Ijumaa, 24 Mei 2024

ASILIMIA 83 YA IDADI YA WATU WANAPATA HUDUMA ZA MAHAKAMA KUU

 Na Magreth Kinabo-Mahakama

 

Hadi kufikia mwaka 2023, asimilia 83 ya idadi ya watu nchini wanapata huduma za Mahakama Kuu ukilinganisha na asilimia 53 ya mwaka 2015 baada uboreshaji wa upatikanaji wa huduma za kimahakama.

 

Hayo yamesemwa na Mkuu Kitengo cha Maboresho ya Huduma za Mahakama na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania,Mhe. Dkt. Angelo Rumisha  hivi karibuni, wakati akitoa mada kuhusu mradi wa uboreshaji wa huduma za mahakama kwa Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia wa Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbabwe,  Bw. Nathan Beleke kwenye Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki cha Masuala ya Familia na Mirathi (IJC)Temeke jijini Dar es Salaam.

 

Dkt. Rumisha alisema uboreshaji wa huduma za kimahakama kwa kujenga miundombinu ya majengo ya kisasa mfano IJC, kufungua masjala ndogo za Mahakama Kuu Morogoro, Babati na Geita ndiyo imechangia kuwepo kwa idadi kubwa ya watu wanaopata huduma za Mahakama Kuu.

 

“Ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utaji haki Morogoro kumesaidia kuondoa adha ya kusafiri umbali wa kilometa 500 kutoka Mahenge Morogoro hadi Dar es Salaam na kuokoa takribani Tsh. 240,000 ya kipato cha kaya kwenye kesi za madai,” alisema Dkt. Rumisha.

 

Aidha, alisema kuwa ifikapo mwisho wa mwaka 2024, huduma za Mahakama Kuu zitakuwa zimewafikia wananchi kwa asilimia 100 mikoani kwao baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Vituo Jumuishi vya Utoaji Haki katika Mikoa ya Geita, Simiyu, Katavi, Njombe, Songwe, Songea, Singida, Ruvuma na Pemba.

 

Aliongeza kwamba kwa upande wa Mahakama Inayotembea asilimia 90 ya mashauri inawezesha mtu kupata haki yake ndani ya siku 30, ukilinganisha na siku 120 kwenye mahakama ya kawaida.

 

Alifafanua kuwa huduma ya Mahakama Inayotembea hufikia watu 4,131 kati yao 1,920 sawa na asilimia 46 ni wanaume na 2,211 sawa na asilimia 54 ni wanawake. Pia watu hutapata huduma hiyo ndani ya kilometa 5 ukilinganisha kilometa 12-21 kwa mahakama ya kawaida. 

 

Dkt. Rumisha alisema Mahakama pia imeweza kupunguza muda wa usikilizwaji wa shauri kutoka siku linapofunguliwa hadi kutolewa uamuzi kutoka malengo ya siku 800 mwaka 2023 hadi siku 231 mwaka 2023.

Mkuu Kitengo cha Maboresho ya Huduma za Mahakama na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania,Mhe. Dkt. Angelo Rumisha  akitoa mada kuhusu mradi wa uboreshaji wa huduma za mahakama kwa Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia wa Tanzania, Malawi, Zambia na Zimbabwe,  Bw. Nathan Beleke kwenye Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki cha Masuala ya Familia na Mirathi (IJC)Temeke jijini Dar es Salaam.

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni