 2024

JAJI MKUU ASHIRIKI MAADHIMISHO MIAKA 60 YA MUUNGANO TANZANIA

Na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 26 Aprili, 2024 ameungana na Watanzania nchini kote kuadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mhe. Prof. Juma aliwasili katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam mapema asubuhi kuungana na Viongozi wengine wa Kitaifa na Kimataifa kwenye maadhimisho hayo ambayo Mgeni Rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

Sehemu ya Viongozi wengine wa Kitaifa waliohudhuria maadhimisho hayo ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango.

Wengine ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Mhe. Kassim Majaliwa KassimSpika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Mhe. Dkt. Tulia Ackson, Mawaziri wa Wizara mbalimbali, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa na Viongozi wengine.

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa pia na Marais na wawakilishi kutoka Nchi mbalimbali za Bara la Afrika, ikiwemo kutoka Kenya, Uganda, Comoro, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Zimbabwe, Burundi, Zambia, Somaria, Namibia pamoja na Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.

Gwaride maalum lililoandaliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Polisi na Magereza limepamba maadhimisho hayo, licha ya mvua kubwa iliyokuwa inanyesha.Rais Samia amekagua gwaride hilo na kupokea salamu za utii.

Wakati wa maadhimisho hayo, gwaride hilo lilipita mbele ya Rais na wageni mbalimbali kwa mwendo wa pole na baadaye mwendo wa haraka na kushangiliwa na wananchi waliokuwa wamefurika kwa wingi katika Uwanja wa Uhuru.

Katika miaka 60 ya uhuruTanzania imefanikiwa kupiga hatua katika maendeleo katika nyanja mbalimbali, ikiwemo kuulinda uhuru na mipaka, kudumisha amani; kuimiraisha uchumi  na demokrasia na kuboresha huduma za kujamii.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliundwa tarehe 26 Aprili, 1964, ikiwa ni Muungano wa Mataifa mawili huru ya Jamhuri yaTanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambayo yaliingia mkataba wa Muungano mnamo mwaka 1964 na kuanzishwa Dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mkataba wa Muungano ulitiwa saini na aliyekuwa Rais wa Tanganyika, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, tarehe 22 Aprili, 1964 huko Zanzibar.



Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia aliyeangalia pembeni) akiwa na Viongozi wengine wa Serikali wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya muungano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wengine ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson (katikati) na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Dotto Biteko. Picha chini ni sehemu ya Viongozi wengine waliohudhuria maadhimisho hayo.


Sehemu ya Wananchi (juu na chini) waliofurika kwenye Uwanja wa Uhuru kwenye maadhimisho hayo.


Gwaride maalum lililoandaliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Polisi na Magereza likiingia katika Uwanja wa Uhuru kwenye maadhimisho hayo.

Kikosi ya Bendera katika gwaride maalum lililoandaliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Polisi na Magereza kikitoa heshima mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan (hayupo kwenye picha) wakati wa maadhimisho hayo.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (kushoto) na Sheikh Abeid Amani Karume (kulia) wakibadilishana Hati za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar tarehe 27 Aprili, 1964.

 



 

 







 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni