Na. Innocent Kansha – Mahakama, Pemba
Jaji
Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla amesema mradi wa ujenzi wa Kituo Jumuishi
cha Utoaji Haki Pemba unaenda kuandika histori mpya ya ushirikiano
baina ya Mahakama ya Tanzania na Mahakama ya Zanzibar.
Akizungumza
katika hafla ya utiaji saini Mkataba wa ujenzi wa Kituo hicho iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano katika jengo la Mamlaka ya Mapato
Chakechake Pemba jana tarehe 23 Mei, 2024, Mhe. Abdalla alisema kuwa kwa mara ya
kwanza Mahakama ya Zanzibar imepata msaada mkubwa wa ujenzi wa kituo jumuishi Zanzibar.
Jaji Mkuu huyo aliihakikishia Mahakama ya Tanzania kuwa Mahakama ya Zanzibar kupitia
Pemba ipo tayari kutoa ushirikiano wa hali ya juu kwa kipindi chote cha ujenzi
wa kituo hicho hadi kukamilika kwake na kuanza kutumika. Akamtaka mkandarasi
wakati wa ujenzi akikutana na changamoto zozote aujulishe uongozi wa Mahakama
Zanzibar ili kwa pamoja wazitatue haraka na ujenzi ukamilike kwa wakati
uliokusudiwa.
Aidha,
Mhe. Abdalla alitoa rai kwa Mkandarasi wa ujenzi wa kituo hicho kusimamia
ujenzi huo kwa makini kama mkataba unavyoelekeza na kwamba Mahakama haitarajii
kusikia masuala ya wizi au udokozi wa vifaa vya ujenzi wa jengo hilo.
“Nitoe
ahadi kwamba majengo haya tunayoyajenga sio tu kwa kujengwa na kukamilika pia
tunakusudia kuboresha utendaji kazi wetu wa utoaji haki kwa wananchi kupitia
majengo manne ya kisasa yanayendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali Zanzibar, ikiwemo kituo hiki cha Pemba,” aliongeza Jaji Mkuu.
Mahakama
ya Zanzibar inaendela na mchakato wa kujenga mifumo ya kisasa ya TEHAMA kwa ajili
ya kusikilizia mashauri mahakamani itakayo simikwa katika majengo yote ya
kisasa yanayojengwa Zanzibar ikiwemo kituo hicho.
Mhe. Abdalla alisema Mahakama ya Tanzania na Mahakama ya Zanzibar wapo kwenye
mazungumzo ya kufufua utaratibu wa Majiji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Majiji
wa Mahakama Kuu ya Zanzibar kuwa wanapangiwa kusikiliza mashauri katika pende
zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mhe. Abdalla pia alimshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi kwa kubariki mchakato mzima na kuridhia ujenzi wa
Kituo hicho kujengwa kisiwani Pemba na kwa kuunga mkono Mahakama ya Zanzibar
kwa kiwango kikubwa sana.
Naye, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel alisema Mahakama
imetimiza ndoto iliyokuwa nayo muda mrefu ya kuanza safari ya ujenzi wa jengo
la kituo jumuishi kisiwani Pemba na ujenzi huo umesabishwa na matokeo ya
mahusiano mazuri ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Taasisi za
kimataifa za kifedha. Alisema kuwa rasilimali fedha inayotumika kujenga kituo
hicho inatokana na mkopo wa gharama nafuu kutoka Benki ya Dunia uliochukuliwa
na Serikali ya Tanzania.
“Lengo
la kujenga jengo hili lina mambo makubwa matatu, ikiwemo kutoa pia fursa kwa
wenzetu wa Pemba wawaze kupata huduma hii ya kituo jumuishi kwa kuzingatia
kwamba ngazi zote za kimahakama zinapatikana katika mwanvuli mmoja kwa maana ya
Mahakama ya Mwanzo, Wilaya, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mahakama Kuu na Vikao vya
Mahakama ya Rufani,” alisema Prof. Ole Gabriel.
Prof.
Ole Gabrel aliongeza sababu nyingine ya kujenga kituo hicho Pemba ni
kushajihisha matumizi ya rasilimali katika muktadha wa Muungano ambao hadi sasa
umetimiza miaka 60. "Kwa kuwa mkopo huo ni kwa ajili ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hakuna Jamuhuri ya Muungano bila Zanzibar na
kwa kuwa hata kodi za mrejesho wa mkopo unafanyika na kodi za watanzania, Mahakama ikaona ni jambo jema kuweka alama hiyo ya kumbukumbu ya kuhakikisha
kwamba suala la Muungano linazidi kuendelea...
“Jambo
la tatu ni kuhakikisha kwamba maboresho haya yanayotokea ya Mahakama kwa upande
wa Bara kuwa ni vema pia yakaletwa upande wa pili wa Muungano. Kuwa na jengo
kama hili la kituo jumuishi ni kichocheo kikubwa cha kuweza kuleta miundombinu
ya mifumo ya TEHAMA kama vile Tafsiri na Unukuzi (TTS) na matumizi mengine ya
ki-TEHAMA katika uendeshaji wa mashauri,” aliongeza Prof. Ole Gabriel.
Prof.
Ole Gabriel alisema mchakato wa ujenzi huo umewezekana kutokana na kuwa na timu
nzuri na imara ya maboresho ya Mahakama ya Tanzania upande wa Bara inajulikana
kama Kitengo cha Maboresho ya Mahakama ‘Judiciary Delivery Unit’ (JDU)
inayosimamiwa na Mkuu ya Kitengo cha Maboresho Jaji wa Mahakama Kuu Mhe. Dkt.
Angelo Rumisha.
“Niishukuru
Banki ya Dunia kwa kutuamini na kuendelea kutupa mikopo kama hii ili tueweze
kuboresha miundombinu kwa hali ya juu. Pia nimpongeze Mkandarasi wetu kwa
kupata nafasi hii ya ujenzi wa jengo hili kwani kinyanganyiro kilikuwa ni
kikali na kigumu lakini alikidhi vigezo vyote vya kimataifa ambayo tulikuwa
tunaviitaji,” alibainisha Mtendaji Mkuu
Prof.
Ole Gabriel alitoa rai kwa Mkandarasi huyo wa M/s Deep Construction Limited kwa
kumsisitiza kwamba mradi huo ni wa kipekee na wa kimkakati na akamtaka asifanye
kosa la kushindwa kukidhi kigezo cha ukomo wa muda uliopangwa kukamilika kwa
mradi huo ambao ni tarehe 23 Februari 2025.
“Niwaombe
wakaazi wa Pemba watambue kwamba hii ni heshima ya pekee ambayo Mhe. Rais Dkt.
Hussein Ally Mwinyi amewapa na kuonyesha kuwajali kwa kiasi kikubwa, kwani yeye
ndiye aliyeamua kwamba jengo lijengwe Zanzibar lakini lijengwe Pemba,”
aliongeza Mtendaji Mkuu.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa
Mahakama ya Zanzibar, Bw. Kai Mbaruk alisema, hafla ya utiaji
saini ya ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki na kukabidhi eneo la ujenzi ni
ishara ya kuandika historia mpya na kubwa kwa wananchi wa Tanzania.
“Mkataba
huu uliosainiwa baina ya Mahakama ya Tanzania na Mkandarasi wa ujenzi wa kituo
jumuishi hichi ni ishara tosha ya ushirikiano na utengamano wa wa taasisi hizi
mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Mtendaji Mbaruk.
Bw.
Mbaruk akiongeza kuwa jambo kubwa litakalo fanyika kupitia ujenzi wa kituo hicho
kitajumuisha Mahakama za ngazi mbalimbali lakini pia kitakuwa kinatoa fursa kwa
ajili ya Mahakama ya Rufani ya Tanzania kwani Mahakama hiyo ya juu kabisa
imekuwa ikifanya kazi zake katika kanda mbalimbali nchini Tanzania na kwa
upande wa Zanzibar imekuwa ikifanya vikao vyeke pale kisiwa cha Unguja pekee.
Wananchi wa Pemba wanalazimika kusafiri hadi Unguja kwa ajili ya kufuatilia
mashauri yao.
“Sasa
ujio wa mradi huu wa ujenzi wa kituo jumuishi cha utoaji haki unakwenda
kuwapunguzi shida kwa kiasi kikubwa wananchi wa Pemba lakini pia utaoa nafasi
kwa maana ya mazingira bora ya kufanyai kazi kwa Waheshimiwa Majaji, Mahakamu
na watendaji wengine wa Mahakama Pemba,” alisema Mtendaji Mkuu huyo.
Bw.
Mbaruk alisema jengo la kituo hicho likikamilika litatumia mifumo ya kisasa TEHAMA
ya kuendeshea mashauri yote yatakayosajili mahakamani hii itasaidia kuharakisha
usikilizaji wa mashauri lakini vilevile kuongeza uwazi katika uendeshaji wa
mashauri hayo na kumrahisishia mwananchi ambaye atafika mahakamani kutafuta
huduma ya haki.
“Sisi
kama Zanzibar tunatoa shukrani nyingi kwa Mahakama ya Tanzania kwa kutuletea
mradi huu na Viongozi wakuu wa nchi ambao mara zote wamekuwa wakisisitiza
mashirikiano baina yetu na sasa juhudi hizo zimeonekana na kuzaa matunda,”
alisisita Bw. Mbaruk
Akitoa
maelezo mafupi ya Mradi wa ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kisiwani
Pemba, Mkuu wa Kitengo cha Maboresho ya
Mahakama ya Tanzania na Jaji wa Mahakama Kuu Mhe. Dkt. Angelo Rumisha alisema
Mahakama za pande zote mbili za Muungano na wananchi watashuhudia historia
ikiandikwa tena kwa kusaini mkataba wa ujenzi wa kituo jumuishi cha utoaji haki
Pemba
“Kupitia
picha mjongeo zinazoonekana pale ukutani kwenye ‘Projector’ zinatoa tafsiri ya
kwa nini leo sote tumekusanyika hapa ni historia inayoandikwa katika mstakabali
mzima wa utoaji haki nchini,” alisema Jaji Dkt. Rumisha.
Mhe. Dkt. Rumisha alisema kwa nini kinaitwa
Kituo Jumuishi ni kwa sababu kimekusanya pamoja na kujumuisha Mahakama za ngazi
zote kuanzia Mahakama ya chini mpaka Mahakama ya Rufani na wadau wote muhimu
katika mnyororo wa utoaji haki ili kurahisisha upatikanaji wa haki na kwa kuwapunguzia
gharama na kadha wananchi wanapotafuta haki.
Mhe.
Dkt. Rumisha alisema kutokana na ripoti ya Tume ya haki jinai iliyowasilishwa
kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mnamo mwezi Januari
2023. Kwa upande wa Mahakama ya Tanzania baada ya kuichambua kwa kina ripoti ile
Mahakama ilibainisha mambo 19 ya kufanyiwa kazi ili kuboresha utoaji haki nchini.
Katika maoni hayo moja ilionekana kwamba wananchi wa Pemba walipohojiwa
walisema wanapata kadha ya kusafiri ubali mrefu kufuata huduma za Mahakama ya
Rufani.
Mhe.
Dkt. Rumisha alibainisha kuwa wananchi walisema wangependa Mahakama ya Rufani
iende Pemba na kwamba Mahakama ndiyo taasisi ya kwanza pekee kuanza mara moja
kutekeleza mapendekezo ya ripoti hiyo ya Mhe. Rais.
“Kwa
hiyo ujenzi wa kituo jumuishi Pemba kinakidhi na kutibu kiu ya wananchi wa
Pemba waliosema wanataka kupata huduma za Mahakama ya Rufani. Lakini wakati
kituo kinaendelea kujengwa Mahakama ikajiuliza kwa nini ijengwe Mahakama ya
Rufani peke yake kwani hizo rufaa zinatoka wapi? Tukaona ni hekima kujenga
Kituo Jumuishi kitakacho beba Mahakama zote ikiwemo ya Rufani kama wananchi wa
Pemba walivyosema,” aliongeza Jaji Dkt. Rumisha.
Mhe.
Dkt. Rumisha alisema Kituo Jumuishi hicho kitakuwa na ukubwa wa mita za mraba 3,782
na ghorofa nne pamoja na sakafu ya chini, ni pamoja na jengo kubwa, nyumba za
walinzi, nyumba ya kangavuke ‘Generetor’, Mgahawa na Ofisi mbalimbali za wadau
wa utoaji haki.
“Kituo
Jumuishi cha Pemba kitakuwa cha pekee hapa Visiwani kwanza usanifu wake
umezingatia kanuni za usanifu wa kisasa, pili kituo kitakuwa na Mahakama ngazi
zote pamoja na kusogeza huduma karibu na wananchi pia kitapunguza gharama za
upatikanaji wa haki na kuimarisha uwajibikaji kwa kutumia matumizi makubwa ya
TEHAMA,” alisema Mhe. Dkt. Rumisha.
Mhe.
Dkt. Rumisha alisema mradi huo utakamiliaka kwa kununuliwa samani pamoja na
kuwekewa vifaa vya TEHAMA vya kisasa. Pia mradi huo unajengwa kwa unazingatia
na kufuata taratibu zote za uasalama na mazingira ikiwa ni pamoja na kupata ridhaa
kutoka Mamlaka ya Mazingira Zanzibar.
Mradi
huo utakamiliki kwa gharama ya pesa za kitanzania Bilioni 9,882,759,789.96
gharama hiyo ni pamoja na ongezeko la thamani ‘VET’ pamoja na fedha za dharula.
Hata hivyo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeonesha nia ya dhati ya kusamehe
kodi na tozo kwenye mradi huo. Iwapo hilo litakamilika huo mradi utakamilika
kwa gharama ya Bilioni 7,976,400,153. 53
Kituo
hicho kitajengwa ndani ya miezi tisa (9) bila nyongeza, muda wa ujenzi utaanza
kuesabiwa kuanzia tarehe 23 Mei, 2024 Mkandarasi atakapokabidhiwa kiwanja na mnamo
tarehe 23 Februari, 2025 Mkandarasi atakabidhi jengo.
Mradi
huo unatekelezwa na Mkandarasi M/s Deep Construction Limited na utasimamiwa na
Mkandarasi mshauri Arqes Africa ambaye atakuwa kiongozi wa washauri elekezi wa
mradi.
Aidha,
akitoa salamu fupi za Mahakama ya Tanzania, Msajili
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya alitoa shukrani kwa wadau wote
wa maendeleo wanaosaidia kuiwezesha Mahakama kufanya maendeleo ya maboresho ya
ujenzi wa vituo jumuishi vinavyoendelea kujengwa ili kuboresha utoaji huduma za
kimahakama kwani safari ya maboresho ya Mahakama ilianza 2016.
“Ujenzi
wa Kituo Jumuishi hiki kinachojengwa hapa Pemba kitawasaidia wananchi kupunguza
gharama za kufuata umbali mrefu huduma za kimahakama hasa ngazi ya Mahakama ya
Rufani kwani sasa vikao vitafanyika hapa, kitu ambacho kitamsaidia mwananchi
kutumia muda uliobakia kufanya shughuli nyingine za kimaendeleo za ujenzi wa
Taifa letu,” alisema Mhe. Nkya.
Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla akitoa hotuba wakati wa hafla ya utiaji saini Mkataba wa ujenzi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki kisiwani Pemba iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano katika jengo la Mamlaka ya Mapato Chakechake Pemba jana tarehe 23 Mei, 2024.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni