Jumatano, 22 Mei 2024

WATUMISHI WA MAHAKAMA KATAVI WAPIGWA MSASA MFUMO WA TAARIFA ZA WATUMISHI, MISHAHARA

Na. James Kapele – Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi

Watumishi wa Mahakama  Mkoa wa Katavi wamepata mafunzo ya namna bora ya matumizi ya Mfumo wa Taarifa za Watumishi na Mishahara unaojulikana kitaalam kama (Employment Self Service -ESS).

Mafunzo hayo yamefanyika leo tarehe 22 Mei, 2024 katika ukumbi wa Mahakama ya wazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi, ambayo yaliendeshwa na maafisa kutoka Ofisi ya Rais -Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kushirikiana na maafisa wengine kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda.

Lengo la mafunzo hayo ni kuongeza uelewa kwa watumishi kuhusu matumizi ya mfumo huo pamoja na kutatua changamoto mbalimbali ambazo watumishi wanakutana nazo katika matumizi ya mfumo.

Akizungumza wakati anafungua mafunzo hayo, Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Katavi, Bw. Allan Mwela aliwaomba washiriki katika mafunzo hayo kushiriki kikamilifu ili kuondoa changamoto ambazo watumishi wamekuwa wakikutana nazo katika matumizi ya siku kwa siku ya mfumo huo.

“Mafunzo haya ni muhimu sana kwetu na hii fursa ni adhimuhivyo ni vyema tukaitumia ipasavyo ili kuondoa changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikitukwamisha pindi tunapotumia mfumo huu,alisema.

Akitoa mafunzo hayo, Afisa Utumishi kutoka Ofisi ya Mkurugenzi, Bi. Bahati Kyando amesema mfumo huo ni mpya, hivyo wataalamu wanaendelea kupokea maboresho mbalimbali yanayotoka kwa watumiaji ili kuufanya uwe rafiki kwa watumiaji na kuleta zaidi tija kwa Serikali na watumishi wake.

“Kuweni huru kutoa maoni hasa yale ambayo mnafirikiri yanahitaji maboresho ili na sisi tuyafikishe kwa wataalam wetu ili waendelee na maboresho ya mfumo uweze kuleta tija na ufanisi zaidi,” alisema.

Mafunzo hayo yamefanyika kwa kupitia madirisha yote yaliyopo kwenye mfumo huo kwa vitendo na kuonyesha namna bora ya matumizi ya madirisha hayo, yakiwemo yale ya Upimaji wa Utendaji Kazi wa Watumishi(PEPMIS), likizo na mingineyo. 

Aidha watumishi wameomba mafunzo hayo kutolewa mara kwa mara ili kuongeza ufanisi katika kutumia mfumo huo.


Pichani aliyesimama ni Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Katavi, Bw. Allan Mwella alipokuwa akifungua mafunzo hayo.

Katika picha ni Bi. Bahati Kyando alipokuwa akitoa mada katika mafunzo hayo.

Pichani ni sehemu ya watumishi wa Mahakama Mkoa wa Katavi wakifuatilia mafunzo hayo. Aliyeketi kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi, Mhe. Gway Sumaye akiwa sehemu ya washiriki wa mafunzo hayo.

Katika picha aliyesimama ni Mkurugenzi Ofisi ya Rais -Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Bernard Makhanda alipokuwa akifafanua jambo katika mafunzo hayo.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni