Jumamosi, 27 Aprili 2024

WATUMISHI WAWILI WALIOKOMA UTUMISHI WAAGWA MAHAKAMA KUU SONGEA

Na Hasani Haufi- Mahakama, Songea.

Watumishi wawili wa Mahakama Kuu Songea, ambao ni Bi. Baina Chowo, Msaidizi wa Ofisi pamoja na Maurus Kapinga, Mlinzi ambao ajira yao imekoma kwa kustaafu kwa umri Machi 2024, wameagwa na watumishi wa Mahakama Kuu Songea.

Hafla hiyo iliyofanyika tarehe 25 Aprili, 2024, kwenye ukumbi wa wazi Mahakama Kuu Songea, iliongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha. 

Viongozi wengine waliokuwepo ni Jaji wa Mahakama Kuu Songea, Mhe. Upendo Madeha, Naibu Msajili wa Mahakama Kanda ya Songea, Mhe. Elizabeth Nyembele na Mtendaji wa Mahakama Kanda ya Songea Bw. Epaphras Tenganamba.

Akizungumza katika hafla hiyo, Jaji Karayemaha aliwapongeza wastaafu hao kwa kuwa na subra na kufanya kazi na vizazi mbalimbali hadi kufikia umri wa kukoma utumishi wao bila kuingia katika shida wala misukosuko na mwajiri.

“Ninachoweza kusema kwa niaba ya watumishi wote wa Mahakama Kuu Songea, kuwa nawapongeza sana kwa subra mliyokuwanayo, kwani bila ya kuwa na subra msingeweza kufanya kazi na vizazi mbalimbali,” alisema.

Jaji Mfawidhi aliwashukuru kwa muda wao wote waliotumikia Mhimili wa wa Mahakama ya Tanzania na Taifa kwa ujumla na kudumisha upendo kwa watumishi wengine bila kuangalia wadhifa wake.

“Niwashukuru sana kwa muda wenu wote mliojitoa kutumikia Taifa na Mhimili wa Mahakama ya Tanzania, najivunia kuona mmedumisha upendo kwa kila mtu,” alisema.

Aidha, Mhe. Karayemaha aliwakabidhi wastaafu hao zawadi, ikiwa ni sehemu ya upendo na shukrani ambazo kwa kipindi cha utumishi wao walikuwa wakidumisha kwa wengine.

Naye Mhe. Madeha aliwaasa kuwa wachamungu na kuwasihi kutumia vizuri fedha za mafao watakazozipata ili ziendelee kuwajenga na kutafakali watazifanyia nini.

“Hongereni sana, kimsingi safari hii ni ndefu, hivyo aliyeifanikisha hii safari ni mungu, mnapaswa kuwa wachamungu. Bila kusahau, fedha mtakazozipata mzitumie vizuri, muwe na malengo nazo ili ziendelee kuwajenga na mtafakari kwa kina nanma ya kuzitumia,” alisema.

Alitumia nafasi hiyo kuwasihi watumishi wote kwa ujumla kujifunza kwa wastaafu hao na kufanya maandalizi ya kustaafu kwa kujishughulisha na shughuli za kijamii na kiuchumi kama kilimo, ufugaji na biashara ili kuweza kujikwamua katika maisha. 

“Tujifunze kwa wenzetu wanaostaafu, kwa kufanya maandalizi, pia mshahara wako uufanyie kitu cha maana, uwe na kitu cha kuonyesha. Tujishirikishe na shughuli zingine za kijamii na kiuchumi, anza kujifunza kilimo, kufuga na biashara,” alisema.

Kwa upande wa ke, Mhe. Nyembele alisisitiza upendo kwani ni agizo kutoka kwa Mungu linasema, ukiwa na upendo huwezi kumkwaza mtu na utamwombea mwenzio anapopatwa na shida au anapolielekea jambo fulani.

 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha akikabidhi zawadi kwa wastaafu (juu na chini).


Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Upendo Madeha akizungumza na wastaafu pamoja na watumishi wa Mahakama Kuu Songea (hawapo kwenye picha.)

Naibu Msajili wa Mahakama Kanda Songea, Mhe. Elizabeth Nyembele akitoa neno fupi kwa wastaafu hao.


Sehemu ya watumishi wakifuatilia kilichokuwa kinajiri wakati wa hafla hiyo.

Wastaafu kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama Kuu Songea (wa pili kutoka kushoto na wa pili kutoka kulia) akiwemo Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha (watatu kutoka kulia.) 

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni