Ijumaa, 24 Mei 2024

ASKARI JESHI LA WANANCHI PANGAWE WAPATIWA MAFUNZO KUHUSU MIFUMO YA KIMAHAKAMA

Na Evelina Odemba – Mahakama Morogoro

 

Askari 99 Jeshi la Wananchi wa Tanzania walioko kwenye Shule ya Mafunzo ya Huduma kutoka Kituo cha Mafunzo cha Kijeshi Pangawe mkoani hapa wamepatiwa elimu juu ya matumizi ya mifumo mbalimbali ya kimahakama.

 

Elimu hiyo ilitolewa hivi karibuni na Mkurugenzi wa Menejimenti ya Mashauri wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Desdery Kamugisha kwa Askari hao ambao walifanya ziara ya kimafunzo katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro.

 

Mhe. Kamugisha aliwaeleza kuwa kwa sasa Mahakama ya Tanzania imejikita zaidi katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), hivyo kama wadau wa Mahakama ni muhimu kuifahamu mifumo inayotumika na jinsi inavyofanya kazi.

 

Aliwapitisha kwenye baadhi ya mifumo hiyo, ikiwemo E- CMS, TANZLII, E- Wakili, J- Map pamoja na matumizi ya Akili Bandia na kufafanua kuwa maboresho hayo makubwa yaliyofanywa na Mahakama ya Tanzania yamelenga kusogeza huduma ya haki kwa mwananchi.

 

“Kwa sasa mwananchi anaweza kufungua shauri muda wowote na akiwa sehemu yeyote. Pia anaweza kufuatilia hatua za kesi yake kupitia mifumo yetu,” alisema Mhe. Kamugisha.

 

Naye Mkurugenzi Msaidizi kutoka Menejimenti ya Mashauri, Mhe. Moses Ndelwa alisema kwamba licha ya majengo mapya ya Mahakama kuijengwa, kuna huduma ya Mahakama Inayotembea (Mobile Court), hivyo aliwaomba askali hao kuwa mabalozi wazuri kuelezea huduma hiyo ya kimahakama.

 

Kiongozi wa msafara huo, Kapteni Yona Mtaita alisema kuwa ziara hiyo imetokana na somo la Sheria ya Ushahidi ambalo linafundishwa kwa Jeshi la Wananchi ili kupata ufafanuzi wa kanuni za kutoa ushahidi mahakamani.

 

Alisema wanamategemeo baada ya ziara hiyo watapata uelewa juu ya taratibu za Mahakama katika mashauri ya jinai na madai, kinga na utetezi wa kisheria katika makosa ya jinai, uwasilishaji wa nyaraka na vielelezo vya ushahidi mahakamani, haki na utaratibu wa rufaa na tafsiri ya sheria katika utoaji wa haki kwa watuhumiwa wa makosa ya jinai.

 

Walipowasili kituoni hapo, wanajeshi hao walipokelewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Morogoro, Mhe. Mary Kallomo ambaye aliwatembeza katika maeneo mbalimbali. 


 

Mkurugenzi wa Menejimenti ya Mashauri wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Desdery Kamugisha akitoa elimu ya mifumo ya Mahakama kwa Askari wa Jeshi la Wananchi (hawapo pichani).


 

Mkurugenzi Msaidizi kutoka Menejimenti ya Mashauri, Mhe. Moses Ndelwa akitoa elimu ya matumizi ya Mahakama Inayotembea kwa Askari wa Jeshi la Wananchi (hawapo Pichani).


 

Kaimu Afisa TEHAMA toka Mahakama ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Bw. Tofiki Sumbuo akiwaeleza Askari wa Jeshi la Wananchi juu ya matumizi ya Mfumo wa Akili Bandia unaotumika wakati wa kusikiliza mashauri.

 


Askari wa toka Jeshi la Wananchi wakifuatilia mada mbalimbali toka kwa wawezesha wakati wa ziara yao.


  

 

  

 

  

 Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Morogoro, Mhe. Mary Kallomo (wa saba kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania waliofika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro kwa ziara ya mafunzo (juu na chini).



(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni